Sunday, October 23, 2011

Ujumbe Wa China Wamtembelea Rais Dk. Shein Zanzibar

Rais wa Zanzibar na Mwenyekitim wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein,akipokea zawadi kutoka kwa kiongozi wa Madaktari kutoka China Naibu Mkuu Idara ya Afya katika jimbo la Jiangsu,Zhou Zhengxing,ikulu mjini Zanzibar,jana ujumbe huo umekuja katika kuimarisha sekta ya Afya.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekitim wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein,akizungumza na ujumbe wa madaktari kutoka jimbo la jiangsu,nchini China ukiongozwa na Naibu Mkuu Idara ya Afya katika jimbo hilo,Zhou Zhengxing,(wa pili kushoto),pia Balozi mdogo wa China anyeishi Zanzibar,Chen Qiman,aliongoza ujumbe huo,Ikulu Mjini Zanzibar.
Picha Na Ramadhan Othman
NA HABARI MAELEZO ZANZIBAR
UJUMBE kutoka Jimbo la Jiangsu nchini China umeeleza azma yake ya kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika uimarishaji wa sekta ya afya ikiwa ni pamoja na kuanzisha upasuaji kwa njia za kisasa na mradi wa tabasamu kwa kuwafanyia upasuaji watoto wanaozaliwa na athari za midomo.
Ujumbe huo ulieleza hayo leo Ikulu mjini Zanzibar, wakati ulipokuwa na mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein. Katika mazungumzo, ujumbe huo kutoka Jimbo la Jiangsu nchini China ukiongozwa na Naibu Mkuu wa Idara ya Afya wa Jimbo hilo Bwana Zhou Zhengxing ulieleza kuwa lengo kuu la ujio wao ni kuendeleza uhusiano na Zanzibar katika sekta ya afya.
Ujumbe huo ambao pia, uliambatana na Balozi Mdogo wa China anayefanyia kazi zake hapa Zanzibar Bibi Chen Qiman ulieleza kuwa Jimbo la Jiangsu lina mambo mengi ya kujivunia katika mashirikiano na uhusiano na Zanzibar. Akitoa maelezo kwa Rais pamoja na mafanikio yaliopatikana katika Jimbo hilo la Jiangsu kiongozi wa ujumbe huo bwana Zhengxing alisema kwa mashirikiano ya pamoja Jiangsu ina mpango huo wa kuanzisha upasuaji wa kutumia njia za kisasa pamoja na mradi huo wa tabasamu unaohusu upasuaji kwa watoto wanaozaliwa na athari za midomo. Alieleza kuwa ni imani yake kuwa kutokana na azma hiyo itazidi kupanua zaidi ushirikiano wa kitaalamu pamoja na kuimarisha ushirikiano katika kubadilishana utaalamu kwa ajili ya kukuza afya ya jamii.
Kiongozi huyo wa ujumbe huo alieleza kuwa Jiangsu na Zanzibar zina uhusiano katika uimarishaji wa sekta ya afya kwa takriban miaka 47 hivi sasa. Alisema kuwa mashirikiano katika sekta hiyo hayakuimarisha huduma katika sekta ya afya pekee bali yameweza kuimarisha urafiki mkubwa uliopo baina ya pande mbili hizo. Bwana Zhengxing aliwasifu watu wa Zanzibar kwa ukarimu wao wanaowafanyia madaktari kutoka China ambao hufanya kazi zao Zanzibar. ‘Ijapokuwa ni mara yangu ya kwanza kuja Zanzibar nimeweza kujionea mwenyewe urafiki mkubwa uliopo kati ya watu wa Zanzibar na China pamoja na Madaktari kutoka China”,alisema Bwana Zhengxing. Nae Balozi Mdogo wa China anayefanyia kazi zake hapa Zanzibar Bibi Chen Qiman alieleza kuwa China inampango wa kujenga hospitali mpya ya kisasa huko Mkoani Pemba ambayo itakuwa hospitali ya Rufaa kwa Pemba.
Aidha, Balozi huyo alieleza kuwa China ina mpango wa kujenga ICU mpya katika hospitali kuu ya MnaziMmoja mjini Unguja. Aidha, Balozi huyo alisisitiza kuwa taratibu zote za ujenzi wa miradi hiyo zinatarajiwa kuanza mapema mwakani. Pamoja na hayo, Balozi huyo alitoa shukurani kwa Rais Dk. Shein na serikali anayoiongoza pamoja na wananchi wa Zanzibar kwa kuendeleza mashirikiano makubwa na China pamoja na watu wake hatua ambayo imepelekea kuimarika uhusiano na udugu.
Nae Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein kwa upande wake alitoa pongezi kwa ujumbe huo kutoka Jimbo la Jiangsu kwa kuja Zanzibar ukiwa na lengo la kuzidisha uhusiano katika uimarishaji wa sekta ya afya. Alisema kuwa tokea aingie madarani ni mara ya tatu ujumbe kutoka nchini China unaohusiana na sekta ya afya kufika afisini kwake hali ambayo inaonesha dhahiri kuwa kumekuwa na uhusiano mwena na wakihistoria kati ya Zanzibar na China.
Dk. Shein alipongeza mafanikio makubwa yaliopatikana katika Jimbo la Jiangsu sanjari na hatua za kuimarisha uhusiano kati yake na Zanzibar tokea mara tu baada ya uhuru wa Zanzibar mwaka 1964. Katika maelezo yake Dk. Shein alieleza kuwa madaktari kutoka Jiansu wamekuwa wakifanya kazi kwa mashirikaino makubwa hapa Zanzibar na kutoa huduma bora kwa wananchi hasa huduma za upasuaji. Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeweka mikakati mbali mbali ya uimarishaji wa sekta ya afya tokea uongozi wa Rais wa kwanza wa Zanzibar marehemu mzee Abeid Amani Karume ambapo pia, iliwahi kuwa ya kwanza katika kuandaa baadhi ya mipango ya huduma ya afya kwa bara la Afrika. Sambamba na hayo Dk. Shein aliueleza ujumbe huo azma ya serikali kuimarisha huduma za afya kwa kuzikarabati hospitali zake za Mkoa na Wilaya pamoja na kuzipatia vifaa vya kisasa sanjari na kuanzisha kitengo cha kutoa huduma za utibabu wa maradhi ya saratani, maradhi ya figo na maradhi ya moyo.

No comments: