Tuesday, July 26, 2011

DC - Chunya atoa onyo kwa wenzake


Mkuu wa wilaya ya Chunya Mheshimiwa Deodatus Kinawiro.




Mkuu wa wilaya ya Chunya Deodatus Kinawiro amesema kuwa wakuu wa wilaya tisa zinazopakana na wilaya yake wasitishe haraka utoaji wa vibali vya kusafirishia mifugo hasa Ng'ombe wanaoingia wilayani humo.



Hayo ameyasema leo baada ya kumalizika maombolezo ya siku ya mashujaa yaliyofanyika Jijini Mbeya ambayo mgeni rasmi alikuwa mkuu wa mkoa wa Mbeya John Mwakipesile chini ya vikosi imara vya ulinzi na usalama mkoani hapa.

Kinaworo amesema mwaka jana kulifanyika kikao cha ujirani mwema cha wakuu wa wilaya zote zinazopakana na wilaya hiyo iliyopo mkoa wa Mbeya ambapo walikubaliana kutoingiza mifugo wilayani humo lakini mpaka sasa makubaliano hayo hayajatekelezwa.

Amesema wilaya yake imeandaa utaratibu wa kukamata mifugo yote inayoingizwa katika wilaya hiyo na kuirejesha inakotoka hasa katika wilaya ya biharamuro ambako kumeonekana kuwa na mifugo mingi inayoingizwa wilayani humo.

Sanjari na hayo alilitaja eneo maarufu linalotumika kupitishia mifugo hiyo na wafanyabiashara wa Ng'ombe kuwa ni eneo la Kambi Katoto lililopo mpakani mwa Tabora na Singida ambapo amesema mara kadhaa wanapowakamata wasafirishaji huwa na vibali vya kupitisha mifugo hiyo kwenda Songea lakini wanapofuatilia mifugo hiyo haifiki Songea mkoani Ruvuma matokeo yake huishia katika eneo oevu la Bonde la Songwe wilayani Chunya.

Wilaya zilizoelezwa kufikia muafaka wa kutotoa vibali vya uingizaji na utoaji wa vibali vya mifugo ni pamoja na Chunya, Mbarali, Mbeya, Mbozi, Mpanda, Sumbawanga, Sikonge, Urambo na Manyoni.

Kwa hisani ya Gordon Kalulunga na Tanzania yetu Blog.

No comments: