Na Mwandishi wa Jeshi la Polsi- Zanzibar
Askari wa mapokezi katika vituo vya Polisi hapa nchini, wametakiwa kuwa kioo cha Jeshi hilo kwa kuonyesha ukarimu na kauri nzuri wanapowahudumia wananchi wanaofika kwenye vituo hivyo ama wanapoombwa msaada mahala popote wanapoombwa kufanya hivyo.
Afisa Uhusiano wa Jeshi la Polisi Zanzibar Inspekta Mohammed Mhina, amesema hatua hiyo italiwezesha Jeshi hilo kuendelea kujenga heshma mbele ya Jamii wanayoihudumia na taifa kwa ujumla.
Akifungua mafunzo kwa wakuu wa Vituo vya Polisi na Askari Viongozi wa vyumba vya mashtaka yanayoendeshwa kwenye Chuo cha Polisi Zanzibar, Mkuu wa Operesheni Maalum wa Jeshi la Polisi Zanzibar SP Issa Juma Suleiman, amesema dhamira ya Jeshi hilo ni kutaka kila askari kubadilika na kutoa huduma bora kwa wananchi.
Kamanda Suleiman amesema mafunzo hayo yatawawezesha washiriki kubadili kwelekeo wa kiutendaji wawapo vituoni mwao na kuwafanya wananchi kuona kuwa vituo vya Polsi ni kimbilio la watafuta haki.
Amesema mwananchi anapokwenda katika kituo cha Polisi anatarajiwa kupata huduma anayoitegemea na kwamba kama atakuwa na tatizo anaamini atapata mapokezi mazuri na kutatuliwa tatizo lake.
Kamanda Suleiman amesema kutokana na mabadiliko ya mifumo ya Majeshi ya Polisi Duniani Kote, Polisi anatakiwa kumuona Raia kama sehemu ya Polisi kwani ni Raia huyo huyo atalazimika kutoa taarifa za wahalifu Polisi na hivyo kurahisisha utendaji wa Jeshi zima.
Awali kaimu Mkuu wa Chuo cha Polisi Zanzibar SSP Andrew Mwang’onda, alisema kuwa washiiriki hao watalisaidia Jeshi la Polisi katika kuboresha utendaji wa kazi za Polisi katika maeneo mbalimbali.
Mafunzo hayo ya wiki moja yanawashirikisha Wakuu wa Vituo vya Polisi 18 na Viongozi 42 wa Vyumba vya Mashtaka kutoka vituo mbalimbali vya Polisi katika mikoa mitatu ya Unguja.
No comments:
Post a Comment