Thursday, October 20, 2011

MWANAFUNZI ANUSURIKA KUUWAWA KWA KUCHOMWA MOTO

Hapa kijana Erick Mduda akiwa ameshika redio ambayo alikwenda kuiba katika gari hilo ambalo amekalia hapa ni baada ya kunaswa.
Mkazi wa Frelimo Muungano mjini Iringa akimtwanga vichwa mwanafunzi. Erick Mduda baada ya kufumwa akiiba radio katika gari.
Kijana Erick Mduda akiomba msamaha ili asiuwawe baada ya wananchi kupendekeza kuchomwa moto
Mwanafunzi Erick Mduda akijaribu kutimua mbio baada ya kupokea kipigo kikali kutoka kwa wananchi wenye hasira kali usiku huu.
Hapa Mwanafunzi Erick Mduda akiandaliwa kwa ajili ya kuchomwa moto baada ya kupoteza fahamu kwa muda baada ya kupigwa na rungu kichwani na wananchi wenye hasira kali.
WANANCHI wenye hasira kali wakazi wa eneo la Muungano kata ya Mwangata katika Manispaa ya Iringa nusuru wamuue kwa kumchome moto Mwanafunzi wa kidato cha kwanza ‘B’ katika shule ya sekondari ya Kwakilosa katika manispaa ya Iringa Erick Mduda baada ya kukamatwa akivunja gari na kuiba radio ndani ya gari hilo lililoegeshwa eneo la kanisa la TAG eneo la Frelimo Muungano.


Tukio hilo limetokea ndani ya dakika 10 majira ya saa 2 usiku huu baada ya
umeme kukatika ambapo kijana huyo kibaka alipata kuitumia nafasi hiyo kwa kuingia ndani ya gari hilo na kufanikiwa kuiba radio hiyo kabla ya kukamatwa na wananchi hao wenye hasira kali na kutaka kumchoma moto baada ya kijana huyo kuonekana kuishiwa nguvu kwa kipigo cha nguvu alichopokea.


Wakizungumzia juu ya tukio hilo wakazi wa Muungano walisema kuwa walitaka kumuua kijana huyo kwa kumchoma moto baada ya kuwa wamechoshwa na matukio ya wizi na upigaji nondo yaliyopata kutokea katika eneo hilo kabla ya kumamatwa kwa watuhumiwa nane hivi karibuni ambao juzi walisomewa kesi ya kumuua kijana Damasi Kisinga ambaye aliuwawa kwa kupigwa nondo eneo hilo la kata ya Mwangata.


Hata hivyo walisema kuwa mwanafunzi huyo alikutwa ndani ya gari hilo akiendelea kuiba baadhi ya vitu huku akiwa tayari amefanikiwa kuifungua radio ya gari hilo.


Mwanafunzi huyo Erick Mduda ambaye ni makazi wa Kata ya Mkwawa anadai kufika katika eneo hilo la Kanisa kwa kushiriki mkutano wa injili unaoendelea katika kanisa hilo na baada ya umeme kukatia anadaiwa kutoka eneo la kanisa hilo na kusogea nyumba ya jirani ambako kulikuwa na gari aina ya Taxi ambayo imeegeshwa katika eneo hilo baada ya kuwa bovu.


Hata hivyo katika maelezo yake aliyotoa mwanafunzi huyo wakati akiomba asiuwawe alisema kuwa alifika eneo hilo kuiba radio hiyo ili kuweza kuitumia katika chumba chake (geto) kutokana na wazazi wake kushindwa kumwekea radio katika chumba chake.


Pia alikiri kuwa na ushirikiano wa karibu na mtandao wa vijana nane waliokamatwa kwa upigaji nondo katika kata hiyo ya Mwangata ambao kwa sasa wamekamatwa na polisi na kuwa alikuwa akitumwa na vijana hao kuingia katika nyumba mbali mbali na kuiba.


Diwani wa kata ya Mwangata Mheshimkiwa Galus Lugenge amethibitisha kukamatwa kwa mwanafunzi huyo Erick Mduda kwa tuhuma za wizi na kuwa bila huruma za wasamaria wema katika kunusuru uhai wa mwanafuzi huyo hivi sasa angekuwa ameuwawa kwa kuchomwa moto.


Katika hatu nyingine diwani huyo amempongeza Afande Tedy ambaye ni mkuu wa upelelezi wilaya ya Iringa mjini kwa kazi nzuri na ushirikiano ambao ameendelea kutoka pindi waharifu wanapokamatwa katika kata hiyo huku akisikitishwa na askari Nhongo Kuyela kwa hatua yake ya kutaka kuwapiga ngumi wasamaria wema ambao walisaidia kuokoa maisha ya kibaka huyo mwanafunzi na kumfikisha polisi.


Hata hivyo alisema kuwa kitendo cha polisi huyo na wenzake kutaka wasamaria wema waliookoa maisha ya kijana huyo kutumia gharama zao kwenda kumtibu Hospital baada ya kumfikisha kituo cha polisi ni moja kati ya mapungufu ya utendaji kazi wa baadhi ya askari hali ambayo inaweza kuvunja ushirikiano kati ya raia na polisi.


Wakati huo huo mwanafunzi huyo kibaka amedai kuibiwa simu yake wakati wa heka heka za wanachi kumpa kipigo .


Alidai kuwa simu hiyo aliyoibiwa ni ile ambayo alikuwa akiitumia kupata mwanga wakati wa kufungua radio hiyo katika gari hilo.

CHANZO: FRANCIS GODWIN

No comments: