Thursday, September 1, 2011

Vodacom yaidhamini timu ya taifa mbio za mashua kwenda Msumbiji

Ofisa Udhamini wa Vodacom Tanzania Ibrahim Kaude (Kulia) akiwakabidhi Tshirt wawakilishi wa Tanzania kutoka timu ya taifa ya Mbio za Mashua watakaoshiriki mbio za "All African Games Sailing" zitakazofanyika Maputo Msumbiji kuanzia Septemba 3 hadi 11. Vodacom imeidhamini timu hiyo kwa shilingi milioni 8/-.
Wawakilishi wa Tanzania kwenye mashindano ya mbio za mashua za "All African Games Sailing" zitakazofanyika Maputo Msumbiji kuanzia Septemba 3 hadi 11 wakiwa wameshikilia bendera ya Taifa waliokabidhiwa kabla ya kuondoka. Kutoka kushoto ni Meneja Uhusiano na habari za Mtandao wa Vodacom Tanzania Matina Nkurlu,Ibrahim Kaude Ofisa Udhamini wa kampuni hiyo iliyodhamini timu hiyo kwa shilingi Milioni 8/-.
Wawakilishi wa Tanzania kwenye mashindano ya mbio za mashua za " All African Games Sailing" zitakazofanyika Maputo Msumbiji kuanzia Septemba 3 hadi 11 wakiteta jambo mara baada ya kukabidhiwa bendera ya Taifa. Vodacom Tanzania imeidhamini timu hiyo kwa shilingi milioni 8/-.
Na Mwandishi Wetu
Kampuni ya mawasiliano ya Vodacom Tanzania imewadhamini washiriki watatu wa Timu ya Taifa ya Mbio za Mashua kwenda Maputo Msumbuji kuliwakilisha taifa kwenye mbio za mashua zitakazofanyika Septemba 3 hadi 11 kwa shilingi Milioni 8/-.
Wachezaji walioenda kuliwakilisha taifa kwenye mbio hizo zitakazoshirikisha baadhi ya nchi za Afrika 'All African Games Sailing' kutoka timu hiyo inayofanyia mazoezi yake kwenye ufukwe wa Yacht Club ni Watanzania Mwambao Helef, Halife Mpondi na Hassan Said wameondoka leo (jana) kuelekea nchini Msumbuji.
Mwenyekiti wa Kamati ya Utendaji ya Chama cha Mashua Tanzania (TSA) Phillemon Nassari amesema kuwa ana uhakika vijana wake ambao wamefanya mazoezi makali kwa kipindi cha miezi mitatu wataliwakilisha vema taifa na kuliletea medali ya dhahabu.
Akifafanua Nassari alisema kuwa mbio hizo zitakazoshirikisha mataifa mbalimbali ya Afrika zitakuwa na changamoto baada ya kila nchi kudai kwamba imejiandaa vizuri ili kuwa bingwa wa jumla kwa mashindano hayo.
"Fedha hizi zilizotolewa na Vodacom Tanzania ni matumaini yetu zimetoa hamasa kwa washiriki wetu kwenda kufanya vizuri msumbiji. Wamejiandaa vya kutosha kwa takribani miezi nane ambapo kila wiki walikuwa wakifanya mazoezi mara moja kwenye ufukwe wa Yatch Club," alisema Nassari.
Mbali na hayo Mwenyekiti huyo wa Kamati ya Utendaji wa TSA aliiomba serikali kuigeukia na kuitilia uzito michezo mingine ikiwemo ya baharini hususan wa mashua.
Nae Alli Bush ambaye ni bingwa wa mashua kwa Afrika aliekuwa akifanya mazoezi na wawakilishi hao alisema amewakubali na kwamba vijana hao wameiva kwenda kuiwakilisha Tanzania kwenye michuano hiyo ya kimataifa.
Kwa upande wake Ibrahim Kaude ambaye ni Afisa Udhamini wa Vodacom Tanzania amesema kwa kuwa kampuni yake imekuwa ikidhamini michezo mbalimbali nchini imeona pia ni vema kuwekeza katika mchezo huo wa mashua nchini.
"Tunajisikia fahari kuwa mmoja ya wadau waliofanikisha kusafiri kwa timu hiyo ya Taifa ya mbio za mashua kwenda mjini Maputo na tunaendelea kudhamini pia michezo mingine lengo likiwa kupandisha hadhi ya Tanzania katika tasnia ya michezo duniani," alisema Kaude.
Mwakani Tanzania inatarajiwa kuwa mwenyeji mashindano hayo ya mbio za mashua za All African Games Sailing yatakayofanyika Agosti 4 hadi 14 kwenye ufukwe wa Msasani chini ya usimamizi wa Yatch Club.

No comments: