Na Tiganya Vincent- MAELEZO- Morogoro
Jumla ya mikoa 11 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatarajiwa kushirikia katika sensa ya majaribio ya watu ma Makazi itakayoanza Septemba 4 mwaka huu. Kauli hiyo ilitolewa leo mjini Morogoro na Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dr. Albina Chuwa wakati akitoa maelezo mafupi kabla ya kumkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Kanali Mstaafu Issa Machibya ili aweze kufungua mafunzo ya wiki moja ya wakufunzi wa Sensa ya majaribio yanayofanyika mkoani humo. Alisema katika sensa hiyo ya majaribio jumla ya kaya zipatazo elfu tano(5,000) kutoka mikoa tiza ya Tanzania bara na miwili ya Tanzania Visiwani zitahusika katika zoezi la majaribio ya sensa yanayoanza tarehe mwezi Septemba mwaka huu. Dr. Chuwa alitaja mikoa itakayoshiriki katika Sensa ya majaribio kuwa ni Dar es salaam, kilimanjaro, Njombe, Mara, Arusha, Manyara, Mtwara , Kigoma na Pwani kwa upande wa Visiwani ni Mjin Magharibi na Kaskazini Pemba. Alisema kuwa mara baada ya kukamilika kwa Sensa ya Majaribio Ofisi ya Takwimu kwa kushirikiana na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Zanzibar itakaa na wadau mbalimbali kwa ajili ya kuboresha changamoto mbalimbali zilizojitokeza katika zoezi la majaribio ikiwa ni maandalizi ya Sensa yenyewe hapo
Agosti mwaka 2012. Aidha Mkurugenzi Mkuu huyo alisema kuwa katika Sensa yenyewe itakayofanyika hapo mwakani(2012) , zoezi hilo linatajarijia kukusanya taarifa ambazo hazijawahi kukusanywa ikiwa ni pamoja na idadi ya vifo vinavyotokana na uzazi, maswali kuhusu watu wenye ulemavu , hali ya umaskini usio wa kipato na watanzania wanaosihi nje ya nchi(diaspora). Aliongeza kuwa hadi hivi sasa maandalizi ya sensa ya watu na makazi kwa ajili ya mwaka 2012 imekamilika kwa asilimia 80 sawa na mikoa 18 ya Tanzania.
Kwa upande wa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Kanali Mstaafu Issa Machibya alitoa kwa wakufunzi kutumia mafunzo watakayopata ili kuhakikisha kuwa wanakuwa mabalozi na walimu mahiri katika kusambaza taaluma watakayopata kwa walengwa itakayotoa taarifa sahihi. Alisema kinyume cha hapo wanaweza kusababishia madhara na gharama kubwa Serikali na Taifa kwa ujumla kwa sababu ya uzembe unaoweza kuharibu maana nzuri ya sensa kwa manufaa ya Watanzania kwa ajili ya kizazi cha sasa na kijacho. Kanali Mstaafu Machibya alisema kuwa kukamilka kwa zoezi la majaribio itakuwa ni mwongozo wa kutathmini changamoto zilizojitokeza kwa ajili ya kuboresha maandalizi ya Sensa ya watu na makazi ya hapo mwakani.
Hivyo basi alisema kuwa ni jukumu la vyombo vya habari kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu katika kuhakikisha kuwa zoezi la majaribio na hatimaye Sensa yenye inafanikiwa kwa ajili ya kusaidia Serikali kupanga shughuli mbalimbali za maendeleo ya wananchi. Sensa ya watu na makazi ya majaribio itafanyika kuanzia Septemba mwaka huu lakini Sensa kamili itafanyika mwakani. Sensa ya mwakani itakuwa ya tano tangu uhuru ambapo ilifanyika mwaka 1967,1978,1988, na mwaka 2002.
|
No comments:
Post a Comment