Tuesday, August 2, 2011

BASATA YAWAKUTANISHA WASANII NA WASAMBAZAJI

Katibu Mtendaji wa BASATA,Ghonche Materego akiongea na wasanii kuhusu usambazaji wa kazi zao kwenye Jukwaa la Sanaa wiki hii.Wengine kutoka kulia ni watendaji kutoka Kampuni ya Usambazaji ya Steps Claud,Jairay na Kambarage.
Meneja uzalishaji kutoka Kampuni ya Usambazaji kazi za wasanii ya Steps Entertainment (Kulia) akifafanua masuala mbalimbali kuhusu kazi zinazofanywa na kampuni hiyo kwenye Jukwaa la Sanaa linalofanyika kila wiki kwenye Ukumbi wa BASATA.Kushoto ni Katibu Mtendaji wa BASATA,Ghonche Materego.
Afisa anayeshughulikia maudhui ya kazi za Filamu kutoka Bodi ya Filamu Bw.Tairo akieleza kuhusu zoezi la ukaguzi wa kazi za filamu.
Mdau huyu naye alikuwa ameandaa nondo za kutosha kwa ajili ya kupata ufafanuzi na maelezo kuhusu usambazaji wa kazi za wasanii nchini.
Msanii wa Filamu Michael Sangu akihoji masuala mbalimbali kuhusu usambazaji wa kazi zao kwa Watendaji wa Kampuni ya Usambazaji ya Steps.Mjadala ulikuwa mzito.
Wasanii wakifuatilia mjadala kuhusu mikakati ya kuboresha usambazaji wa kazi za wasanii nchini

Na Mwandishi Wetu

Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kupitia program yake ya kila wiki ya Jukwaa la Sanaa imewakutanisha wasanii na moja ya Kampuni ya usambazaji kazi zao ya Steps Entertainment kwa lengo la kuja na mikakati ya pamoja ya uboreshaji wa soko.

Wakizungumza kwenye Ukumbi wa Baraza hilo,wasanii wengi walitupa lawama kwa wasambazaji hao kwa kile walichodai kwamba,wamevuruga mfumo wa usambazaji wa kazi zao hapa nchini kiasi cha kufanya wasambazaji wengine waliokuwepo kushindwa kuhimili.

Walizitaja sababu zilizosababisha kuvurugika kwa mfumo wa usambazaji wa kazi za wasanii kuwa ni pamoja na wasambazaji hao kushusha bei za CD/DVD hadi shilingi elfu moja,kutokusambaza kazi za wasanii wanaochipukia hadi zishirikishe wasanii maarufu na kutokuwepo kwa mfumo eleweka wa bei.

Sababu zingine ni wasambazaji kuwabana wasanii wenye majina (maarufu) kushirikiana na wale wanaochipukia,ununuaji wa hakimiliki za wasanii kinyume cha sheria za hakimiliki,kutokuwepo kwa mfumo mzuri wa kugawa kazi za wasanii kwenye madaraja na sababu nyingine nyingi.

“Leo hii CD zinauzwa mtaani kwa shilingi elfu moja,hivi kweli kazi za wasanii wa Tanzania zimefikia kiwango cha kuuzwa kwa shilingi elfu moja?Ni msambazaji gani ataweza kuhimili ushindani wakati kuna kampuni imeshusha thamani ya kazi za wasanii kwa kiwango hiki? Alihoji Michael Sangu ambaye ni Msanii wa Filamu.
Akijibu hoja za wasanii,Meneja wa Uzalishaji wa Kampuni ya Steps Entertainment, Kambarage Ignatus alisema kwamba,Kampuni yake inafanya biashara hivyo inajikita katika kutafuta faida na kusambaza kazi zenye ubora na kuuzika.

Aidha alikanusha shutuma kwamba kampuni yake imekuwa ikiwabana wasanii maarufu wasifanye kazi na wale wanaochipukia huku akisema kwamba,usambazaji wa kazi yoyote ya msanii ni makubaliano baina yake na kampuni ambayo yanakuwa kwenye mkataba.

“Kampuni ya Steps inafanya biashara na kuhitaji faida hivyo, inanunua na kusambaza kazi zenye ubora na zinazokubalika kwa wateja.Hatuwezi kusambaza kila kazi ya msanii,wasanii ni wengi sana ila tunalenga zile zenye ubora na kuuzika”alisisitiza Kambarage.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa BASATA,Ghonche Materego alisema kwamba,tatizo linalojitokeza ni kwa baadhi ya wasanii ama kutozingatia mikataba au kutokujua umuhimu wake hivyo kuahidi kuandaa programu maalum ya elimu ya mikataba kwa wasanii.

“Ndugu zangu kupitia Jukwaa hili nimejifunza kwamba,wasanii hatuzingatii mikataba na hata hatuoni umuhimu wake.Baraza sasa linajipanga kuwaleta wataalam mbalimbali wa mikataba na hakimiliki ili kuwajengea uelewa wasanii” aliahidi Materego.

Aidha,aliwaahidi wasanii kwamba,BASATA kwa kushirikiana na Mashirikisho ya Sanaa nchini litaandaa utaratibu wa kuhakikisha kunakuwa na mfumo wa bei unaoeleweka kwa kazi za wasanii.

No comments: