Tuesday, November 29, 2011

Posho za wabunge zazua mjadala


Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe
Waandishi Wetu NYONGEZA ya posho za wabunge imewakera wasomi, wanasiasa na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania(Tucta) ambao kwa nyakati tofauti jana, walieleza kutoridhishwa na hatua hiyo.Posho za vikao vya wabunge imeongezeka kutoka Sh70,000 kwa siku walizokuwa wakilipwa awali, mpaka Sh200,000 fedha ambayo ilianza kulipwa tangu Mkutano wa Bunge uliopita. Kutokana na ongezeko hilo, kwa sasa kila mbunge atakuwa akilipwa Sh80,000 kama posho ya kujikimu anapokuwa nje ya jimbo lake, posho ya vikao (sitting allowance) Sh200,000 na mafuta ya gari Sh50,000 kila siku sawa na Sh 330,000 kwa siku. Nyongeza hiyo ya posho za vikao imefanya bajeti ya Bunge kwa ajili ya posho za vikao kufikia Sh28 bilioni kwa mwaka. Zitto adai ni usaliti Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, alisema kuwa ameshtushwa na taarifa za kupandishwa kwa posho za vikao kwa wabunge huku wananchi wakiugulia ugumu wa maisha na kusema kuwa ipo siku Watanzania watawapiga mawe kwa usaliti huo. “Nimeshtushwa zaidi kwamba posho hizi zimeanza kulipwa katika mkutano wa Bunge uliopita kabla hata Rais hajaamua, maana maslahi yote ya wabunge huamuliwa na Rais baada ya kupokea mapendekezo ya Bunge kupitia Tume ya Bunge,” alisema Zitto. Aliwataka wabunge wote kutambua kwamba, kuamua kujipandishia posho bila kuzingatia hali ya maisha ya mwananchi wa kawaida ni usaliti usio na mfano. “Mbunge yeyote ambaye anabariki jambo hili labda anaishi hewani, haoni taabu za wananchi au ni mwizi tu na anaona ubunge ni kama nafasi ya kujitajirisha binafsi,” alisema Zitto. Aliwataka pia wabunge wa Chadema, wajue uamuzi kuhusu posho ni wa chama na ni wa kisera. “Mbunge yeyote wa Chadema anayepokea posho za vikao anakwenda kinyume na maamuzi ya sera za chama tulizoahidi wananchi wakati wa uchaguzi,” alisema Zitto. Alisema kuwa amemwomba Katibu Mkuu wa chama chake kuitisha kikao maalumu cha Kamati Kuu ya chama kujadili suala hilo. Alisema kuwa tangu Juni 8 mwaka huu, alikataa kupokea posho za vikao na kuwa, popote anapohudhuria vikao huwa anaomba risiti za posho anazokataa. “Baadhi ya wabunge kama Januari Makamba wamekataa posho na hata kwenye semina ya kamati ya nishati alikataa na tumeona kwenye vyombo vya habari jina lake likiwa limekatwa ilhali viongozi wakubwa kabisa wamechukua posho,” alisema Zitto. Alieleza kwamba anampongeza Makamba kwa uzalendo wake na kuwataka wabunge wengine wenye moyo wa dhati kukataa siyo tu ongezeko la posho bali posho yote ya vikao. “ Kwa nini mbunge akubali kulipwa kwa kukaa? Tazama nchi hii, juzi Serikali ilipokea msaada wa Sh20 bilioni kwa ajili ya Sensa ya mwakani wakati wabunge wanalipwa Sh28 bilioni kama posho ya kukaa tu kwa mwaka,” alisema Zitto. Tucta wawaka Akizungumza na Mwananchi jana, Katibu Mkuu wa Tucta, Nicolaus Mgaya alisema kitendo cha wabunge hao kujiongezea posho ni ishara ya kushindwa kutetea maslahi ya wananchi wao waliowapeleka bungeni. “Tucta inalaani kitendo cha wabunge kujiongezea posho kubwa kama hizo huku wakijua kuwa wananchi waliowachagua wanawategemea wao, hasa katika kipindi hiki kigumu cha maisha. Jambo hilo linaonyesha wazi kuwa hawako kwa ajili ya kutetea maslahi ya wananchi, bali kujinufaisha wenyewe,” alisema Mgaya. Alisema wabunge hao wameshindwa kujali hali ya wananchi wao hasa katika kipindi hiki cha mfumuko wa bei, hali ngumu ya maisha na migongano ya hapa na pale, badala yake wameamua kujipigia debe ili waweze kunufaika wenyewe. "Nasema hawafai, huu ni unyonyaji,"alisema. AlisemaTucta inapinga kitendo hicho na imeitaka Serikali kuangalia upya suala la posho ili kusiwe na matabaka kati ya wabunge na wafanyakazi wengine ambao ndio msingi wa uchumi wa taifa. Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana alisema uamuzi wa kuongeza posho kwa wabunge unatakiwa kuchukuliwa kwa umakini kwa kuwa suala hilo limepigiwa kelele kwa muda mrefu. “Tanzania ni nchi masikini, vipaumbele vya kulikomboa taifa letu vipo vingi na bado havijatekelezwa. Ubunge ni utumishi na kama ni hivyo wabunge wanatakiwa kuishi kama wanavyoishi wananchi wengine,” alisema Dk Bana. Mhadhiri mwingine wa Chuo hicho, Bashiru Ally alisema suala hilo litatengeneza matabaka kati ya aliye nacho na asiye nacho. “Tunapaswa tujenge taifa la kujitegemea kulingana na hali ya uchumi wetu na sio kuiga mambo ya watu, watawala kupenda kuwa katika nafasi za juu kwa misingi ya kupata fedha ni tatizo,” alisema Bashiru. Shibuda adai posho muhimu Mbunge wa Maswa Mashariki (Chadema), John Shibuda alisema suala la wabunge kuongezewa posho halina ubaya wowote kwa kuwa litawafanya wasiwe ombaomba. Shibuda ambaye katika mkutano wa Bunge la Bajeti alipingana na sera ya chama chake iliyokuwa katika Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2010 kuhusu posho za vikao, alisema ili mbunge atekeleze majukumu yake vizuri ni lazima alipwe fedha ya kutosha. “Umefikia wakati Waafrika tulinde fedheha kwa viongozi wetu ili wasiwe ombaomba. Viongozi wakilipwa vizuri wataweza kuitumikia nchi na jamii inayowazunguka, ipasavyo. Kutokulipwa vizuri ndio mwanzo wa viongozi kusaini mikataba mibovu,” alisema Shibuda. Makamba ashtushwa Mbunge wa Bumbuli, January Makamba, alieleza kushangazwa na ongezeko hilo la ghafla akisema kamwe wabunge wasifikiri kuwa wanaweza kumaliza matatizo yao au ya wapigakura wao kwa fedha ya posho. Alisema kitendo cha wabunge kuongezewa posho za vikao kwa asilimia 185.7, kinaleta jazba kwa wananchi ambao wanahangaika kila kukicha kwa ugumu wa maisha. “Kwenye jamii lazima kuwe na usawa, kama watu tupo kwenye hali mbaya (ugumu wa maisha) lazima wote tuenende sawa. Wabunge kuongezewa posho kwa asilimia 185 siyo sawa kabisa, tunajiweka mbali na wananchi na wanatuona tunafaidika sana wakati wao wanateseka kwa ugumu wa maisha,” alisema Makamba. Alisema kuwa, kutokana na msimamo wake huo, Juni mwaka huu alikataa posho iliyotolewa na Wizara ya Nishati na Madini baada ya kuhudhuria semina iliyoandaliwa na wizara hiyo. “Tulikaa kwenye semina kwa saa mbili, tunamaliza naletewa karatasi nisaini posho ya Sh280,000. Nilikataa. Nilikataa kwa sababu nilitambua kuwa ile ni kazi yangu kama mbunge, sasa unanilipa hela ya kazi gani?” alihoji Makamba. Habari hii imeandaliwa na Fredy Azzah, Frederick Katulanda, Mwanza, Patricia Kimelemeta, Fidelis Butahe na Ellen Manyangu


Mwananchi

No comments: