Rais Jakaya Kikwete akimsaidia kuteremka ngazi za Ikulu Prof Mark Mwandosya baada ya kumwapisha kuwa Waziri asiye na Wizara Maalumu, katika hafla iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam jana. Picha na Emmanuel Herman
Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya, jana aliapishwa Ikulu kushika wadhifa huo huku akikataa kuzungumzia mipango yake ya baadaye ya kisiasa. Profesa Mwandosya akijibu moja ya maswali ya waandishi wa habari baada ya kuapishwa, lililohusu iwapo bado ana nia ya kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, alisema hawezi kuzungumzia suala hilo mpaka hapo afya yake itakapotengemaa.
“Mbona mnapenda sana kuniuliza suala hili? Maana kila mwandishi akiniona anapenda kuuliza hili au leo mmeuliza kwa sababu mmeona nimekuja karibu na jengo hili? (Ikulu)…” alihoji huku akicheka na kuongeza: “Ngoja kwanza tuangalie afya…. Eeh! Afya kwanza halafu hayo mambo mengine yatafuata.” Profesa Mwandosya alihamishiwa Ofisi ya Rais kutoka Wizara ya Maji aliyokuwa akiiongoza awali, baada ya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri yaliyofanywa na Rais Jakaya Kikwete, Mei 4, mwaka huu.
Hata hivyo, waziri huyo ambaye aliomba kugombea urais kupitia CCM akipamba na Rais Kikwete mwaka 2005, hakuweza kuapishwa na mawaziri wenzake Mei 7, mwaka huu kwa kuwa ndiyo kwanza alikuwa amerejea kutoka India alikokuwa kwa muda mrefu akipatiwa matibabu kutokana na ugonjwa ambao hata hivyo, haujawahi kuwekwa hadharani.
Katika mchakato wa kinyang’anyiro hicho ndani ya CCM, Profesa Mwandosya alishika nafasi ya tatu, nyuma ya Rais Kikwete na Dk Salim Ahmed Salim. Jana, Profesa Mwandosya alizungumzia afya yake kwa kusema kuwa anaendelea vizuri... “Afya yangu ni kama mnavyoiona, naendelea vizuri tu, mwaka jana nilikuwa nikitembea kwa msaada wa magongo lakini leo nimeweza kutembea mwenyewe bila msaada wa magongo, kwa kweli naendelea vizuri,” alisema Waziri huyo.
Kuhusu wadhifa wake mpya alisema anafahamu kwamba kazi aliyonayo ni kubwa na kwamba yuko tayari kumsaidia Rais katika majukumu mbalimbali ya kitaifa yanayomkabili. “Mnafahamu Rais ana majukumu mengi sana ya kitaifa, yanamhitaji kwenda hapa na pale, kwa hiyo mimi kwanza nashukuru kwa kupewa wadhifa huu na niko tayari kumsaidia mheshimiwa Rais katika majukumu hayo,” alisema.
Ugonjwa wake Profesa Mwandosya alikwenda katika Hospitali ya Apolo, India kwa ajili ya matibabu Mei, mwaka jana ambako alikaa huko kwa miezi ipatayo sita kabla ya kurejea Novemba 29, 2011.
Desemba 3, 2011 zikiwa zimepita siku sita tangu aliporejea, alifanya mkutano na waandishi wa habari katika makao makuu ya Wizara ya Maji na kusema kwamba alikuwa bado ana kiu ya kuwatumikia wananchi. Katika mkutano huo, Profesa Mwandosya alikataa kuzungumzia suala la urais wa 2015 kwa maelezo kwamba yapo mambo mengi ya kufanya na kwamba haukuwa wakati mwafaka.
“Kama kuna watu wana fedha za kuwekeza katika kutafuta uongozi ni wao, lakini mimi bado nahitaji kuwahudumia wananchi kwa kutatua matatizo ya maji,” alisema na kuongeza:
“Bado kuna mambo mengi, vilivyopo kwenye ajenda za Wizara ya Maji sijavikamilisha. Kwa hiyo siwezi kuzungumzia masuala ya urais wakati bado nina majukumu mazito ya kuwahudumia wananchi.” Januari mwaka huu, Profesa Mwandosya alikwenda tena India kuendelea na matibabu kabla ya kurejea nchini siku chache zilizopita.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment