Friday, August 12, 2011

Pinda amshangaa Mbowe kuhusu madiwani
WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda amewaruka viongozi wa Chadema, akiwamo Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe akisema hawakufikia hatua ya kuunda kamati ya pamoja ya kitaifa katika mazungumzo yao ya wiki iliyopita kuhusu kutafuta suluhu ya mgogoro wa Umeya wa Jiji la Arusha. Msimamo huo wa Waziri Mkuu unapingana na ule wa Mbowe aliyetangaza mara baada ya mazungumzo hayo kwamba wamekubaliana kuunda tume hiyo na taarifa yake ya awali ikiwa imepokewa na kujadiliwa na Kamati Kuu (CC) ya Chadema iliyoketi mjini Dodoma kuanzia Agosti tano hadi sita. Mbowe katika mkutano wake na waandishi wa habari mnamo Agosti saba, mwaka huu mjini Dodoma, alisema: “Kamati hii itakuwa na wajumbe kutoka CCM na Chadema, itaundwa haraka iwezekanavyo ndani ya mwezi mmoja na Mwenyekiti anatarajiwa kuwa Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa.” Hata hivyo, akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Dk Mary Mwanjelwa katika kipindi cha maswali ya kwa Waziri Mkuu, bungeni jana, Pinda alikiri kukutana na Mbowe na Katibu Mkuu wake, Dk Willibrod Slaa, kujadili hali ya kisiasa isiyoridhisha jijini Arusha kutokana na mgogoro huo wa umeya, lakini akasisitiza kuwa hakukuwa na makubaliano ya moja kwa moja ya kuunda kamati. Pinda alisema alipokea ombi la Mbowe kutaka kufanya naye mkutano huku pia akiomba awepo na Dk Slaa, lakini akasema alistuka kuona taarifa katika vyombo vya habari kwamba amekubaliana na viongozi hao wa upinzani kuunda tume hiyo. Alisema katika mazungumzo hayo, aliwaeleza viongozi hao kwamba kwa kuwa suala hilo ni la kisiasa litakuwa nje ya uwezo wake lakini anaweza kumuomba Msajili wa Vyama vya Siasa aweze kusaidia uwepo wa mazungumzo hayo na kushangaa lakini alishangaa kuona Chadema kutangaza hadharani kuwapo kwa tume wakati ndiyo kwanza mchakato ulikuwa unaanza. “Nilikutana na Mbowe Agosti sita mwaka huu saa tatu asubuhi, baada ya kuniomba nikutane nao nyumbani kwangu. Katika mazungumzo yetu lilijitokeza suala la Arusha ambalo walionekana kulitilia shaka na kutaka upatikane ufumbuzi kwa maslahi ya wananchi.” Pinda alisema msimamo wake katika mazungumzo hayo ulikuwa kwamba kama ni ufumbuzi huo wa kisiasa asingeweza kutoa majibu ya moja kwa moja huku akisisitiza, kama ni sheria basi anayeona hakutendewa haki angekwenda mahakamani.Lakini, aliongeza, “Niliwaeleza kuwa suala hilo Msajili wa Vyama vya Siasa (John Tendwa), angeweza kutusaidia…, niliwaeleza kuwa nitamtafuta msajili na kumweleza aandike barua kwa CCM na Chadema ili kuvikutanisha vyama hivyo...” “Juzi nilipomuona mheshimiwa (Mbowe) akizungumza kuwa tumekubalina hivyo (kuunda tume ya muafaka) nilishangaa…,hakuwa sahihi, namshukuru Mwanjelwa kwa kulileta suala hili kwa ajili ya kupatiwa ufafanuzi.” Kutokana na majibu hayo Mwanjelwa alitaka kusikia ushauri wa Waziri Mkuu kwa madiwani wa Arusha waliofukuzwa.
Akijibu swali hilo Pinda alisema: “...Nilichomshauri Mbowe, nilimwabia maamuzi anayokwenda kuyafanya Arusha ni ya Chadema, lakini busara inahitajika, busara yenyewe ni kuendelea na hali iliyopo mpaka hali itakapokuwa nzuri.” “Sasa nashangaa maamuzi waliyochukua ya kuwafukuza madiwani, sijui hayo mazungumzo yatakuwaje. Ushauri wangu kwa madiwani waliofukuzwa kama wanaona si sahihi waende mahakamani.”

Chanzo - Mwananchi

No comments: