Madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya wamesema uongozi wa Chimala Saccos umekuwa hautendi haki wakati wa kutoa mikopo kwa wananchi na badala yake wamekuwa wakiutumia ushirika huo kujinufaisha wao na familia zao.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika kikao cha Baraza la Madiwani wamesema kuwa sehemu kubwa ya mkopo wa shilingi bilioni 4 umewanufaisha viongozi wa Ushirika huo na sio wananchi.
Wakitoa azimio la pamoja chini ya mwenyekiti wa halmashauri hiyo KENETH NDINGO Wametaka kufanyika kwa ukaguzi wa vitabu vya Saccos wilayani humo ili kudhibiti vitendo vya baadhi ya viongozi wa Ushirika kujinufaisha wao na familia zao.
Awali Ofisa Ushirika wa wilaya ya Mbarali John Manyama, amesema Chimala saccos inazo hisa zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni sitini na tano na laki saba akiba ya zaidi ya shilingi milioni mia nne sitini na tisa elfu na amana ya zaidi ya shilingi milioni sitini na mbili.
Kwa mujibu wa Manyama mikopo iliyotolewa na Chimala saccos hadi sasa ni zaidi ya shilingi milioni 4 na kwamba marejesho hadi sasa ni zaidi ya shilingi milioni 3 huku kiasi cha mkopo ambacho bado hakijarejeshwa ni zaidi ya bilioni moja.
MANDAMANO YA WANANCHI KATA YA UTENGULE USANGU - MBARALI.
Zaidi ya wakazi 80 wa kata ya Utengule Usangu iliyopo wilayani Mbarali wameandamana hadi ofisi ya Diwani wa kata hiyo kupinga kuhamishwa kwa Dakta Joseph Megafu kutokana na mchango wake katika kituo cha Afya cha Utengule.
Wamesema dakta huyo anamchango mkubwa katika kutoa huduma kwa akina mama na watoto na kwamba kuhamishwa kwake kunaweza kuzorotesha utoaji wa huduma kwa kundi hilo muhimu ndani ya jamii.
Aidha inadaiwa kuwa mpango wa kuhamishwa kwa dakta huyo unatokana na umakini alionao katika kusimamia huduma kwa jamii.
Naye Diwani wa kata hiyo Juntiva Mwalyaje amepokea malalamiko hayo na kuwataka kuwa watulivu wakati akiliwasilisha ombi lao kwa mganga mkuu wa wilaya ambaye ndiye mwenye dhamana ya kumrejesha Dakta JOSEPH MEGAFU kuendelea kutoa huduma katika kituo hicho cha afya.
USAFI WA MAZINGIRA KATA YA ILEMI JIJINI MBEYA.
Juhudi za vyombo vya habari kwa kushirikiana na uongozi wa kata ya Ilemi jijini Mbeya kutoa elimu ya usafi wa mazingira, wakazi wa Mtaa wa Mwafute wameanza kuchukua hatua ya kusafisha maeneo yao ikiwa ni pamoja na kujenga Ghuba za kuhifadhia taka.
Afisa mtendaji wa kata hiyo Bwana Stivu Mwamboneke amesema baada ya vyombo vya habari kuhamasisha usafi wa mazingira wakazi wa eneo hilo wamekuwa na mwamko wa kusafisha mazingira yanayo wazunguka ikiwa ni pamoja na kuzuia maji machafu kutiririka kwenye mto Jihanga.
Aidha amewaomba waandishi wa habari kutembelea maeneo hayo ili kuwahamasisha wakazi hao kuendeleza usafi wa mazingira na kukarabati vyoo vyao.
WIZI NA ULINZI KATA YA SINDE JIJINI MBEYA.
Wakazi wa mtaa wa Janibichi kata ya Sinde jijini Mbeya wanaishi kwa wasiwasi mkubwa wa kuvunjiwa nyumba zao kisha kuibiwa vitu vya thamani kutokana kuibuka kwa vitendo vya wizi mtaani hapo.
Mwenyekiti wa mtaa huo Bwana Joel Kitwika amesema wizi huo hufanywa nyakati za usiku wakati wengine wakiwa wamelala ndipo wezi hao hupata nafasi ya kuiba baadhi ya vitu na mifugo kama kuku na bata.
Aidha amewataka wakazi wa mtaa huo kuweka ulinzi wa jadi (Sungusungu) ili kudhibiti vitendo hivyo na kuwataka vijana kujitokeza kwa wingi pindi wanapohitajika kuunda kikosi cha Sungusungu kwenye mtaa wao.
HABARI NA MWANDISHI WETU MBEYA
HABARI NA MWANDISHI WETU MBEYA
No comments:
Post a Comment