Thursday, August 18, 2011

WAKUNGA HOSPITALI YA IGAWILO MATATANI KWA KUSABABISHA KIFO CHA MTOTO




WAKUNGA na wauguzi wa hospitali ya Igawilo iliyopo Jijini Mbeya, wameingia matatani baada ya kuhusishwa na kifo cha mtoto mchanga.

Habari za uchunguzi zinaeleza kwamba, uzembe wa wakunga na wauguzi hao katika ukataji wa kitovu ndio uliosababisha kifo cha mtoto huyo wa kike aliyezaliwa akiwa na uzani wa kilo 3.5.

Tukio hilo lilitokea Agosti 17 mwaka huu katika hospitali hiyo majira ya saa sita mchana baada ya Bi. Naumi Fredy (23) kujifungua salama.

Hata hivyo, taarifa zinasema kwamba, wakati wa ukataji wa kitovu wakunga na wauguzi hao walimweleza kuwa mtoto wake alikuwa na matatizo ya kupumua.

Akizungumza na mtandao huu katika Hospitali ya Wazazi yaMeta alikohamishiwa kabla ya kifo cha mwanaye, mama huyo alisema uamuzi wa kupelekwa kwenye hospitali hiyo ulitokana na matatizo ya kupumua ya mtoto huyo huku akiwa tayari amekatwa kitovu.

Bi. Naumi alisema kwamba kwa uzoefu wake ukataji wa kitovu cha mwanaye haukufanywa kwa usahihi na ndicho chanzo cha mauti ya mtoto huyo.

Baada ya kuhamishiwa kwenye Hospitali ya Meta, madaktari walimwekea mtoto huyo mashine ya kupumua, lakini kwa kuwa tayari alikuwa ameathirika na hali hiyo, huduma hiyo haikuweza kusaidia.

Kutokana na hali hiyo iliyojitokeza, baba mzazi wa mtoto huyo Tumaini Asajile (28) aliamua kufungua kesi katika Kituo Kikuu cha Polisi mkoani Mbeya ambayo namba ya jalada ni MB/IR/7286/2011.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Advocate Nyombi, hakuweza kupatikana kuzungumzia suala hilo, lakini askari aliyeshika jalada hilo na kuomba hifadhi ya jina lake, alisema kwamba suala hilo litafanyiwa uchunguzi.

Kwa hisani ya Tanzania Yetu

No comments: