Friday, August 12, 2011

Sugu alipua bomu Bungeni


Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi maarufu kama Mr II 'Sugu', amesema jina la Rais Jakaya Kikwete litachafuka na kuonekana kuwa anafanya kazi chini ya maslahi ya watu binafsi badala ya umma, kama studio aliyoahidi kiongozi huyo mkuu wa nchi kwa ajili ya kusaidia wasanii itabaki mikononi mwa taasisi binafsi ya Nyumba ya Vipaji ya THT.
Aidha, Sugu alihoji uhalali wa nyumba iliyotolewa na serikali kwa ajili ya studio hiyo kugeuzwa kuwa makao makuu ya THT wakati akiwasilisha bungeni bajeti ya Kambi ya Upinzani ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo kwa mwaka 2011/2012 mjini Dodoma jana.

'Kambi ya Upinzani inapendekeza kuwa studio na nyumba hiyo iliyotolewa na Rais viwe chini ya Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), kwa manufaa ya wasanii wote si THT peke yao kama ilivyo sasa,” alisema na kuongeza kuwa:
“Tunatadharisha kuwa hili lisipozingatiwa jina la Rais na hadhi ya urais itachafuka kwa kuonekana kufanya kazi kwa maslahi ya watu binafsi (THT), badala ya kufanya kazi kwa maslahi ya umma (wadau wa sanaa),” alisema.
Sugu alisema Rais Kikwete kupitia Bunge alitangaza kuwa amewapa wasanii studio ya kufanyia kazi zao.
Hata hivyo, alisema baadaye wananchi na wadau wengi wa sanaa akiwemo yeye alishangaa kusikia kuwa studio hiyo wamepewa shirika lisilo la kiserikali (THT).
Alisema Rais aliahidi kutoa nyumba ya serikali kwa wasanii ambayo ingetumika kuendeshea studio husika, lakini nyumba hiyo ya serikali iliyotolewa na Rais sasa iko chini ya THT na ndio makao makuu ya THT.
“Kambi ya upinzani inahoji kwanini ahadi hizo zitolewe kwa kikundi kimoja tu cha THT, tena kilichojikita zaidi katika biashara ya kazi za sanaa, wakati ahadi hizo za Rais zililenga wasanii wote wa Tanzania?” alihoji.
Alisema kambi rasmi ya upinzani inatambua na kuthamini mchango wa THT katika sekta ya sanaa ya nchi, lakini si kwa taasisi hiyo ya binafsi kupewa jukumu la kuhodhi studio na nyumba iliyotolewa na Rais kwa ajili ya wasanii wote.
Alisema Kambi ya Upinzani ina taarifa kuwa mwenyekiti wa bodi ya wadhamini na wanachama waanzilishi wa Nyumba ya Sanaa ilifutwa na baadhi ya wajumbe wake waleta mwekezaji ambaye wameshaingia naye ubia kimkataba kwa ajili ya kujenga jengo la ghorofa katika eneo lenye jengo la sasa.
'Izingatiwe hapa kuwa mwekezaji atapaswa kulivunja na kubadilisha mfumo wa jengo la sasa la nyumba ya sanaa ndipo aweze kujenga ghorofa.
'Kambi ya upinzani na bunge inataka kujua yafuatayo: Kujua kuwa nyumba ya sanaa hivi sasa inawanufaisha wachache na sio walengwa waliokusudiwa.
'Tunataka kufahamu wanufaika hawa hawana rekodi ya uwekezaji katika nyumba ya sanaa, hivyo wanavuna matunda yaliyopandwa na wengine hasa kupitia ushirikiano mwema baina ya serikali ya Tanzania na kupitia Ikulu, kupitia nchi ya Norway kupitia shirika la Norad na Uholanzi kupitia shirika la Novib. Tutambue kwamba nyumba ya sanaa ilikuwa ni mlango wa soko la sanaa na kazi za mikono, hivyo kutokuwepo kwake kunakwamisha juhudi za wazalishaji wa sanaa,' alisema Sugu.
Aidha, alisema lengo la kuanzishwa kwa THT ni kutoa mafunzo ya sanaa kwa vijana na wanawake na wasiojiweza pamoja na kutafuta masoko ya sanaa na kazi za mikono.
Sugu pia ilitaka viwanja vyote vya michezo ambavyo vinamilikiwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) katika maeneo mbalimbali nchini, virejeshwa serikalini ili viboreshwe na kutumika kwa maslahi ya Watanzania wote.
Alivitaja baadhi ya viwanja hivyo kuwa ni Uwanja wa Majimaji (Songea), Sheikh Amri Abeid (Arusha), Uwanja wa Jamuhuri (Morogoro ), Uwanja wa Jamuhuri (Dodoma), CCM Kirumba (Mwanza).
Sugu aliitaka pia serikali pia ijenge kiwanja kimoja kila mwaka chenye hadhi ya kimataifa ili baadaye Tanzania iweze kuandaa mashindano makubwa ya Afrika.
Akichangia Mbunge wa Dimani (CCM) Abdallah Sharia Ameir, alitaka kuanzishwa viwanja vya michezo katika maeneo mbalimbali na kuitaka serikali kuvisimamia.
Mbunge wa Uzuni (CCM), Mohamed Seif Khatibu, alisema kuwa michezo ni afya inayowawezesha watu kufanya kazi vizuri hivyo alitaka serikali kuendelea kuwekeza katika viwanja vya michezo nchini sambamba na kutafuta walimu bora wa michezo ambao watawafundisha wanamichezo.
Mbunge wa Masasi (CCM), Mariam Kasembe, alitaka viwanja vya michezo kujengwa katika shule za kata ili wanafunzi waweze kushiriki katika michezo.
Mbunge wa Singida Magharibi (CCM), Mohamed Missanga, alihoji kuhusiana na usalama wa Uwanja wa Taifa wa Jijini Dar es Salaam kwa kuwa lifti iliyopo katika sehemu ya wageni mashuhuri imeharibika.
Alisema kuwa mlango wa kutokea uliopo ni mmoja na hivyo kuleta hali ngumu kwa watazamaji pindi inapotokea dharura kama ile ya kukosekana kwa umeme kwenye fainali ya Kombe la Kagame.
CHANZO: NIPASHE



No comments: