Na Nova Kambota,
Naam! kwa hili siwezi kukaa kimya, siwezi kukubali linipite kirahisi rahisi hivi ndivyo navyoanza uchambuzi wangu huu wa leo ambao unalenga kujadili kwa undani kuhusu hotuba ya Rostam Aziz aliyoitoa juzi tarehe 13 siku ya jumatano mwezi huu mwaka 2011 huko Igunga wakati akitangaza rasmi kujiuzulu Ubunge na ujumbe wa kamati kuu ndani ya CCM.
Nitamulika kipengele kimoja baada ya kingine kwanza kwa lengo la kuwaelewesha wasomaji wangu mtazamo wangu lakini pili ni kumtumia ujumbe Rostam na wafuasi wake kuwa watanzania tupo macho tunafatilia siasa za nchi yetu mwisho wa yote kwa vile hotuba ya Rostam ilikuwa imejengwa kwa misingi ya hoja, mantiki na ufundi mkubwa wa fasihi nami nitatembea kwa mapigo hayohayo ya hoja, mantiki na fasihi.
UTANGULIZI
Katika sehemu hii ya hotuba ya Rostam anasema kuwa ameamua kuzungumza na “wazee wa Igunga” , hapa kuna jambo linajificha, tena kuna utata mkubwa sana wa Rostam kuamua kuzungumza na wazee, kuzungumza na wazee ni style aliyokuwa anaitumia Mwalimu Nyerere wakati akizungumza mambo mazito na wazee wa Dar es salaam, kwa maana nyingine mantiki ya Rostam kuzungumza na wazee wa Igunga inalenga kutuhabarisha kuwa alikuwa akizungumza mambo mazito? Sasa je kujiuzulu kwake ni jambo zito kwa nani? kwa wana Igunga? Wazee wa Igunga? WanaCCM? Au watanzania? Kwanini liwe jambo gumu? Mbona hata Nyerere na Kawawa waliwahi kutoka kustaafu uongozi CCM? je Rostam ni nani ndani ya CCM? je upi uzito wa Rostam?
YATOKANAYO
Hapa Rostam anaonyesha wazi yeye ni mtu wa namna gani? tena anasisitiza kwa maneno haya “Nyinyi wenyewe ni mashahidi wazuri kwamba tangu matukio yanayogusa jina langu yaanze kutokea miezi michache tu baada ya serikali ya Awamu ya nne inayoongozwa na Rais Jakaya Kikwete kuingia madarakani mwaka 2005, tumekuwa tukiyapuuza na kuendelea kufanya kazi kwa bidii”, sasa hapa Rostam anasema alikuwa anayapuuza matukio yale, hebu tujiulize kwanini mtu anapuuza kitu? Mtu makini ni yupi anayepuuza au anayechukua tahadhari? Je tukisema dharau na kupuuza kwake leo hii kumemlazimisha kutema ubunge na ujumbe wa NEC tutakuwa tumemwonea? Labda niseme wazi kuwa Rostam siyo kwamba alikuwa anapuuza bali kinachoonekana minyukano ya kimakundi ilipamba moto na kujikuta wenzake wamemzidi kete kiasi kwamba hata utetezi wake ungepuuzwa, kwani mara ngapi alijaribu kujitetea? Au tupige kura tubaini watanzania wangapi wanamwona Rostam msafi? Kupuuza haimaanishi ni msafi ila wakati mwingine yaweza kuwa ni tuhuma za ukweli kiasi kwamba mtu anashindwa hata kujitetea.
