Na Maggid Mjengwa,
KIJANA wangu wa miaka 16 amenieleza sababu moja kuu ya Barcelona kushindwa kufanya vizuri msimu huu. Anasema; Barcelona wamekuwa wakiamini siku zote, kuwa kuna njia moja tu ya kucheza kandanda, na njia hiyo ni ya Barcelona!
Kwamba hata kama Barcelona walifungwa na Chelsea na wakashindwa kucheza fainali za Kombe la Mabingwa Ulaya, Barcelona bado inaamini, kuwa tatizo si njia yao ya kucheza kandanda, bali ni bahati mbaya tu wameshindwa. Kwamba wao ndio walistahili kucheza mechi ya fainali dhidi ya Bayern Munich!
Barcelona wameshindwa kutambua, kuwa tatizo la Barcelona ni Barcelona yenyewe. Kwamba hata katika soka wakati umebadilika. Njia ya Barcelona kucheza kandanda ni moja, na kuna njia nyingine nyingi za kucheza kandanda. Barcelona mpaka dakika ya mwisho hawakuwa na uthubutu wa kubadili njia yao ya kucheza kandanda, hivyo basi, kupelekea anguko lao.
Mfano wa kijana wangu wa klabu ya Barcelona ulinisukuma kwenye kuitafakari CCM na shida inayopata sasa, hususan kupoteza umaarufu miongoni mwa Watanzania na hasa zaidi vijana. Kama Barcelona, CCM nayo inaamini, siku zote, kuwa kuna njia moja tu ya kuendesha siasa katika nchi hii, na njia hiyo ni ya CCM!
Na hata CCM iliposhindwa kiti cha Ubunge Arumeru na viti vya madiwani maeneo kadhaa ya nchi, bado ndani ya CCM kuna wanaoamini, kuwa tatizo si njia ya CCM, bali kuna ‘mapungufu ya hapa na pale’ yaliyopelekea kushindwa kwao.
Kauli za hivi karibuni za baadhi ya Wana-CCM ikiwamo ya Kamati ya Abdulhaman Kinana kuwataka CCM wajiandae kisaikolojia na Katiba Mpya ikiwamo uwepo wa wagombea binafsi inaashiria CCM kuanza kuamka.
Maana, wakati umebadilika. Na ndani ya CCM, Mwenyekiti wao, Jakaya Kikwete anaonekana ni mmoja wa walioliona mapema hili la mabadiliko ya wakati. Hatuwezi tena leo, kutumia nadharia za miaka 40 iliyopita kuendeshea mambo yetu ya leo katika dunia iliyobadilika. Upepo wa mabadiliko ya wakati una tabia moja kuu; usipoendana nao, basi, utakupiga kikumbo.
Nimepata kuandika, kuwa vijana wengi leo wanaikimbia CCM na hawataki kuhusishwa nayo. Tujiulize; ni kwa namna gani vijana hawa watakuwa na mapenzi na chama kinachohusianishwa mara kwa mara, na kashfa kubwa za kifisadi. Kashfa zinazoathiri maisha yao? Kwao wao, wanayaona ‘madudu’ kwenye vazi la chama. Hatuyaoni?
Ni sawa na kisa kile cha ‘ Mfalme aliyetembea uchi’. Watu wazima walijipanga barabarani kusifia vazi jipya la mfalme huku wakiifumbia macho kasoro kubwa ya vazi hilo, kuwa lilimwacha mfalme nusu uchi. Na hata pale mtoto alipotamka; “ Jamani, mfalme yuko uchi!” Kuna waliofunika nyuso zao kwa aibu. Maana, mtoto aliusema ukweli wake.
Chama cha Mapinduzi ni chama kikubwa, kikongwe na kinachotawala kwa sasa. Lakini, kwa sasa, si chama kinachopendwa, bali kinachozidi kuchukiwa sana na kundi kubwa la vijana. Huu ni ukweli ambao, wanafiki ndani ya chama hicho hawataki kuusema, wala hawataki kuusikia ukisemwa. Ndio, ukweli mwingine haufurahishi, lakini ni lazima usemwe ili kuwasaidia wahusika kujisahihisha, kama wana nia ya dhati ya kufanya hivyo.
