Thursday, August 18, 2011

Wabunge wamlipua Luhanjo wa Ikulu




Katibu Mkuu Kiongozi Phillemon Luhanjo
WAMTUHUMU NDIYO CHANZO KIKUU CHA UFISADI MALIASILI NA UTALII, MWENYEWE ANG'AKA
Neville Meena, Dodoma
KAMATI ya Wabunge wa CCM imeendelea kuwa mwiba kwa Serikali baada ya jana baadhi yao kumtaja kwa jina, Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo kwamba ni chanzo cha ufisadi na uozo katika Wizara ya Maliasili na Utalii.
Wabunge hao wamemtaja Luhanjo ikiwa ni siku moja baada ya kukataa kufungwa mdomo katika kujadili Bajeti ya Maliasili na Utalii na kutaka iwasilishwe kwanza bungeni ili wapate fursa ya kuchangia kama wabunge wengine, kuliko kuwa na msimamo wa kichama katika kuipitisha bila kuijadili kwa kina na uwazi.


Jana, kamati hiyo ilikutana mnamo saa 7:00 mchana katika kikao ambacho kilichukua takriban saa mbili na nusu na kutoa maelekezo magumu yanayoitaka Serikali kuchukua hatua za kukabiliana na wizi, ufisadi na ubadhirifu wa mali ya umma unaofanywa kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii, inayoongozwa na Waziri Ezekiel Maige.


Maelekezo mengine yaliyotolewa na wabunge hao kwa mujibu wa taarifa ambazo zilipatikana ni kumtaka Waziri Maige kushughulikia tatizo la ukabila katika Idara ya Wanyamapori, kufutwa kwa vibali vya kukamata na kusafirisha wanyama hai nje ya nchi na kurejeshwa kwa wanyama waliotoroshwa na kupelekwa nje Novemba mwaka jana, kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).


Habari za uhakika kutoka ndani ya kikao hicho zilidokeza kwamba awali, wabunge hao walikuwa wametishia kukwamisha bajeti ya wizara hiyo kama walivyofanya ile ya Nishati na Madini, lakini waliridhishwa na ahadi za Serikali kwamba itachukua hatua stahili.


Kwa mujibu wa habari hizo, Luhanjo alitajwa kwa jina kwamba amekuwa chanzo cha utendaji mbovu katika Idara ya Wanyamapori iliyoko chini ya wizara hiyo kwa kushawishi uteuzi wa watendaji kwa misingi ya ukabila ili kulinda kile kilichodaiwa kuwa ni maslahi yake binafsi.


“Hata orodha ya watendaji wa idara hiyo ambao wanatoka kwa mheshimiwa huyo wa Ikulu imesomwa pale na tumeomba Serikali ichukue hatua, sasa watafanya nini watajua wao wenyewe,” kilisema chanzo hicho cha habari na kuongeza:


“Idara hiyo ni nyeti na ndiyo inasimamia wanyamapori, sasa haiwezekani watendaji wake wote wakatoka sehemu moja tu ya nchi tena kabila moja, hapa tumenusa kitu na tumesema Serikali ikifanyie kazi.”


Awali, wabunge hao walihusisha hata uhamisho wa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Maimuna Tarishi kwamba ulilenga kulinda kile kilichodaiwa kuwa ni “maslahi ya Luhanjo” wizarani hapo lakini baadaye walijulishwa kuwa katibu mkuu huyo hakuwa sehemu ya mkakati huo.


Luhanjo aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, kabla ya kuhamishiwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.


Baada ya Rais Jakaya Kikwete kuingia madarakani alimteua kuwa Katibu Mkuu Kiongozi kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Martin Lumbanga ambaye sasa yuko Geneva, Uswisi akiiwakilisha Tanzania katika mashirika ya Umoja wa Mataifa yaliyoko nchini humo.


Luhanjo anena
Alipopigiwa simu kujibu madai hayo ya wabunge Luhanjo alionekana kupata taarifa hizo kabla ya kupigiwa simu kwani aliuliza: “Unaulizia hao wabunge waliokutana kwenye kikao na Waziri Mkuu siyo... sasa unasemaje?”


Baada ya kuulizwa juu ya tuhuma hizo alijibu kwa kifupi: “Sikubaliani na hoja zao hizo, si kweli ni majungu, achana na hiyo kitu bwana.”


“Mimi ni Katibu Mkuu Kiongozi wa nchi nzima, sasa hayo mambo ya wizara mimi naingiaje huko, si kweli kabisa na mimi sikubaliani nao,” alisema kisha kukata simu akijiepusha na kombora hilo.


Kamati ya Bunge
Mapema akisoma maoni ya Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, mwenyekiti wake, James Lembeli alisema kamati yake inasikitishwa na hatua ya Serikali kupuuza mapendekezo yake kuhusu suala la kufuatilia na kurejeshwa kwa wanyama waliotoroshwa nchini.


“Mapendekezo hayo ya kitaalamu yalilenga kuisaidia Serikali kuhakikisha upatikanaji wa wanyama hao. Ni jambo la kufedhehesha Mheshimiwa Spika, kuona kwamba tangu utoroshwaji wa wanyama hao ufanyike Novemba 24, 2010 hadi leo bado Serikali ilikuwa haijui wanyama hao wako wapi hali inayotia shaka na kuhoji kulikoni?,” alisema Lembeli na kuongeza:


“Yapo maswali mengi ya kujiuliza kuhusu suala hili la utoroshwaji wa wanyama hao. Katika wanyama 116 waliotoroshwa wenye thamani ya Sh163,732,500 ni pamoja na twiga wanne. Kama ndivyo, Kamati inauliza kwa nini Sheria ya Wanyamapori inayozuia raia wa kigeni kupewa leseni ya kukamata wanyama wakiwamo twiga ambao ni nembo ya taifa haikuzingatiwa?”


Alisema hali hiyo inaashiria kuwapo kwa dalili kubwa ya uzembe na kulindana ndani ya Wizara ya Maliasili na Utalii na kwamba hicho ndicho chanzo cha kigugumizi katika kuchukua hatua.


Lembeli alisema shaka hiyo inajidhihirisha wakati wa uhamisho wa maofisa uliofanyika hivi karibuni na kwamba haukuwagusa kabisa wa kitengo cha Uwindaji wakiwamo wa Arusha na kuongeza kwamba licha ya kadhia hiyo ya kutorosha wanyama, baadhi ya maofisa hao wamepandishwa vyeo.


Kamati hiyo ya Bunge iliitaka Serikali kuwabaini wote waliohusika na kashfa hiyo na kuwafikisha kwenye vyombo vya dola mara moja, huku ikipendekeza kuwepo kwa ofisa wanyamapori wa kudumu katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro ambacho nyara nyingi zinazosafirishwa nje hupitia.


Mwananchi

No comments: