Friday, July 15, 2011

MV SERENGETI KUPATA HITILAFU IKIWA SAFARINI

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA), inapenda kuutarifu Umma juu ya Meli ya MV Serengeti kupata hitilafu ilipokuwa safarini.

Mnamo tarehe 14 Julai 2011 Meli ya abiria na mizigo MV Serengeti iliyosajiliwa Zanzibar, iliondoka katika Bandari ya Zanzibar, majira ya saa 3 usiku kuelekea Pemba ikiwa na abiria wapatao 810 pamoja na mizigo.

Moja ya injini ya Meli hii ilipata hitilafu ikiwa safarini na kushindwa kuendelea kufanya kazi.
Vikosi vya ulinzi na uokoaji, viliandaliwa ili kukabiliana na dharura yoyote ambayo ingeweza kutokea kutokana na hitilafu hiyo.

Hata hivyo kwa mwendo mdogo, Meli hiyo iliweza kuendelea na safari kwa kutumia injini moja, na kuwasili Pemba katika Bandari ya Mkoani saa 4: 35 asubuhi badala ya saa 12 asubuhi leo tarehe 15 Julai 2011 kama ingesafiri kwa mwendo wake wa kawaida, hivyo kuchelewa kwa takribani kwa saa tano hivi.

Abiria wote pamoja na mabaharia waliokuwamo chomboni walishuka salama.

Imetolewa na:
Ofisi ya Mkurugenzi Mkuu
SUMATRA