Rais Jakaya Kikwete
----
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete,Julai 18, 2011, ameanza Ziara ya kihistoria ya Kiserikali (State Visit)nchini Afrika Kusini,ikiwa ziara ya kwanza kufanywa na Rais wa Tanzania nchi humo.
Rais Kikwete anafanya ziara hiyo kwa mwaliko wa Rais wa Afrika Kusini,Mheshimiwa Jacob Zuma ambaye utawala wake umekuwa karibu na wenye uhusiano mzuri na Tanzania tangu aliposhika madaraka ya kuongoza taifa hilo linalokuwa kiuchumi barani Afrika.Rais Kikwete ameambatana na mkewe Mama Salma Kikwete sambamba na Ujumbe wa viongozi wa Kiserikali ambao wameondoka nchini kuelekea mjini Pretoria tayari kuanza ziara hiyo ya siku nne.
Rais Kikwete anayetembelea Afrika Kusini amepewa heshima yaa kipekee katika ziara hiyo tangu nchi hiyo ipate Uhuru na kuingia katika mfumo wa kidemokrasia mwaka 1994.Kwa mujibu wa ratiba ya ziara hiyo,Rais Kikwete, Mama Salma Kikwete na ujumbe wa Tanzania watapokelewa kwenye Ikulu mjini Pretoria na Rais Zuma pamoja na mkewe ambapo watakaribishwa kwa sherehe ambazo zitafuatiwa na mazungumzo ya Kiserikali kati ya Tanzania na Afrika Kusini.
Baada ya mazungumzo kutafuatiwa na utiaji saini wa mikataba na makubaliano katika Nyanja mbalimbali kati ya nchi hizo mbili,na baadaye viongozi hao watazungumza na waandishi wa habari.
Rais Kikwete pia atatembelea Uwanja wa Uhuru akiandamana na mwenyeji wake Rais Zuma.
Mchana viongozi hao wawili watashiriki chakula cha mchana pamoja na wafanyabiashara wa Tanzania na Afrika Kusini ambako watazungumza kuelezea umuhimu wa kuimarisha uhusiano wa kibiashara na kiuchumi kati ya nchi hizo mbili.
Jioni, Rais Zuma ataandaa dhima ya kitaifa kwa ajili ya Rais Kikwete na ujumbe wake kwenye Nyumba ya Wageni ya Rais wa Afrika Kusini.
Rais Kikwete na ujumbe wake watatembelea pia mji wa Cape Town wenye historia ambao ndio kilipo Kisiwa cha Robben ambako wapigania uhuru wa Afrika Kusini, wakati wa ubaguzi wa rangi akiwamo Rais Mstaafu Nelson Mandela walifungwa kama wafungwa wa kisiasa.
Rais Kikwete atarejea nyumbani Alhamisi,Julai 21, 2011.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
18 Julai, 2011
No comments:
Post a Comment