Thursday, August 11, 2011

Pinda ampuuza mbunge aliyeghushi saini yake

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, amesema hatua iliyochukuliwa na Mwenyekiti wa Bunge, George Simbachawene, kuhusiana na mbunge aliyeghushi saini yake inatosha.
“Inawezekana kama wameleta, maana wakati mwingine napata makaratasi mengine na kwamba kama wameleta formally kama barua, inawezekana ikawa kwenye mail (sanduku) kwa sababu muda mrefu sijapata nafasi ya kwenda kuangalia,” alisema.


Alisema hata kama akiipata hilo jina la mbunge aliyeghushi saini yake, asingependa kuchukua hatua, ambayo italifanya kuwa kama jambo kubwa ndani ya Bunge.

Alisema madhali mwenyekiti wa Bunge kishawaonya, basi ni sahihi.

“Hata nikiipata nitareact. Lakini nisingelipenda likawa ndio jambo kubwa ndani ya Bunge kama vile ni kubwa sana. Madhali tumeshawaonya, basi inatosha limalizike hivyo hivyo,” alisema.

Alisema wakati mwingine wabunge wamekuwa wakiona raha kumsumbua na kuandika ujumbe mfupi unaosomeka kwamba: “Nakuomba uje hapa haraka sana kuna jambo la dharura nataka nizungumze nawe. Kule chini anachoandika Waziri Mkuu na kisha Mizengo Pinda.”

Alisema ujumbe huo unapofika kwa mbunge na ukizingatia hakuna hata siku moja, ambayo aliwahi kumtania, atainuka na kwenda kwake.

“Unapofika namie nageuza kiti, najua kuna jambo unataka kuzungumza na wewe. Unasema si umeniita, yule aliyeandika ‘ki-note’ anasema leo kapatikana kweli pale. Na mimi kwa sababu sijakuita nasema sijakuita labda kama una jambo nawe unasema haya sawa mzee unaondoka,” alisema.

Alisema ulipokuja ujumbe wa kwanza hakujali sana, lakini mara ya pili ndipo alipoona mambo hayo yamezidi.

“Kilipotokea kile cha pili nikasema hili sasa limezidi na hii ya pili tena ndio nikaamua kumwambia Lukuvi (Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-Sera, Uratibu na Bunge), haya matani mengine haya unaweza ukafanya mtu aka collapse (akazimia) bure. Kwa hiyo awatahadharishe wabunge wasichukue mambo mengine ya mzaha mzaha, wakati mnapokuwa kwenye mambo serious (makini),” alisema.

Alisema tangu siku lilipotolewa tamko bungeni, hajaona jambo kama hilo likitokea tena.

Kaimu Katibu wa Bunge, John Joel, aliwahi kukaririwa na NIPASHE, akisema mbunge huyo alipatikana na kwamba jina lake lilikabidhiwa kwa Waziri Mkuu siku hiyo hiyo.

Alisema walilikabidhi jina hilo kwa Waziri Mkuu ili aamue kama atamchukulia hatua ama la na kwamba wamefanya hivyo kwa sababu hakuna mtu aliyelalamikia tukio hilo.

Hata hivyo, alikataa kusema mbunge huyo anatokea chama gani wala jina lake.

Mbunge huyo anadaiwa kuandika ujumbe mfupi wenye sahihi ya Waziri Mkuu kwenda kwa Mbunge wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini, akidai kuwa anaitwa na kiongozi huyo mkuu wa shughuli za serikali bungeni.
CHANZO: NIPASHE

No comments: