Monday, August 15, 2011

Nyumba Ya Kapteni Komba Yachomwa Moto Huko Mbinga Mkoani Ruvuma

Kapteni John Komba
----
WATU wasiojulikana wanadaiwa kuchoma moto nyumba ya Mbunge wa jimbo la Mbinga Magharibi, Kapteni John Komba, katika kijiji alikozaliwam, Lituhi, kata ya
Lituhi wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma.

Habari zinaeleza kuwa tukio hilo limetokea Agosti 14 mwaka huu majira ya usiku katika kijiji hicho ambapo nyumba hiyo imeteketea kabisa.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu mmoja kati ya ndugu wa jirani na Bw. Komba ambaye alikuwa katika eneo la tukio, alijitambulisha kwa jina moja la Malumba, alisema kuwa moto huo umesababisha hasara kubwa ya kuteketeza nyumba na vitu vyote vilivyokuwa ndani ya nyumba hiyo.

'Ndugu yangu hapa ninavyosema, nyumba na vitu vyote vya ndani vimeteketea kwa moto lakini hakuna vifo vilivyojitokeza tupo salama,' alisema.

Aliongeza kuwa mbunge huyo alikuwa katika ziara ya kutembelea wapiga kura wake katika jimbo hilo na kwamba taarifa za kuunguliwa nyumba hiyo alizipata usiku akiwa katika mji mdogo wa Mbambabay na kuamua kurejea nyumbani.
Kadhalika Majira lilipomuuliza Bw. Malumba ni kitu gani hasa kilichosababisha moto huo kuunguza nyumba, alisema inadaiwa kuna watu wasiojulikana wametumia mafuta aina ya petroli kuchoma nyumba hiyo.

Vilevile alipotafutwa kwa njia ya simu Bw. Komba hakupatikana kwa kuwa simu yake muda mwingi ilikuwa imefungwa.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, Bw. Michael Kamuhanda alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kwamba jeshi la polisi linafanya uchunguzi na litatoa taarifa kamili mara baada ya kukamilisha kazi yake.

Bw. Kamuhanda alisema polisi wamekwenda huko katika kijiji cha Lituhi, kwa lengo la kukamilisha uchunguzi wa tukio hilo. Chanzo, Gazeti Majira





No comments: