Philemon Luhanjo
Yaliyomo kwenye ripoti ya ukaguzi wa tuhuma zinazomkabili Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini aliyesimamishwa kazi, David Jairo, hadi sasa hayajulikani, kutokana na Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi, kushindwa kuweka ripoti hiyo hadharani.
Ukaguzi wa tuhuma hizo, ambazo Jairo anadaiwa kuchangisha fedha ili kuwashawishi wabunge kupitisha bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2011/2012, ulifanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa siku kumi mfululizo.
Ukaguzi huo kwa mujibu wa aliyekuwa Kaimu CAG, Jumaa Mshihiri, ulianza rasmi Julai 26, mwaka huu.
Ulikamilika Agosti 4 na ripoti hiyo ilikabidhiwa kwa Katibu Mkuu Kiongozi, Agosti 9, mwaka huu.
Hata hivyo, kuanzia wakati huo, Luhanjo amekuwa ama akikwepa kujibu lini ripoti hiyo itawekwa hadharani au akitoa majibu yanayoonyesha uwezekano wa suala hilo kuwa ni ndoto.
Mara ya kwanza, NIPASHE iliwasiliana na Luhanjo kwa njia ya simu na alipoulizwa lini ripoti hiyo itawekwa hadharani, alikataa kuzungumzia suala hilo kwa maelezo kwamba yuko kwenye kikao.
NIPASHE iliendelea kumtafuta na kila ilipofanikiwa kupata simu yake, ilikuwa ikipokelewa na mtu, ambaye mara zote alidai kuwa Luhanjo yuko kwenye kikao.
Juzi NIPASHE kwa mara nyingine ilifanikiwa kumpata Luhanjo kwa njia ya simu, alipoulizwa lini ripoti hiyo itawekwa hadharani, alijibu kwa ufupi: “Itakapokamilika tutawaita (waandishi wa habari) wote.” kisha akakata simu.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment