Tuesday, July 26, 2011

Chadema yamjibu Nape kuhusu nyaraka

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimezikana nyaraka za siri zilizodaiwa kunaswa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye, kuwa si zake na hazikuandikwa na chama hicho.
Katibu Mkuu wa Chadema Dk. Wilbroad Slaa, alitoa ufafanuzi huo alipokuwa akizungumza na NIPASHE kuhusiana na taarifa zilizoandikwa juzi na gazeti dada la NIPASHE JUMAPILI likimunukuu Nnauye kuwa amenasa nyaraka za Chadema zilizokuwa zikitoa maelekezo kwa viongozi wa chama hicho wa ngazi ya mikoa na majimbo.

Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika mwishoni mwa wiki mjini Moshi, Nape alisema nyaraka alizonasa ni pamoja na barua yenye kumbukumbu namba CDM/DSM/HU/Vol 040/2011 ya Julai 20, 2011 iliyosambazwa kwa wenyeviti wa kila mkoa kuandaa maandamano nchi nzima baada ya Mkutano wa Bunge la bajeti.
Alisema barua hiyo iliyokuwa imesainiwa na Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, Erasto Tumbo, ilikuwa ikiwashinikiza wenyeviti kuandaa maandamano hayo kwa nia ya kuiabisha serikali kwa madai kwamba imeshindwa kutekeleza majukumu ya kuwaletea maendeleo wananchi.
Aidha alisema kwamba aliinasa barua nyingine ya Chadema yenye kumbukumbu namba CDM/DSM/Vol.138/2011 ya Juni 30, 2011 iliyosainiwa na Tumbo kwenda kwa makatibu wa majimbo kutekeleza agizo la Dk. Slaa la kuwahamasisha wananchi wagomee shughuli za maendeleo katika maeneo yao.
Dk. Slaa alisema mfumo wa namba za kumbukumbu katika barua zote mbili zilizotolewa na Nnauye kwenye mkutano huo, haziendani na mfumo wa kuweka namba za kumbukumbu unaotumiwa na Chadema.
“Mbali na dosari hiyo iliyoko kwenye barua za Nnauye, hata katika tarehe ambazo Nnauye anadai kwamba barua hizo ziliandikwa yaani, Julai 20, 2011 na Juni 30, 2011, hakuna barua yoyote iliyoandikwa toka au kuingia makao makuu ya Chadema,” alisema.
Dk. Slaa alisema yeye binafsi na Chadema kwa ujumla, wanafahamika na wananchi jinsi walivyomstari wa mbele kuhamasisha maendeleo ya wananchi, kwa hivyo haiwezekani wakashiriki kwa namna yoyote ile kuwazuia wananchi wasichangie maendeleo.
Dk. Slaa alisema suala la maandamano kwa Chadema halihitaji kuandikiwa waraka wa siri hata siku moja kwa kuwa wao hutangaza hadharani wanapohitaji kufanya maandamano.
“Chadema huwa tunatangaza maandamano yetu hadharani, mbele ya vyombo vya habari, kupitia kwenye mikutano tunayofanya. Tumeshasema kwamba tutaendelea kuandamana mpaka kieleweke na watu wote wanatambua hilo,” alisema na kuongeza: “Sasa kwa nini tuandike barua ya siri? “
Alisema bado wananchi wanakabiliwa na maisha magumu,ufisadi, tatizo la umeme nchini na bei ya vyakula kuendelea kupanda, Chadema wataendelea kuandamana na safari hii maandamano yao yatakuwa katika mikoa ya Dodoma, Singida, Morogoro, Manyara na Tabora.
CHANZO: NIPASHE

No comments: