Moto mkubwa ambao chanzo chake bado ni kitendawili kigumu kwa wakazi wa Manispaa ya Iringa umezuka katika nyumba ya mfanyabiashara wa mchele katika eneo la Frelimo 'A' katika manispaa ya Iringa Bw.Alfred Mbwilo maarufu kwa jina la Emerro huku familia yake ya watoto saba ikinusurika kuteketea kwa moto huo.
Tukio hilo limetokea usiku huu majira ya saa 2 hadi saa 3 za wakati familia ya mfanyabiashara huyo maarufu wa mchele ikiwa sebuleni ikiendelea kujisomea.
Mtoto mkubwa katika familia hiyo Roida Mwinuka (22) na Remsi Mbwilo wameueleza mtandao huu wa www.francisgodwin.blogspot.com kuwa moto huo ulianza kuwaka katika chumba cha wageni katika nyumba hiyo yenye vyumba zaidi ya vitano .
Walisema kuwa wakati moto huo ukianza walikuwa pamoja sebuleni wakijikumbusha masomo mbali mbali na kuendelea na stori za hapa na pale kama ilivyo siku zote.
Hata hivyo walisema waki hawana hili wala lile ghafla walishangazwa kuhisi joto kali ndani ya sebule hiyo na baada ya kutaka kufungua madirisha ndipo waliposhuhudia mwanga mkali nje na tayari wananchi wamekusanyika nje ya nyumba hiyo kwa ajili ya kutaka kuvunja nyumba ambayo tayari ilikuwa imepata kushika moto .
Walisema kuwa kutokana na hali hiyo walilazimika kutoka nje na kuungana na wananchi hao kuzima moto huo huku baadhi ya wananchi wakiwasiliana na gari ya zima moto ambayo bila kuchelewa ilifika eneo hilo na kusaidia kuzima moto huo.
Alitaja waliokuwemo ndani ya nyumba hiyo kuwa ni pamoja na Teddy Shedracky (16)Remsi Mbwilo (19), Roida Mwinuka (22),Tito Mbwilo(8), Sebastian Mbwilo (6), Abigaili Mbwilo (1) na Vicky Mbwilo(12) ambao wote walitoka salama katika nyumba hiyo.
Hata hivyo alisema kuwa wasamaria wema ambao swalikuwepo eneo hilo mbali ya kunusuru maisha yao pia walipata kuliokoa gari dogo aina ya Saloon ambalo lilikuwa limefungiwa katika nyumba hiyo.
Wakati huo huo wananchi wenye hasira kali nusuru wamchome moto kijana mmoja ambaye alidaiwa kuiba mali mbali mbali katika eneo hilo ,mali ambazo zilikuwa zikiokolewa ndani ya nyumba hiyo na kibaka huyo kuzifaulisha kutaka kuzificha vichakani eneo hilo.
Pona na kibaka huyo ni gari ya zima moto na askari wa kikosi cha Zimamoto ambao walimuokoa kutoka mikononi mwa wananchi wenye jazba kali na kumficha katika gari hilo.
Tayari jeshi la polisi mkoa wa Iringa kupitia kamanda wa polisi mkoa Evarist Mangalla limepata kuthibitisha tukio hilo la moto kuteketeza nyumba hiyo.
No comments:
Post a Comment