KUJIVUA GAMBA
Hapa Rostam anaonyesha jinsi gani anavyokwepa ukweli, anaacha kusema waziwazi kwa mhusika anawageukia Nape na Chiligati, hivi Rostam anataka tuamini kuwa wanachokifanya Nape na Chiligati hakina baraka za Kikwete? Hivi ndo tuseme Nape na Chiligati ni waropokaji majukwaani? Hawajatumwa na Kikwete? Tukiamini hivi tutakuwa kama tunakimbia ukweli ambao ni lazima tutakutana nao mbele tu, kwa kifupi Rostam alikuwa anamsuta swahiba wake Kikwete kwa mgongo wa Nape na Chiligati. Kwanza kabisa Rostam anamaanisha kuwa Kikwete anang’ata na kupuliza kwa maana yeye hakusema kwenye kamati kuwa “magamba” lazima waondoke ndani ya siku 90 lakini wakati huohuo Rostam hajasema iwapo Kikwete aliwahi kuwaonya Nape na Chiligati kuwa waache kujitungia maneno yao hivyo Rostam anamaanisha kuwa Kikwete alikuwa nyuma ya Nape na Chiligati hivyo Rostam anaonesha jinsi gani swahiba wake Kikwete amemwacha asombwe peke yake na mawimbi ya minyukano na makundi ndani ya chama.
MAAMUZI YANGU
Hapa ndipo ambapo Rostam kaniacha mdomo wazi na imani sio mimi peke yangu bali wengi wameshangaa kauli zake zilizojaa ubinafsi. Rostam anasema kuwa hana ameamua kuacha uongozi kwasababu siasa za kupakana matope zinamjeruhi kibiashara, hivyo Rostam kaona bora biashara zake kuliko wananchi wa Igunga halafu “eti nimesikia wanamlilia” ajabu sana , hapa kuna mambo mawili matatu yaliyojificha, la kwanza ni kuwa Rostam kwake biashara kwanza na kuwatumikia wananchi ni kiporo tu, pili tunarudi kulekule wafanyabiashara wengi wanawania ubunge ili kulinda maslahi yao ya kibiashara na si vinginevyo na tatu laana ya baba wa taifa inatuandama aliwahi kutuonya kuwa makini na matajiri wanaojichomeka kwenye siasa tuwahoji mara mbilimbili nia yao , sasa nadhani watanzania wameona kuwa wafanyabiashara huwa wapo kimaslahi na wanapoona hawapati basi hawaoni kazi kuchukua uamuzi wowote hata ikibidi kujiuzulu.
HITIMISHO
Naomba nihitimishe kwa kutoa mapendekezo kadhaa;
Kwanza kabisa mpaka sasa Rostam hajaonyesha kupinga shinikizo la Nape la kumtaka kung’atuka, hivyo amekubali kosa , siwezi kujadili maneno yake kuwa hakubaliani na shinikizo kwasababu ikiwa anapinga shinikizo la Nape na Chiligati basi hakupaswa kujiuzulu badala yake alipaswa kwenda mahakamani kupinga kudhalilishwa au angewataka wanaomtuhumu kumfikisha mahakamani.
Pili Rostam aache kuwafanya watanzania watoto eti kwa kauli kuwa ataendelea kuwa mwanachama mwaminifu wa CCM, nani kasema? Nasema labda Nape na Chiligati waondoke vinginevyo ni swala la muda tu ila misuguano itaendelea tu.
Tatu natoa wito kwa Kikwete ajivalishe nafasi ya Nyerere, je angekuwa Nyerere angefanya nini? je angevumilia mazingaombwe “CHAPA KUJIUZULU” au angeongeza na “CHAPA TAIFISHA MALI ZAO” , Naam nasema tena “vision 2015” itazidi kuiyumbisha CCM , naona wapigane na mfumo mbovu ambao usiwe na mipaka hata ikibidi serikali kung’oka naona ing’oke tu ili kunusuru nchi vinginevyo kwa mbali naanza kuamini utabiri wa baba wa taifa aliposema “CCM watakapoanza kugawanyika mjue itaanguka” na huu kama si mgawanyiko ni nini basi? Tafakari!
Nova Kambota Mwanaharakati,
Tanzania, East Africa
Ijumaa, 15 julai, 2011.