Tunavyoenenda sasa, ili CCM ibaki salama katika chaguzi zijazo inahitaji mawili; mosi, Katiba iliyofanyiwa marekebisho makubwa, pili, kurudisha imani ya kundi la vijana kwa chama hicho. Kwanini?
Ni ama wanafiki au wasiojihangaisha kufikiri kwa bidii ndani ya CCM ambao bado wanaamini chama hicho kitaendelea kubaki madarakani daima. Maana, hakuna uchaguzi mkuu ambao umeanza kusubiriwa kwa hamu kubwa na kundi kubwa la vijana kama uchaguzi wa 2015.
Tunaojichanganya na vijana mitaani na kwenye mitandao tunalifahamu hilo. Kwa vijana wa sasa, kuchagua upinzani ni fasheni. Ni kuondokana na ukongwe, ni vijana wangapi wasiotaka hilo? Vijana hawa, wanaweza kuiondoa madarakani CCM hata kwa Katiba ya sasa. Katiba mpya ni salama ya CCM. Na CCM ikianguka kwa Katiba ya sasa, basi, itakuwa ni sawa na nyumba ya karata. Yumkini kitabaki kuwa chama kwenye vitabu vya historia.
Ni ukweli pia, CCM haiwezi kutegemea kubaki madarakani kwa muda mrefu kwa kura za wazee, maana, idadi yao inapungua kila kukicha. CCM haina jinsi, bali kuungana na Mwenyekiti wao, Jakaya Kikwete, katika kuongoza mabadiliko haya ya kihistoria katika nchi yetu. Mabadiliko makubwa ya Katiba ambayo, mbali ya mambo mengine yaruhusu uwepo wa Tume Huru ya Uchaguzi, Uundwaji wa Serikali ya Mseto na hata kumpunguzia Rais nguvu nyingi za maamuzi alizo nazo. Kwa kufanya hivyo, kuna hadhi , heshima na imani kwa CCM itakayorudi.
Maana, katika jamii, mabadiliko yanapaswa yaendane pia na fikra mpya . Na jamii huingiwa na mashaka na kukosa imani pale fikra mpya zinapotekelezwa na watu wale wale ambao hawataki kabisa kuwaruhusu wengine kushiriki uongozi wa nchi. Watu ambao bado miongoni mwao wanaamini kuwa tofauti za kifikra ni jambo baya. Kwamba upinzani ni uadui, ni uhaini. Kwamba wapinzani ni wa kuwakatakata na kuwatupa.
Sasa, katika hali ya sasa utawachinja wangapi ukawamaliza? Ni fikra za kiwendawazimu.
Nchi yetu inapita sasa katika kipindi kigumu tangu tupate uhuru wetu. Ni kipindi kinachowataka viongozi, na hususan viongozi wa kisiasa, kutanguliza hekima na busara badala ya jazba, chuki na visasi. Hayo matatu ya mwisho ni mambo maovu yenye kuambukiza kwa haraka.
Kamwe tusiruhusu jazba, chuki na visasi vitawale siasa zetu. Hii ni nchi yetu. Ni nchi yetu sote. Hakuna mtu, kikundi au chama cha siasa chenye haki zaidi ya kuongoza nchi hii kuliko wengine wote.
Ukweli, ndani ya CCM kuna wenye hofu ya kupoteza mamlaka ya kuongoza dola. Ni hofu hiyo inayowasukuma kuwa tayari kufanya lolote lile kuzuia mabadiliko ambayo wengi sasa wanataka yatokee katika nchi hii.
Hakuna busara nyingine yeyote kwa sasa bali ni kwa CCM kuruhusu na kuendesha kwa salama mchakato wa mabadiliko makubwa yanayotakiwa na umma. Mabadiliko hayaepukiki. Ni hali ya dunia kwa sasa. Ni kama wimbi la maji ya bahari. Limeshajikusanya. Kwa CCM chaguo ni moja tu, kuenenda na wimbi hilo la mabadiliko au kukubali kufunikwa nalo.
Hilo la mwisho laweza kuharakisha kifo cha CCM. Ni jambo baya, maana, hata kama Watanzania watachagua upinzani ifikapo 2015, nchi yetu inahitaji chama imara cha upinzani, na CCM inaweza kuvaa viatu hivyo. Nahitimisha.
0788 111 765
No comments:
Post a Comment