Nora Damian
ALIYEKUWA Mtangazaji wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Jerry Muro, anayekabiliwa na kesi ya kuomba rushwa ya Sh10 milioni, ameieleza mahakama kuwa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha, alimtisha kuwa hatochomoka katika sakata hilo.
Muro alieleza hayo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu alipoanza kujitetea kwa mara ya kwanza dhidi ya tuhuma zinazomkabili.Katika utetezi wake uliodumu kwa saa tatu akiongozwa na mawakili wake, Majura Magafu na Richard Rweyongeza, Muro alidai kwamba Masha alisema mwisho wa kesi hiyo unampeleka yeye (Muro) kaburini.
Alisema siku chache baada ya yeye kukamatwa, Masha akiwa waziri alimfuata ofisini kwake TBC Mikocheni na kumtupia bahasha ikiwa na maneno ya vitisho.“Masha alinifuata ofisini, nikaenda kuongea naye lakini ghafla nilipoingia tu kwenye chumba cha mkutano alinitupia bahasha ya rangi ya kaki,” alizidi kutoa madai yake Muro na kuongeza:
“Nilizifungua bahasha hizo na kukuta picha tatu za CCTV ambazo Masha aliniambia ni za kwangu, aliniambia kaka umekwisha, mimi naondoka na wewe lazima utaondoka.”Hata hivyo, picha hizo ambazo zilitolewa na upande wa mashitaka kama kielelezo katika kesi hiyo, Muro alizipinga akisema hakuna sura yake na kinachoonekana ni maumbo tu ya watu watatu ambao hata sura zao hazifahamiki.
Alidai mahakamani hapo kwamba, Masha alimwambia (Muro) aitishe mkutano wa waandishi wa habari na kusema Jeshi la Polisi halijamuonea, ila wamegongana tu kwenye utendaji wa kazi, lakini yeye hakufanya hivyo.
Muro ambaye kesi yake imekuwa ikivuta hisia za watu, alidai kuwa baada ya kuanza kuripoti habari za uchunguzi amekumbana na zaidi ya matukio 15 yanayohatarisha usalama wake na kwamba, licha ya kuyaripoti polisi hakuna hata moja lililofanyiwa kazi.
Alidai kutokana na matukio hayo, bosi wake wa awali Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni za IPP Reginald Mengi aliamua kumnunulia bastola ili imsaidie katika usalama wake na kwamba, aliwahi kuitumia.“Hata pingu niliamua kununua ili inisaidie pale ninapoona nimebanwa, nimkamate mwenyewe mhalifu, kwa sababu nilisharipoti matukio mengi polisi, lakini hakuna lililozaa matunda,” alidai Muro.
Mtangazaji huyo alidai watuhumiwa anaoshtakiwa nao hawafahamu na kwamba, hajawahi kuwaona na hata Wage anayetajwa kwenye hati ya mashitaka kuwa alimuomba rushwa hamfahamu.
Alidai kuwa habari zilizomletea matatizo ni zile zinazohusu askari polisi wa Kikosi cha Usalama Barabarani kufanya ufisadi katika Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Nyerere, biashara ya uchangudoa, rushwa kwenye rumbesa Njombe na uchunguzi wa raia wa Korea aliyekuwa amemilikishwa eneo kubwa la ardhi huko Bagamoyo, mkoani Pwani.
Aliendelea kudai mahakamani hapo kwamba, baada ya uchunguzi kuhusiana na suala la raia huyo wa Korea baadhi ya watu walimpigia simu na kumfuata ofisini na kumshawishi achukue rushwa ya Sh60 milioni, ili aachane na habari hiyo, lakini alikataa na kuirusha habari hiyo hewani.
Muro alisema hakuwahi kumuomba Wage rushwa ili asirushe habari zake za ufisadi, kwa sababu mtu huyo tayari alishavuliwa madaraka na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, hivyo kwake (Muro) hakuwa habari.
Aliongeza kwamba, hata baada ya kufikishwa mahakamani na kushtakiwa bado ameendelea kupata majanga mengi yakiwemo kuachishwa kazi, kukosa zawadi yake ya Dola za Marekani 4,000 zilizotokana na kupewa Tuzo ya Mwandishi bora na Baraza la Habari (MCT), kukosa nafasi ya kwenda kusoma katika Chuo Kikuu cha Tumaini na kufukuzwa kwenye nyumba aliyokuwa amepanga.
“Kabla ya kuachishwa kazi nilikuwa nalipwa pesa kidogo, lakini walipomuondoa Tido hata kile kidogo nikawa sipati na hata zawadi yangu ya MCT hadi leo sijapewa,” alidai Muro.
Aliendelea kudai kuwa, ndani ya Jeshi la Polisi wako wanaomkandamiza na wanaoendelea kumuandama na kwamba, mwisho wa kesi hiyo unampeleka yeye kaburini.
Muro aliiomba mahakama imuachie huru kwa sababu hakutenda kosa lolote na kudai kuwa ni njama watu wachache wenye lengo la kutaka kumwangamiza.Hakimu Frank Moshi anayesikiliza kesi hiyo aliiahirisha hadi Septemba 27. mwaka huu washtakiwa wengine watakapoendelea kujitetea.
Mbali ya Muro washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Edmund Kapama na Deogratias Mgasa ambao kwa pamoja wanadaiwa kumuomba rushwa Wage aliyekuwa Mhasibu wa Halmashauri hiyo ya Bagamoyo.Kapama na Mgasa pia wanadaiwa kujifanya maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment