Akizungumza na Mtandao wa Sufianimafoto, Mkurugenzi wa Kundi hilo, Amini Salmini, alisema kuwa tayari wamekwishakamilisha jumla ya nyimbo nane ikiwa ni sawa na albam mbili kwa mpigo.
Aidha alisema pamoja na kukamilika kwa nyimbo za albam ya pili lakini bado haijapewa jina kutokana na ukali wa kila wimbo uliomo katika albam hiyo na kuwafanya kuwa na kigugumizi kuchagua jila albam hiyo ya pili.
Albam hiyo inatarajia kuanza kuuzwa siku ya uzinduzi wa kundi hilo ambao unatarajiwa kufanyika Oktoba 28 mwaka huu jijini Dar es Salaam, ambapo kwa sasa tayari nyimbo mbili zimekwisha sambazwa katika Vituo mbalimbali vya Redio ili kuwasikilizisha mashabiki wa miondoko hiyo.
Kundi hilo linatarajia kurudi mjini Zanzibar kuweka Kambi na kuendelea na mazoezi yamaandalizi ya uzinduzi wao ambapo wanatarajia kuvunja Kambi rasmi siku mbili kabla ya uzinduzi.
“Tumeamua kurekodi albam mbili kwa mpigo ili tuweze Kuwapa raha mashabiki wetu pindi tutakapoanza kufanya maonyesho yetu ya majukwaani,
Na pia baada ya tu ya kukamilisha zoezi hili la kurekodi sasa wasanii wote watarejea mjini Zanzibar kuweka kambi na kuendelea na mazoezi hadi siku mbili kabla ya uzinduzi, tumeamua kufanya hivyo ili kuwafanya wasanii wetu waweze kufanya vitu kwa uhakika na kujiamini zaidi.” Alisema Amini
Alizitaja nyimbo hizo zilizokwisharekodiwa kuwa ni pamoja na, Aliyeniumba Hajanikosea, itakayobeba albam hiyo iliyoimbwa na Bi Mwanahawa Ally, Unavyojidhani Hufanani, iliyoimbwa na Jokha Kassim, Mchimba Kaburi Sasa zamu yake Imefika, iliyoimbwa na mkali wa BSS, Mrisho Rajab na Top Bongo, iliyoimbwa Hassan Ally.
Nyimbo nyingine ni, Riziki Shoti Kati, iliyoimbwa na Aisha Masanja, Umelisusa Tembele Hela ya Nyama unayo, iliyoimbwa na Hasina Kassim, Majungu yenu Kwetu ni Riziki, iliyoimbwa na Shinuna Kassim na Nipo Simpo, iliyoimbwa na Mosi Suleiman.
No comments:
Post a Comment