Jeshi la Polisi Visiwani Zanzibar limeanza ukaguzi wa mipaka yake ya ardhi na kuwekea alama za kudumu katika maeneo ambayo hayajapimwa ili kuepuka migogoro kati yake na wananchi.
Afisa Uhusiano wa Jeshi la Polisi Zanzibar, Inspekta Mohammed Mhina, amesema kuwa hatua hiyo imechukuliwa ili kuyanusuru baadhi ya maeneo ambayo yakiachwa bila ya kupimwa ama kuwekewa alama za kudumu yanaweza kuwa hatarini kumegwa.
Akizungumzia hatua hiyo, Mkuu wa Maendeleo na Ujenzi wa Jeshi la Polisi Zanzibar Kamishna Msaidizi Mwandamizi SACP Hamisi Juma, amesema kuwa kutokana na kuongezeka kwa thamani ya ardhi, wananchi wamekuwa wakijipenyeza kuingia na hata kumega baadhi ya maeneo yaliyotegwa kwa ajili ya majengo na kambi za Majeshi ya Ulinzi na Usalama.
Kamanda Juma alikuwa akizungumza wakati wa ukaguzi na upimaji wa ardhi eneo linalotarajiwa kujengwa kituo cha Polisi cha Fumba nje kidogo ya mji wa Zanzibar ambapo amesema Jeshi la Polisi limejiwekea utaratibu wa kufanya ukaguzi wa maeneo yake ya mipaka ya ardhi na kupima maeneo mapya yalitengwa kwa ajili yake.
Amesema kwa siku za hivi karibuni kumekuwa na migogoro ya ardhi ambayo mara nyingi imekuwa ikipelekea mifarakano baina ya mtu mmoja na mwingine na hata baadhi ya mingine hupelekea mapigano na hata mauaji jambo ambalo Polisi halitaki kujikuta katika migongano na wananchi.
Kamanda Juma amesema ili kuepuka hali hiyo, Jeshi la Polisi kama chombo cha kudumisha ulinzi na usalama halitaweza kukubali kujiingiza kwenye migogoro na wananchi wake ambao wanawategemea sana katika kuwapatia Polisi taarifa za wahalifu na kushirikiana katika suala la Polisi Jamii na Ulinzi Shirikishi.
Akizungumzia upimaji wa maeneo na ujenzi wa Kituo cha Polisi cha Fumba, Kamanda wa Polisi mkoa wa Mjini Magharibi Zanzibar ACP Aziz Juma Mohamme, amesema kuwa kituo hicho kitakapokamilika kitasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza kero ya upatikanaji wa huduma ya Polisi karibu na wanchi.
No comments:
Post a Comment