Mgeni Rasmi katika ufunguzi wa Fainali za Mashindano ya Mchezo wa Pool Taifa ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Kibakwe Mh. George Simbachawene (wa tatu kulia) pamoja na mwakilishi wa Kampuni ya bia Tanzania (TBL) mkoa wa Dodoma,Nick Tesha (watatu kushoto) wakipiga mipira ya mchezo wa pool kwa pamoja kuashiria kuzinduliwa rasmi kwa fainali za Taifa za mashindano yamchezo huo leo kwenye ukumbi wa Kilimani Club,Mjini Dodoma.
Na Mwandishi Wetu,Dodoma.
MBUNGE wa Jimbo la Kibakwe mkoani Dodoma ambaye pia ni mwenyekiti wa vikao vya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, George Simbachawene ameitaka serikali kuutambua mchezo wa pool kama ilivyo michezo mingine.
Mbunge huyo ameyasema hayo leo wakati alipokuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa fainali za taifa za mashindano ya mchezo wa pool yanayojulikana kama ‘Safari Lager Nationa Pool Championship 2011’.
Fainali za mashindano hayo zinazoshirikisha mikoa 14 ya Tanzania Bara ambazo zinadhaminiwa na kampuni ya bia ya TBL kupitia bia yao ya Safari Lager zinafanyikia kwenye ukumbi wa Kilimani Club mkoani hapa.
Simbachawene alisema kuwa awali kulikuwa na dhana ya kuwa mchezo wa pool ni mchezo wa wahuni hadi serikali ikawa inafikiria kuuzuia lakini dhana hiyo haipo tena hivyo serikali haina budi kuupokea na kuutambua kama ilivyo michezo mingine.
“Naiomba serikali kuanza sasa iutambue mchezo wa pool kama ilivyo michezo mingine kwani ni mchezo mzuri ambao unashirikisha watu wenye heshima zao ikiwemo hata sisi wabunge ambao wiki iliyopita tuliucheza na kuufurahia,”alisema Simbachawene.
Aliongeza kwa kukitaka chama cha mchezo huo nchini (TAPA) kuhakikisha kinausajili mchezo huo kwa kutumia sheria ya mchezo wa ridhaa badala kuusajili kama mchezo wa kamari.
“Mchezo wa pool ni mchezo wa kutumia akili na viwango, hivyo TAPA usajili mchezo huu kwa kutumia sheria ya mchezo wa ridhaa badala ya kuusajili kwa sheria ya mchezo wa kamari na wanaotaka kucheza michezo ya kubahatisha (kamari) waende kwenye klabu za usiku,”alisema.
Aidha aliipongeza kampuni ya bia Tanzania (TBL) kupitia bia ya Safari Lager kwa kuweza kuupatia mafanikio makubwa mchezo huo kutokana na udhamini wao .
Naye mwakilishi wa kampuni ya TBL mkoani Dodoma, Niki Tesha alisema kuwa mafanikio ya mchezo huo yametokana na kampuni hiyo kudhamini michezo nchini.
“Kampuni ya TBL inadhamini na kujali michezo nchini na ndiyo maana mchezo huo ambao zamani ulikuwa ukibezwa umeweza umeweza kupiga hatua na kufikia hapa ulipo,”alisema Tesha.
Ufunguzi wa fainali hizo ulihudhuriwa pia na Afisa michezo mkoa wa Dodoma,Patrick Ernest pamoja na Afisa Utamaduni wa mkoa huo, Abuu Layya.
No comments:
Post a Comment