NA MAGRETH KINABO – MAELEZO SERIKALI imesema iko katika mchakato wa kuangalia upya gharamaza uendeshaji wa shule ili kupata gharama halisi ya kusomesha mwanafunzi mmoja kwa mwaka ili kuweza kutoa mwongozo kuhusu kiwango cha ada kwa shule za serikali na binafsi .Aidha imesema kuwa gharama hizo zitaendana na hali halisi ya uendeshaji wa shule kwa sasa. Kauli hiyo ilitolewa jana Bungeni mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum (CHADEMA) Christina Mughwai lililouliza kuwa je serikali inachukua hatua gani kwa baadhi ya shule binafsi ambazo hazikidhi vigezo vya kusajiliwa na kulazimisha wazazi kuchangia michango mbalimbali ya ada. Pia ni kwa nini serikali haijachukua hatua kudhibiti ada kubwa zinazotozwa na shule binafsi ambazo wazazi wengi hushindwa kuzimudu. Akijibu maswali hayo Naibu Waziri huyo alisema shule inaposajiliwa inakuwa imekidhi vigezo vya kuwa na miundombinu yote muhimu yakiwemo majengo, maktaba, madarasa na viwanja vya michezo. Hivyo ni makosa kwa shule au chuo kusajiliwa bila ya kukidhi vigezo . Aidha ni kinyume cha taratibu na miongozo ya wizara kwa baadhi ya shule binafsi kulazimisha wazazi kuchangia michango ya majengo na kutoza ada kubwa kuliko ilivyoelekezwa na serikali kupitia Waraka wa Elimu Na. 19 wa mwaka 2002 unaelekeza wenye shule binafsi kutoza ada ya kiasi cha sh. 380,000 kwa shule za bweni sh. 150,000 Shule za kutwa . Alitoa wito kwa wadau wa elimu hasa wamiliki wa shule binafsi kuwa na moyo wa uzalendo katika suala la utozaji ada na michango kwa kuzingatia hali halisi ya kipato cha Mtanzania wa kawaida. |
No comments:
Post a Comment