Rais Dr.Jakaya Mrisho Kikwete akihutubia katika ufunguzi wa Mkutano wa Biashara wa Jumuiya ya Madola kwenye ukumbi wa Mikutano wa Burswood convetion centre jijini Perth, Australia,. Picha na Freddy Maro-IKULU
---
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa Bara la Afrika sasa linalo kila aina ya sifa na uwezo wa kuwa Nguzo Kuu ya Uchumi Duniani (Global Economic Power House) katika karne ya 21, kama nyenzo nyingi zilizoko katika Bara hili zitaweza kuendelezwa ipasavyo.
Rais Kikwete ameliambia Baraza la Biashara la Nchi Wanachama wa Jumuia ya Madola (Commowealth Business Forum) mjini Perth, Australia, leo, Alhamisi, Oktoba 27, 2011 kuwa, hata hivyo, ili Bara la Afrika liweze kufikia hadhi hiyo, ziko changamoto kadhaa ambazo lazima zitafutiwe utatuzi ili kufungua uwezo mkubwa wa Afrika kiuchumi.
Akitoa Mada Kuu (Keynote Address) kwenye mkutano huo unaofanyika kwenye Kituo cha Mikutano cha Burswood, Rais amesema kuwa uwezo huo wa Bara la Afrika unatokana na utajiri mkubwa wa maliasili pamoja na uwezo wa watu wake ambazo ni nyenzo muhimu kwa ajili ya maendeleo na ukuaji wa uchumi.
Rais kikwete amesema kuwa Bara la Afrika, kwa mfano, lina asilimia 60 ya ardhi yote inayofaa kwa kilimo duniani, inayo maji ya kutosha juu na chini ya ardhi kwa ajili ya umwagiliaji na linalo hali ya hewa inayofaa kwa kilimo, sifa zinazolifanya Bara la Afrika kuwa na uwezo wa kuzalisha chakula cha kutosha kulisha dunia nzima.
Rais Kikwete amesema kuwa kinachohitajika ni kufanya mageuzi makubwa katika kilimo cha Afrika ili kukitoa katika hali yake ya sasa ya kilimo kinachotawaliwa na ukulima wa kujikimu, kilimo cha jadi, kilimo kilicho duni, kilimo chenye tija ndogo na kukifanya kilimo cha kisasa.
“Hili litahitaji uwekezaji mkubwa wa Serikali na sekta binafsi katika zana za kisasa, umwagiliaji mkubwa zaidi, matumizi ya mbegu bora na zinazozalisha mazao mengi zaidi, dawa za kuua wadudu na matumizi makubwa zaidi ya mbolea,” Rais amewaambia wafanyabiashara na watumishi waandamizi wa Serikali mbali mbali za nchi za Jumuia ya Madola.
Mbali na nafasi kubwa ya kuboresha kilimo, Rais amesema kuwa Bara la Afrika lina nyenzo na utajiri mkubwa wa madini, mafuta na gesi, misitu na utajiri kutokana na viumbe vya majini.
Amesema Rais Kikwete: “Kati ya nchi 11 zinazoongoza kwa madini duniani kwa kuwa na angalau aina moja ya madini muhimu 10 ziko katika Afrika, Afrika ina asilimia 10 ya akiba ya mafuta duniani, asilimia 50 ya akiba ya dhahabu duniani, asilimia 98 ya akina ya madini ya Chromium duniani, asilimia 90 ya madini yaliko katika kundi la madini aina ya cobalt na platinum, asilimia 70 ya madini aina ya tantaline, asilimia 64 ya madini aina ya manganese na theluthi moja ya madini ya aina ya uranium duniani,”
Kuhusu utajiri wa nishati, Rais Kikwete amesema kuwa Bara la Afrika lina utajiri mkubwa wa nyanzo vya kuzalisha umeme na kuwa katika miaka michache iliyopita, uzalishaji wa mafuta na gesi asilia katika Afrika umeongezeka sana.
“Hivi ninavyozungumza nanyi, kuna nchi 19 zinazozalisha kiasi cha kutosha cha mafuta. Isitoshe kuna shughuli nyingi za utafutaji wa mafuta na gesi katika Bara letu. Karibuni nchi yetu ya Tanzania nayo imeingia kwenye ramani ya nchi zilizogundua gesi asilia na makampuni mengine mengi yanaendelea kutafuta gesi zaidi,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Kwa upande wa uzalishaji umeme kutokana na vyanzo vya maji, Afrika pia ina uwezo na utajiri mkubwa katika eneo hilo. Kwa mfano, kwenye chanzo kimoja tu cha umeme cha Inga kwenye Mto wa Congo, kuna uwezo wa kuzalisha megawati 39,000 za umeme.”
Rais Kikwete amesema kuwa isitoshe nchi nyingi za Afrika sasa zina sera nzuri za kiuchumi. “Utabiri wa karibuni zaidi wa IMF (Shirika la Fedha Duniani) unaonyesha kuwa nchi saba kati ya 10 ambazo chumi zake zitakuwa zinakua kwa kasi zaidi duniani katika muongo ujao zitakuwa katika Bara la Afrika. Chapisho la Benki ya Dunia la “Africa’s Pulse” lililotolewa mwezi uliopita linasema kuwa nchi 11 kati ya 15 ambazo chumi zake zinakua kwa kasi zaidi kwa mwaka huu wa 2011, ni nchi za Afrika.”
Isitoshe, Rais Kikwete amesema kuwa katika nchi nyingi za Afrika, kuna ongezeko kubwa la uwekezaji katika eneo la miundombinu ya barabara, reli, bandari na viwanja vya ndege ambazo ni nyenzo muhimu katika maendeleo ya nchi yoyote.
Baada ya kuwa ametoa mada hiyo, Rais Kikwete ameshiriki katika mkutano uliozungumzia uwekezaji katika sekta ya madini kati ya Tanzania na Australia. Mikutano yote miwili imefanyika chini ya uenyekiti wa Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP, Bwana Reginald Mengi ambaye ni mmoja wa viongozi wa Commonwealth Business Forum na ambaye pamoja na wafanyabiashara wengine wa Tanzania anahudhuria mkutano wa Baraza hilo.
No comments:
Post a Comment