Thursday, August 18, 2011

CHAMA CHA CHADEMA SONGEA CHAPATA KATIBU MPYA WA JIMBO



Na,Stephano Mango,Songea
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma kimempata Katibu mpya wa Jimbo la Songea Masumbuko Paulo katika uchaguzi wa wanachama wa chama hicho uliofanyika jana katika Ofisi ya Kata ya Mfaranyaki

Akitangaza matokeo hayo Mwenyekiti wa Jimbo hilo ambaye pia ni Diwani wa kata ya Majengo mjini hapa Idd Abdalah alisema kuwa wanachama waliopiga kura ni 80 ambapo Masumbuko Paulo amepata kura 54,Ajaba Nditi alipata kura 18, Zuber Tindwa alipata kura 8 ambapo Christopha Nyoni alipata kura 0

Abdalah alimtangaza Masumbuko Paulo kuwa ndiye ameibuka mshindi wa kwanza na hivyo kuanzia hapo anakuwa Katibu mpya wa Jimbo hilo na kwamba anatakiwa kuanza kazi mara moja ili kuweza kuendana na kasi ya chama hicho

Awali Mwenyekiti huyo aliwaambia wajumbe kuwa nafasi hiyo ya Ukatibu ilikuwa wazi kutokana na aliyekuwepo katika nafasi hiyo kuiacha na kwenda kufanya kazi kwenye Mashirika yasiyoya kiserikali

Alifafanua zaidi kuwa katika uchaguzi huo Wagombea walikuwa watano ambapo mgombea Said Ligema aliamua kujitoa dakika za mwisho za uchaguzi jambo ambalo viongozi wa Wilaya walikubaliana na uamuzi wake huo

Akiwashukuru wajumbe kwa kumchagua Masumbuko Paulo alisema kuwa imani na dhamana waliyompa ni kubwa sana hivyo atakitumikia chama kwa uadilifu mkubwa ili kiweze kupata ushindi stahiki katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa na chaguzi zingine zijazo

Masumbuko alisema kuwa Chama kipo katika harakati kubwa za kujiimalisha maeneo ya pembezoni mwa miji na vijijini hivyo kazi hiyo ya kujikita maeneo hayo kwa lengo la kukisambaza chama ni jukumu la wananchama wote wenye mapenzi ya dhati na chama hicho

Akifunga mkutano huo wa uchaguzi Mwenyekiti wa Chama hicho Wilaya ya Songea Peter Mboya alisema kuwa wanachama ndio nguzo stahiki ya chama chochote duniani hivyo ni vema popote pale alipo mwanachama anatakiwa afanye jambo kwa maslahi ya chama

Mboya alisema kuwa muda wa mabadiliko ya kitaifa umefika ambapo chama hicho kinatakiwa kuchukua dhamana ya kuwaongoza watanzania hivyo ni vema tukaonyesha kwa dhata mbele ya wananchi kuwa tunaweza kuwaondoha hapa walipo katika kipindi hiki cha miaka 50 ya uhuru na kuwapeleka katika hali nyingine ya ustawi wa maisha yao

No comments: