Friday, April 20, 2012

Mwakalebela atoa somo kwa wajumbe wa mkutano mkuu wa TFF



WAKATI  mkutano
mkuu wa Shirikisho la Kandanda nchini (TFF) unafanyika leo, Katibu Mkuu
wa zamani wa shirikisho hilo, Fredrick Mwakalebela amewashauri wajumbe
kujadili masuala ya kulipatia uwezo  shirikisho hilo na kuepuka kuwa tegemezi.
Akizungumza jijini jana, Mwakalebela alisema kuwa  TFF
inaweza kuepukana na hali ya kuomba fedha kwa wadau ili kusafirisha
timu ya Taifa ya wanawake na baadala yake kutengeneza sera
itakayowafanya wadhamini washindani kudhamini timu na shughuli mbali
mbali bila kuingilia shughuli za mwengine.
Alifafanua kuwa  udhamini
wa kampuni ya simu ya Vodacom unawazuia kampuni nyingine za simu kama
Tigo, Zantel na Airtel kudhamini timu shughuli nyingine za shirikisho
hilo na kunyimwa fursa ya kuendeleza michezo nchini.
Mwakalebela
alisema kuwa TFF inatakiwa kuandaa sera ambazo zitawaruhusu wadhamini
kama hao kudhamini hata timu za taifa za vijana na wanawake ili
watanzania waweze kufaidi matunda ya uwekezaji wao.
Katibu Mkuu huyo pia alitoa ushauri  kwa
wajumbe hao kujadili suala la matumizi ya uwanja wa kumbukumbu ya
Karume kutumika kibiashara zaidi kutokana na ukweli kuwa upo katika eneo
zuri (Prime Area) kwa ajili ya shughuli hiyo na kuwaingizia kipato.
Alisema
kuwa eneo hilo linaweza kutumika kwa ujenzi wa maduka, hotel na vitega
uchumi mbai mbali ambavyo vitaiondolea shirikisho hilo uhaba wa kupata
fedha kwa ajili ya shughuli zake mbali mbali mbali.
Kuhusiana
na kushuka kwa soka la Tanzania, Mwakalebela aliwaomba wajumbe kujadili
na kuweka mikakati mikubwa ya kuanzisha soka la vijana wadogo  kwa
kushirikiana na Cecafa, CAF na Fifa ili kufikia lengo. Alisema kuwa kwa
kuandaa vijana hao, wataweza kushindana katika mashindano ya vijana na
baadaye kufanya vyema kwa upande wa soka la wakubwa.

“Kwa sasa soka la vijana lipo jijini Dar es Salaam, Zanzibar  na
pengine Arusha, mikoa mingine ni sawa na hakuna na hii inatokana na 
changamoto za maeneo ya kuchezea, hivyo mipango thabiti inatakiwa 
kuwekwa ili kufanikisha hilo,” alisema.


 
Vile
vile Mwakalebela aliwataka wajumbe hao kujadili maenedeleo ya soka la
wanawake kwa kupanua wigo na kuiwezesha mikoa mengine nao kuwa na timu
za wanawake na syo kutegemea Dar es Salaam tu na hasa Kinondoni.
Alisema kuwa soka la wanawake limeonyesha kuwa ndilo linaweza kuitoa Tanzania kimasomaso kimataifa.

No comments: