WAHITIMU WA MAFUNZO YA UALIMU 2011
Mhe. Waziri wa Elimu na Mafunzo Ufundi, Shukuru Kawambwa, Tunaomba kwanza kukupa pole kwa majukumu mazito uliyonayo katika ujenzi wa taifa letu. Pia tunakupongeza kwa uimara na ushupavu wako katika kusimamia masuala mbalimbali ya Elimu nchini.
Mhe. Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi lengo kuu la waraka huu kwako ni kukufikishia lalamiko letu moja kwa moja.
Sisi ni wahitimu wa mafunzo ya ualimu tangu mwezi wa tano, mwaka huu mpaka hivi leo ni miezi zaidi ya mitano inaelekea sita bado hatujui mstakabali wetu kuhusu kupatiwa ajira . Katika shule nyingi za serikali, mambo si shwari hata kidogo. Kuna upungufu mkubwa wa walimu
wenye ujuzi wa kufundisha. Ni jambo la kusikitisha kuwa walimu wenye vyeti, stashahada na shahada wametoka vyuoni hawajaweza kuajiriwa. Baadhi yetu tunabangaiza ilimradi mkono uingie kinywani.
Zimetoka habari mbalimbali katika vyombo vya habari zinazoleta mkanganyiko na sisi kushindwa kuelewa mstakabali wa ajira zetu utakuwa vipi. Kwa mujibu wa Gazeti la Mwananchi la tarehe 06 November. Naibu katibu mkuu anayeshughulikia Elimu katika Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (JUMANNE SAGINI) alisema, "ajira tayari zimekamilika na tumepokea majina ya waalimu 23,027 na kwamba ifikapo November 15 mwaka huu ajira za waalimu zitakuwa zimetangazwa" Lakini tarehe hii imepita hakuna kilichotangazwa..sasa tunashindwa kuelewa..Je huyu kiongozi alidanganya umma?
Wakati hilo likiendelea Gazeti la HabariLeo la tarehe 13 November likaandika. "NAIBU Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, (PHILIPO MULUGO) amesema serikali itaajiri walimu wapya 23,000 katika kipindi cha mwaka wa fedha ujao" Sasa hapa ndio tunachanganykiwa zaidi mwaka
wa fedha ujao unaanza Julai 2012. Sasa hatuelewi lipi ni lipi kwa sababu kila kiongozi ameongea la kwake. Tunaomba Mh Waziri utoe tamko rasmi kuhusu swala hili.
Mh. Waziri wa Elimu tunatumaini kuwa lalamiko, kilio na ombi letu utalipokea na kulifanyia kazi. Tunakutakia afya tele na mafanikio katika shughuli mbalimbali za ujenzi wa taifa letu na kuinua kiwango cha elimu nchini.
Ahsante sana
No comments:
Post a Comment