Jesca Msambatavangu diwani mteule Kitanzini
Na Francis Godwin
CHAMA cha mapinduzi (CCM) wilaya ya Iringa mjini kimefanya sherehe kubwa za kuwapongeza wananchi wa kata ya Kitanzini na Gangilonga kwa kuchagua wagombea wa CCM huku kikiwataka madiwani wake walioshinda kutowabagua wapinzani katika maendeleo.
Katika sherehe hizo zilizofanyika juzi mjini hapa kwa maandamano makubwa yalioanzia ofisi ya msimamizi wa uchaguzi Kitanzini maandamano hadi ofisi za CCM mkoa yaliyopelekea baadhi ya shughuli kusimama kwa muda ,wafuasi wa CCM walilazimika kuzunguka katika vijiwe mbali mbali vilivyokuwa vikiongoza kwa kuwapinga wagombea wa CCM na kuwataka kuungana pamoja.
Wakizunguza mara baada ya maandamano hayo madiwani wateule wa kata ya Kitanzini kupitia CCM ,Jesca Msambatavangu na kata ya Gangilonga Nicolina Lulandala walisema kuwa kampeni za uchaguzi mdogo wa kata hizo zimekwisha kwa CCM kuibuka mshindi na sasa ni wakati wa kutekeleza ilani ya uchaguzi ya CCM.
Msambatavangu alisema kuwa imani kubwa ambayo wananchi wa kata ya Gangilonga wamepata kuionyesha kwake ni kubwa na hivyo katika kulipa fadhila ya kura zao atahakikisha anafanya kazi kwa jitihada zaidi na kuepuka siasa za makundi katika kuwatumikia wananchi wote bila kujali itikadi zao za vyama .
Alisema kuwa kata ya kitanzini ni moja kati ya kata zenye vuguvugu kubwa ya upinzani na kuwa kushinda kwake ni matumaini ya wananchi wa kata hiyo ambayo wameendelea kuonyesha kwake na CCM .
Hivyo alisema kuwa ahadi zake kwa wananchi wa kata hiyo zitatekelezwa kwa wakati kama alivyopata kuahidi na ahadi zilizomo katika ilani ya CCM pia atahakikisha zinatekelezwa kwa wakati.
Jesca katika uchaguzi huo alichuana vikali na mgombea wa Chama cha demokrasia na maendeleo (chadema) Gervas Kalolo ambaye alipata nafasi ya pili huku wagombea wa vyama vya NCCR mageuzi na CUF wakiambulia kura 4 kila mmoja.
Kwa upande wake diwani mteule wa kata ya Gangilonga Nicolina Lulandala alisema kuwa wananchi wa kata hiyo wategemee kuona maendeleo ya kweli katika kata hiyo na kuwaomba wale wote ambao walikuwa wakimpinga katika kampeni kushirikiana katika kuleta maendeleo ya kata hiyo.
Katibu wa CCM wilaya ya Iringa mjini Lusiano Mbosa mbali ya kuwapongeza wananchi kwa kuonyesha imani kwa CCM bado alisema kuwa CCM itaendelea kutekeleza ilani yake kwa kata zote kama ilivyowaahidi wananchi wakati wa kampeni na kuwataka viongozi wa vyama vya upinzani kuacha kupotosha ukweli kuhusu kazi zinazofanywa na serikali ya CCM.
No comments:
Post a Comment