Ndugu zangu,
Hii ni simulizi ya kusikitisha na yenye kutia faraja pia.Maana, jana pale Njombe, kulifanyika harusi yenye mchanganyiko wa furaha na huzuni kama ya msibani. Na harusi ile inatukumbusha wanadamu umuhimu wa kujiuliza swali hili; Nini maana ya maisha kwetu?
Naam, jana Jumamosi, saa chache kabla bwana harusi hajaingia kanisani, nilipata bahati ya kuongea nae kwa simu nikiwa Iringa mjini. Anaitwa Freddy Kihwele. Freddy ni kama mdogo wangu. Nimemfahamu tangu mwaka 2005 akiwa masomoniChuo Kikuu Cha Tumaini hapa Iringa. Freddy ana digrii ya Journalism, uandishi wa habari.
Freddy ananisumulia kilichotokea siku nne zilizopita eneo la Nyororo, kilomita 45 kutoka mji wa Mafinga. Ilikuwa inakaribia saa moja usiku. Kwenye gari ndogo walilopanda kulikuwa na watu watatu; Freddy, Lonjino ( Mfanyakazi mwenzake) na shemeji yake. Walitokea Dar kufanya manunuzi ya harusi yake na mpendwa wake Bi. Upendo.
Mara, wakaliona lori la mafuta linateremka mlima likitokea Nyororo. Tenki la nyuma likakatika na kushuka peke yake likielekea upande wa akina Freddy. Dereva akajitahidi kulikwepa. Katika kurudi tena barabarani akayakuta matuta magumu ya barabarani pale Nyororo.
Katika mshtuko na kasi ile ya kurudi barabarani na kuyavaa matuta, gari ya akina Freddy ikapinduka mara nne. Kwamba wote watatu wametoka hai wakiwa na majeraha tu inabaki kuwa ni miujiza ya Mungu na miungu yao.
Na kuna watu wabaya. Walifika mahali hapo na kuiba kila kitu, pamoja na simu za majeruhi.
Kubwa la kufurahisha; Freddy na Upendo wake wamefunga ndoa jana Jumamosi. Nami nikamwambia Freddy jana ile; " Na uwe na furaha kubwa katika Siku yako hii kuu maishaini. Maana, ukweli kuwa u-hai na unapumua, na kuwa unafunga ndoa na mpenzi wako, basi, hiyo ni zawadi kubwa uliyotunukiwa na Mungu wako. Mshukuru Mungu wako, basi."
Habari kwa Hisani ya Mjegwa Blog
No comments:
Post a Comment