Friday, April 27, 2012

Neno La Leo: Bunge Ni Eneo La Umasikini!


 Ndugu zangu,
Hapo juu  ni nyumba ya Waziri Maige na chini ni nyumba ya kabwela Mtanzania. Na Spika wa Bunge, Anne Makinda alipata kutamka, kuwa Bunge ni eneo la umasikini. Astaghafilulahi! Haki ya Mungu, ukistaajabia ya Mussa utayaona ya Firauni.

Na jana, bila haya, Waziri Maige amekaririwa akiyasema haya; 

"Akizungumza na gazeti hili jana, Waziri Maige alisema hakununua nyumba hiyo kwa Dola 700,000 kama inavyodaiwa, bali alinunua kwa Dola za Marekani 410,000.

Mbali ya kukiri, alifafanua jinsi alivyoinunua na kuonyesha nyaraka mbalimbali huku akieleza kuwa sehemu ya fedha alizonunulia, zilikuwa za mkopo kutoka Benki ya CRDB.

Alisema mwaka 2005 alipoanza kuwa mbunge alipata mkopo na yeye na wenzake watatu, waliunda kampuni ya kusafirisha mzigo ya Splendid Logistic na kuanza kununua magari matatu na baadaye magari hayo yaliongezeka na kufikia saba.

Waziri wa Maliasili na Utalii,Ezekiel Maige

Alisema Septemba, 2010 mwenzao mmoja alijitoa katika kampuni hiyo na hivyo wakaamua kugawana mali kwa kuzingatia mtaji wa kampuni. Alipata magari mawili na mwenzake manne na kuongeza kuwa gari moja kati ya hayo saba lilipata ajali.

Alisema baada ya hapo aliamua kuanzisha kampuni nyingine ya kusafirisha mizigo ambayo inaendeshwa na mke wake... “Kampuni hiyo inaitwa Mem Logistic na ina magari mawili.”

Alisema magari hayo aliyakodisha kwa kampuni nyingine ya Bravo Logistic ambayo kila mwezi inamlipa Dola 20,000.

Alisema alipochaguliwa tena kuwa mbunge mwaka 2010 aliamua kutoongeza magari katika kampuni yake na kuanza kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa nyumba.

“Baada ya uchaguzi nilichukua mkopo wa Sh200 milioni katika Benki ya CRDB, baadaye Ofisi ya Bunge ilinikopesha Sh90 milioni kwa ajili ya kununua gari, fedha hizo zote nilizichukua na kuzihifadhi,” alisema Maige.

“Hizo fedha nilikaa nazo nikawa nataka kujenga nyumba baadaye nikaona nitafute nyumba ya kununua tu. Baadaye dada yangu, Angelina Ngarura ambaye ana kampuni ya kuuza matrekta, Dar es Salaam alinifuata na kuniomba fedha hizo kwa ajili ya kuzizungusha na tukakubaliana kuwa atakuwa akilipa riba ndogo kwa makubaliano kwamba siku yoyote nikizihitaji nitazichukua,” alisema.

Alisema ndipo alipopata nyumba iliyokuwa ikiuzwa Dola 450,000 lakini alikubaliana na muuzaji na kuuziwa kwa Dola 410,000.

Alisema katika ununuzi huo, hakuwa na kiasi hicho cha fedha kwani nyingine zilikuwa katika mzunguko katika kampuni ya dada yake na hivyo kuamua kwenda kukopa Dola 200,000 katika CRDB.

Alisema baada ya kupewa fedha hizo za mkopo, hati ya nyumba hiyo ilibaki benki kwa makubaliano kwamba akishindwa kulipa, benki itaichukua.

“Tuliingia mkataba na CRDB kulipia nyumba ile kwa miaka minne na mpaka sasa hivi nalipia Dola 5,127 kila mwezi, haya yote yapo kwa Kamishna wa Maadili,” alisema Maige.

Huku akionyesha mikataba ya ununuzi wa nyumba hiyo, nyaraka za mkopo wa benki, Maige alisema awali, alikuwa na magari mawili ambayo aliamua kuyauza na kununua gari nyingine aina ya BMW kwa Sh70 milioni.

Alidai kwamba kama kuna mali kinyume na hizo yuko tayari kuapa hata kwa Biblia Takatifu na kusisitiza kuwa hivi sasa kuna mapambano ya kisiasa ndiyo maana shutuma dhidi yake zinaibuka kila kukicha.

“Ukisikia mali zangu tofauti na hizo ni uongo ndugu yangu na kwa mkopo niliochukua wakati nikiwa mbunge sina hela mpaka Juni 2015,” alisema na kuongeza:
“Nikijiuzulu ubunge leo hii maana yake ni kwamba itakuwa kazi kweli na sitaweza kulipa mkopo. Sijakopa kwa kivuli cha ubunge wangu, nimekopa kama Maige kwa sababu kiwango cha kukopa bungeni nimeshakimaliza.”  
( Mwananchi, Aprili 26, 2012)

Swali la Watanzania wengi ni hili; " Hivi Rais anasubiri nini kupangua Baraza lake la Mawaziri?"
 Na hilo ni Neno La Leo:
Maggid Mjengwa.

No comments: