na Mwandishi wetu
WAKATI taarifa ya Kamati ya wabunge wa CCM chini ya Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda, juzi iliridhia mawaziri wote wanaokabiliwa na tuhuma za ubadhirifu kwenye wizara zao wajiuzulu, jana Rais Jakaya Kikwete aliwasili nchini akitokea Brazil akiwa na msimamo tofauti.
Taarifa zinasema kumekuwa na mazungumzo baina ya Rais Kikwete na Pinda yaliyolenga kunusuru serikali yao lakini walitofautiana kuhusu hatua inayopaswa kuchukuliwa dhidi ya mawaziri waliotakiwa kujiuzulu.
Msimamo wa Pinda inadaiwa kuwa anataka mawaziri wanaokabiliwa na tuhuma waondoke ili kuleta uwajibikaji serikalini, lakini Rais Kikwete amesema mawaziri hao waachwe waendelee na kazi zao, kwa kuwa suala hili ni la upepo tu, liachwe litapita.
Tanzania Daima Jumapili limeelezwa kuwa rais anakataa shinikizo hilo kwa madai serikali haipaswi kuyumbishwa yumbishwa.
Miongoni mwa mawaziri wanaopaswa kuondoka ni Waziri wa Fedha, Mustafa Mkullo; Waziri wa Viwanda na Biashara Dk. Cyril Chami na naibu wake, Lazaro Nyalandu; Waziri wa Tawala wa Mikoa na Serikali za Mitaa, George Mkuchika na naibu wake, Aggrey Mwanri; Waziri wa Afya, Dk. Haji Mponda na naibu wake, Lucy Nkya na Waziri wa Uchukuzi, Omari Nundu.
Wengine ni Waziri wa Nishati na Madini William Ngeleja na Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige.
Habari zinasema Rais Kikwete na Pinda walitofautiana juu ya hatua dhidi ya mawaziri hao, hivyo kuwafanya baadhi ya mawaziri kutamba mitaani kuwa hawang’oki madarakani kwa sababu tayari bosi wao ameonyesha kutounga mkono tuhuma zinazoelekezwa kwao na wabunge wa upinzani na CCM.
Habari hizi zinasema pia kwamba Pinda amekuwa hafurahishwi na msimamo wa ‘bosi’ wake, hasa katika kushindwa kutoa uamuzi mgumu.
Zinadai kuwa rais amekuwa na tabia ya kuacha upepo uchukue nafasi yake wakati Pinda anataka baadhi ya watu wawajibike bila kujali nyadhifa zao au ukaribu na kiongozi mkuu wa nchi ili kurejesha imani ya serikali kwa wananchi.
Pinda inadaiwa amekuwa akitaka maamuzi magumu yafanyike, kwakuwa yeye ndiye anayesulubiwa na maswali pamoja na hoja za wabunge wawapo bungeni.
Baadhi ya wabunge waliozungumza na Tanzania Daima Jumapili, wameweka wazi kuwa kama Rais Kikwete ataamua kuwalinda na kuwatetea mawaziri wake basi watawaondoa kwa mkakati tofauti utakaomlazimisha rais kukubaliana na hoja za wabunge.
Baadhi ya wajumbe waliozungumza na gazeti hili waliweka wazi hatua hiyo inahitaji muda na mipango madhubuti na wao wapo tayari kufanya hivyo, kwani nchi inazidi kudidimia kwenye umaskini huku watu wake wakikosa huduma muhimu za kijamii.
Walisema kwa muda mrefu wamekuwa wakiwalalamikia watendaji wa serikali na chama tawala lakini rais amekuwa mgumu wa kuyashughulikia matatizo hayo.
Wanasema rais ndiye kikwazo kikubwa cha maendeleo ya chama chao na serikali, hasa kwa kuwateua mawaziri, wakurugenzi na maofisa wengine bila kuangalia uwezo wao wa kiutendaji.
“Kaka kwenye Bunge la Februari kuna mbunge alitoa kauli kuwa kama tunaona mambo hayaendi serikalini tupige kura ya kutokuwa na imani na rais, watu walimshambulia. Sasa tunaona umuhimu wa kauli yake ile,” alisema mbunge mmoja.
Tanzania Daima Jumapili, limedokezwa makada wa CCM wameanza kuingiwa na hofu ya kubomoka kwa chama chao hasa baada ya makada wenzao kuanza kujiunga na vyama vya upinzani.
Wanasema wakati makada wa chama hicho wakiendelea kukihama uongozi wa CCM hauonekani kuchukua hatua zinazostahiki dhidi ya viongozi wanaochangia wananchi wakose imani na chama tawala.
Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe, aliweka wazi kuwa wabunge wa CCM ni lazima wakemee ubadhirifu kwakuwa Tanzania si mali ya CCM.
Mbunge huyo alikwenda mbali kwa kumtaja Waziri wa Fedha, Mustafa Mkullo, kuwa ni mwizi, mwongo na mbadhirifu wa mali za umma.
Mawaziri wasuasua kuwasilisha barua
Hadi jana Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alisema hajapokea barua ya kujiuzulu kutoka kwa waziri yeyote huku akiweka wazi kuwa kesho atatoa taarifa kamili juu ya jambo hilo.
Juzi vyombo vya habari vilipata taarifa kutoka kwenye kikao cha wabunge wa CCM kuwa baada ya wabunge kuzituhumu baadhi ya wizara kukithiri kwa ubadhirifu mawaziri wake wameamua kujiuzulu.
Taarifa hizo zilidokeza kuwa mawaziri hao walishinikizwa kuachia nyadhifa zao ili kukinusuru chama na serikali dhidi ya hasira za wananchi wanaokerwa na ufisadi.
Chami atoboa siri
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Cyril Chami, amejitetea kuwa wizara yake haimlindi Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Charles Ekelege, kama alivyotuhumiwa na baadhi ya wabunge.
Alisema amesononeshwa na taarifa ya ukaguzi wa CAG juu ya TBS iliyotolewa kwa waheshimiwa wabunge bila yeye mwenyewe au wizara kupewa nakala kwa kipindi cha wiki nzima.
Alisema kuwa baada ya kusikia kuwa waheshimiwa wabunge wengi wanayo taarifa hiyo na hata naibu wake kukiri bungeni kwamba taarifa imetoka wakati yeye hana nakala, alikwenda kwa Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashillilah na kuiomba nakala ya taarifa hiyo.
Alibainisha kuwa baada ya kufanya ufuatiliaji katika ofisi ya CAG ilikiri kuigawa kwa wabunge na kusahau kuipeleka kwa wizara hiyo ambayo ndiyo inayohusika.
“Hapa wasomaji wapime wenyewe. Inawezekanaje taarifa ya CAG iliyoandikwa kutokana na takwimu zilizotolewa na wizara yangu, iwafikie wabunge huku wizara yangu itakayotakiwa kuifanyia kazi taarifa yenyewe haipewi nakala, eti kwa kughafilika?
“Ni ukweli ofisi ya CAG walighafilikiwa, au jambo hili limesukwa ili kuniaibisha mimi mbele ya Watanzania, rais aliyeniteua na hasa wapiga kura wangu wa Moshi Vijijini?” alihoji.
Nundu ajitetea
Naye Waziri wa Uchukuzi, Omar Nundu, alisema tuhuma dhidi yake zilizoelekezwa na baadhi ya wabunge, hazina ukweli na zimelenga kumchafua.
Alisema kilichoelezwa na Kamati ya Miundombinu ni uongo na uzushi, kwani nyaraka walizozitumia kuorodhesha tuhuma dhidi yake si halali.
Kuhusu kuingilia utendaji wa Mamlaka ya Bandari kwa masilahi binafsi, alisema si kweli, akaongeza kuwa kinachomponza ni kuipinga kampuni inayotetewa na menejimenti isipewe zabuni ya kufanya upembuzi yakinifu peke yake na kwenda kukopa na baadaye iruhusiwe kujenga gati namba 13 na 14.
“Wanasema namtaka mwekezaji ambaye makubaliano yanaonyesha atamiliki gati hilo kwa miaka 45. Nachelea kusema ni uongo na uzushi,” alisema Nundu.
Mkuchika apata kigugumizi
Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Mkuchika, alipoulizwa juu ya suala hilo alishindwa kukubali wala kukataa iwapo ataandika barua ya kujiuzulu. Alimtaka mwandishi amuulize Katibu wa Kamati ya Uongozi.
chanzo Tanzania daima 22/april/2012
No comments:
Post a Comment