Waziri Mkuu Mizengo Pinda
Waziri Mkuu Mizengo Pinda na Spika Anne Makinda(Kushoto) wakitazama vifaa vya maabara muda mfupi baada ya Waziri Mkuu Kuzindua Meza ya Maabara inayohamishika kwenye viwanja vya Bunge Mjini Dodoma Jana.Picha na Ofisi Ya Waziri Mkuu
Waziri Mkuu Mizengo Pinda na Spika Anne Makinda(Kushoto) wakitazama vifaa vya maabara muda mfupi baada ya Waziri Mkuu Kuzindua Meza ya Maabara inayohamishika kwenye viwanja vya Bunge Mjini Dodoma Jana.Picha na Ofisi Ya Waziri Mkuu
-----
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema wakati Serikali inajipanga kutekeleza mpango wa kuimarisha masomo ya sayansi shuleni, meza ya maabara inayohamishika inaweza kutumika kupunguza tatizo la uhaba wa maabara katika shule za sekondari nchini.
Ametoa kauli hiyo jana mchana(Jumatano, Julai 20, 2011)mara baada kuzindua rasmi meza ya maabara inayohamishika (mobile science laboratory table with equipment) kwenye viwanja vya Bunge mjini Dodoma.
“Kama nchi tuna shida ya kuimarisha fani ya masomo ya sayansi,Serikali imejipanga kwa ujenzi wa maabara kila mkoa lakini ni mpango ambao utachukua muda mrefu kukamilika … tulianza kuonyeshwa science kits hapa Bungeni zile zilikuwa ni ndogo sana ikilinganishwa na hii meza,”alisema.
“Hii meza imejitosheleza inaweza kuruhusu wanafunzi wane wafanye majaribio au mitihani kwa pamoja…inaweza kutumika kwa masomo ya fizikia,kemia na bailojia.Na uzuri wake inaweza kuhamishwa na kupelekwa katika shule nyingine kwa matumizi yaleyale kama vifaa vikitunzwa vizuri,”alisisitiza.
Alisema wakati Serikali inaendelea na mpango wake, ni dhahiri kuwa kuna shule zaidi zitakuwa zinajengwa na ambazo hazikuwemo katika mpango huo.Pia alibainisha kwamba endapo shule moja itakuwa imekalimisha ujenzi wa maabara zake,meza hizo zinaweza kutumiwa na shule za jirani ambazo zitakuwa hazijafikiwa katika mpango wa ujenzi wa maabara wa Serikali.
Alisema yeye amekwishanunua meza tisa hadi sasa na kusizambaza jimboni kwake kupitia mfuko wa maendeleo wa jimbo na akashauri wabunge watumie fursa ya mfuko huo kununua meza za maabara zinazohamishika kwa ajili ya shule za majimboni kwao.
“Tangu hawa watu wameanza mpango huu miaka miwili iliyopita ni meza 59 tuzimekwishanunuliwa zikiwemo hizi tisa tulizochukua..kama Halmashauri zingechangamkia fursa hii, baadhi ya shule zingeweza kufundisha watoto wetu masomo ya sayansi,”alisema.
Alisema aliiomba kampuni hiyo ije kufanya uzinduzi rasmi bungeni ili wabunge wazione meza hizo na waweze kupeleka ujumbe kwenye Baraza la Madiwani ambako nao ni wajumbe.
Pia alitumia fursa hiyo kufafanua kauli ya Spika,Anne Makinda ambaye alikuwepo katika uzinduzi huo na kushauri kwamba ingefaa uandaliwe mfumo wa mikopo ya meza hizo ili wabunge wakopeshwe halafu malipo yake yakatwe kutoka kwenye posho zao.
Mapema,akisoma risala kwa Waziri Mkuu,Mwenyekiti Mtendaji wa kampuni ya ML Group ambayo imebuni na kutengeneza meza hizo,Bw.Emmanuel Makubi alisema gharama ya meza moja ni sh. 5,980,000/- na kwamba gharama hiyo inajumuisha usafirishaji hadi mahali shule ilipo. Meza hiyo ina urefu wa futi saba na nusu na upana wa futi mbili na nusu.
Alisema gharama hizo pia zinajumuisha vifaa 96 vya maabara kwa ajili ya masomo yote matatu ya fizikia,kemia na baiolojia lakini hazijumuishi kemikali za maabara(chemical reagents)bali wahusika wanaweza kuchangia gharama na wao wakawasaidia kuwapatia kemikali za kuanzia.
Bw. Makubo alisema kuwa wameenda katika halmashauri mbalimbali nchini baada ya meza hiyo kupewa kibali na Wizaya ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ili itumike shuleni yaani EMAC lakini mwitikio umekuwa mdogo sana.Pia walipata baraka za TAMISEMI kupitia barua ambayo Naibu Katibu Mkuu(Elimu)aliwaandikia Makatibu Tawala wa Mikoa Novemba 11, 2010.
Alizitaja halmashauri ambazo zimeitikia wito huo ni Temeke(meza 20),Kinondoni(10), Kigoma(5),Ulanga(3),Mvomero(2)na shule binafsi kadhaa(meza 7).Alisema wabunge walionunua meza hizo ni Waziri Mkuu meza tisa na mbunge wa Kindondoni, Bw. Iddi Azzan meza tatu.
Uzinduzi huo ulihudhuriwa na Spika,baadhi ya Naibu Mawaziri,baadhi ya wabunge na wanafunzi kutoka shule za sekondari za Zanaki(Dar es Salaam)na Dodoma Sekondari ya Dodoma.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
DODOMA
No comments:
Post a Comment