Monday, May 28, 2012

Neno La Leo: Jambo La Zanzibar Ni Letu Bara, Lakini....Ndugu zangu,

MFALME Suleiman aliambiwa ndotoni aombe kitu chochote kwa Mola wake, naye akajibu; “ Ewe Mola wangu, nipe mimi mtumwa wako moyo wa adili ili niwahukumu watu wako, na kupambanua mema na mabaya, maana ni nani awezaye kuwahukumu hawa watu wako walio wengi?” Hivyo basi, Mfalme Suleiman aliichagua hekima. Maana, ni Mfalme Suleiman huyo anayekaririwa na vitabu vya dini akitamka, kuwa; “ Watu wangu wanaangamia kwa kukosa hekima”.

Naam, hekima ndilo jambo lililo bora kabisa kwa mwanadamu kuwa nalo. Mwanadamu aliyepunguwa hekima ana hasara kubwa maishani. Hekima ni tunu na kipaji ambacho Mwenyezi Mungu amewajalia waja wake, ili nao waweze kupambanua na kuamua kati ya yalo mema na maovu. Duniani hakuna shule ya hekima.

Zimetufika habari; Zanzibar kuna moto unawaka. Si moto wa kuupuza. Hekima inatuongoza katika kutambua, kuwa ukiupuuzia moto unaowaka kwenye nyumba ya jirani yako, basi, nyumba yako pia imo hatarini kuungua . Naam, ndio sababu ya kusema; Jambo la Zanzibar ni letu.

Ndio, ni letu hata sie tulio bara. msiba wa Unguja ni msiba wetu. Hivyo, kadhia hii ya Zanzibar ni kadhia yetu. Ni wakati sasa wa kutanguliza busara na hekima katika kutanzua kadhia hii. Hoja ya msingi inasemwa kuwa ni suala la Muungano. Mengine ni makandokando yanayotokana na hoja ya msingi. Basi, tuujadili Muungano, kisha tuone kama kuna lingine. Maana, hata bila Muungano wa Serikali moja, sisi bado ni ndugu na majirani wa daima na milele. Tujadili basi aina iliyo bora ya Muungano ili tuendelee kushirikiana kama ndugu.

Binafsi nilifika Zanzibar kwa mara ya kwanza mwaka 1988 ( pichani). Nilikuwa kijana mdogo sana. Zanzibar ndio kisiwa cha kwanza kupata kukitembelea. Tangu hapo niliipenda Zanzibar, nimefika Zanzibar mara kadhaa. Wenyeji ni wakarimu sana. Lakini, ukweli ni huu, tangu safari yangu ya kwanza Unguja miaka hiyo, wenyeji walinikumbusha, tena kwa kutamka kwa vinywa, kuwa mimi ni ' Mtanganyika'- mtu wa mlima. Hivyo, kwangu mimi, hoja ya Muungano nimeionja kwa karibu tangu mwaka 1988 nikiwa Zanzibar.

Si jambo jema wala la kistaarabu kwa watu wachache kule Zanzibar kuchoma moto makanisa, baa na biashara za watu wa kutoka upande wa pili wa Muungano, lakini, vitendo hivi viovu vinavyopaswa kukemewa kwa nguvu zote haviwezi kumalizwa kwa nguvu za kipolisi au kijeshi, bali kwa kuzikutanisha pande zinazotofautiana kwenye meza ya mazungumzo.

Kwa hatua iliyopo sasa, bado Wazanzibari wenyewe wanaweza kukaa chini na kujadiliana kwa uwazi namna ya kwenda mbele. Lililo muhimu ni kuhifadhi amani na utulivu uliokuwepo.

Tayari kinachotokea Zanzibar kimeshakuwa na athari mbaya kiuchumi na kijamii. Kijamii, kuna mbegu za chuki zinapandwa. Ni jambo la hatari. Siku zote , chuki huzaa chuki, silaha huzaa silaha na hatimaye kupelekea uvunjivu wa amani wa muda mrefu.

Katika dunia ya sasa ya teknolojia ya upashanaji habari, habari za uvunjivu wa amani Zanzibar zimeshasambaa duniani kote kama moshi wa kifuu. Watalii wa dunia wanataadharishwa sasa kutokwenda Zanzibar. Tunajua , baada ya kushuka kwa soko la karafuu, asilimia kubwa ya uchumi wa Zanzibar inatokana na mapato kwenye sekta ya utalii. Kadhia hii itapelekea kushuka kwa biashara ya utalii Zanzibar na hivyo kushuka kwa mapato.

Na mfano rahisi wa jinsi Mzanzibar wa kawaida atakavyoathirika, ni pale atakapoambiwa na wenye mahoteli asisitishe kupeleka samaki wake kwa vile wageni watalii wamehadimika. Na kuna vijana wengi wa Zanzibar ambao kipato chao kinategemea sana shughuli za utalii. Nao watakosa cha kufanya, na mapato pia. Mazingira hayo huchangia kuongezeka kwa vitendo vya uhalifu. Na hasira pia ya wananchi, naam, midomo yenye njaa ni midomo yenye hasira.

Kadhia ya Zanzibar inaweza pia kuathiri uchumi wa Bara hasa kwenye eneo hilo la utalii ukiachilia maeneo mengine. Mfano, kuna watalii wanaokuja Bara wakiwa na mipango ya kuunganisha safari zao hadi Zanzibar. Kama Zanzibar hakuendeki na bara hakutaendeka pia. Hivyo, hata mapato ya bara yanayotokana na biashara ya utalii yatapungua.

Naam, huu si wakati tena wa kutanguliza propapanda. Ndio, propaganda iwekwe kando na diplomasia ichukue nafasi yake; mazungumzo, mazungumzo, mazungumzo. Ndicho kinachohitajika sasa. Pande mbili zinazokinzana ziwe kwenye mazungumzo hadi zifikie muafaka ulio na maslahi kwa jamii pana.

Huu si wakati wa kutafuta mshindi, maana, hata tulipofikia sote tumeshashindwa. Ni wakati wa kutanguliza busara na hekima. Na maamuzi mengine tunayotakiwa kuyafanya sasa yasitokane na mazoea ya siku nyuma bali uzoefu mpya tunaoupata sasa.

Na hilo ni Neno La Leo.

Maggid Mjengwa,
Iringa.

0788 111 765
http://mjengwablog.com

No comments: