MWANAFUNZI wa Shule ya Sekondari Tegeta, Dar es Salaam pamoja na watu wengine watatu, wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakikabiliwa na mashitaka ya kujipatia Sh milioni 620 kwa njia ya udanganyifu. Washitakiwa hao ni Dennis Mtui (34), Matilda Sebalua (52) mkulima, Hawa Kuyoga mfanyabiashara na Paulo Shelukindo anayedaiwa kuwa ni mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Tegeta. Ilidaiwa kuwa washitakiwa hao kwa pamoja walijipatia fedha hizo kwa kuuza viwanja vinne vya Hellen Mvuti na kudai kuwa ni vyao. Wakili wa Serikali, Patrick Malogoi alidai mbele ya Hakimu Frank Moshi, kuwa washitakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka sita ambapo katika shitaka la kwanza wanadaiwa kupanga njama ya kutenda kosa hilo. Katika shitaka la pili, ilidaiwa kuwa, katika siku na sehemu isiyofahamika washitakiwa hao walighushi cheti cha ndoa kilichoonesha kuwa kimetolewa na Msajili wa Ndoa wa Manispaa ya Kinondoni, jambo ambalo si kweli. Alidai kuwa, katika mashitaka mengine, Machi 19, mwaka huu katika International Commercial Bank (ICB), washitakiwa walijipatia fedha hizo kutoka kwa Edgar Makwaya baada ya kumuuzia viwanja vinne vilivyopo eneo la Kunduchi Mtongani. Malogoi alidai kuwa, washitakiwa waliuza viwanja hivyo namba 145, 146, 147 na 148 ambavyo kila kimoja walikiuza kwa Sh milioni 155 huku wakijua kuwa si mali yao. Washitakiwa walikana mashitaka yote na kurudishwa rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana yaliyowataka kuwa na wadhamini wawili watakaosaini hati ya Sh milioni 77.5. Kesi hiyo itatajwa tena kesho.
Chanzo Habari Leo
Chanzo Habari Leo
No comments:
Post a Comment