Monday, November 21, 2011

JUMLA YA WATOTO 43,000 WANAOISHI MAZINGIRA HATARISHI WAFIKIWA NA WAMA,FHI



Mke wa Rais na Mwenyekiti wa WAMA Mama Salma Kikwete 
--
Na Anna Nkinda – Maelezo
Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) kwa kushirikiana na Family
Health International (FHI) Pamoja Tuwalee wameweza kuwafikia watoto
zaidi ya elfu arobaini na tatu wanaoishi katika mazingira hatarishi
katika mikoa ya Dar es Salaam , Pwani, Morogoro na Zanzibar.



Hayo yamesemwa hivi karibuni na Mkurugenzi wa Mradi wa FHI Pamoja
Tuwalee Priskila Gobba wakati akiongea na wawakilishi wa Sekta binafsi
katika mkutano uliojadili jinsi ya kuwasaidia watoto hao uliofanyika
katika viwanja vya WAMA jijini Dar es Salaam.

Gobba alisema kuwa mchakato wa kuwafikia watoto wanaoishi katika
mazingira hatarishi ulianza mwaka jana mwishoni na kwa kipindi cha mwaka
mmoja wameweza kuzitambua familia zao na mahali wanapoishi na hivyo
kuanza kutoa huduma mbalimbali.

“Baada ya kuwafikia watoto wote hao, watoto 25,198 wameweza kupata
huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwapatia ushauri nasaha ili waweze
kujitambua kuwa wao ni watoto wa jamii na wanatakiwa kupata huduma
muhimu kama watoto wengine, wameweza kupata vyeti vya kuzaliwa na huduma
ya afya”, alisema Gobba.

Aliendelea kusema kuwa watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi wako
wengi mjini na vijijini hivyo basi jamii nzima inatakiwa kuwasaidia
watoto hawa jambo wanalolifanya hivi sasa ni kushirikiana na mashirika
mengine ili waweze kufahamu sababu zinazowafanya wakimbie majumbani kwao
ili waweze kutatua tatizo hilo lisiweze kutokea tena kwa vizazi
vijavyo.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Taasisi ya WAMA Daud Nasibu alisema
kuwa wameamua kuishirikisha Sekta binafsi katika mradi huo kwani huwa
wanafanya kazi ya kuwalea watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi
pia kutokana na shughuli wanazozifanya wanaifikia jamii iliyopo vijijini
kirahisi zaidi.

Nasibu alisema kuwa wataandaa mkakati wa mawasiliano kuhusiana na mradi
huo ambao utawezesha kuishirikisha jamii nzima ndani ya wilaya na
vijijini ili jamii hiyo iweze kuwatambua na kuwaangalia watoto yatima
wanaoishi katika maeneo yanayowazunguka.

“Jamii ya watanzania imejaliwa kuwa na moyo wa upendo na kujitolea
lakini inahitaji kusisitizwa na kuhimizwa ili iweze kuona umuhimu wa
kuwasaidia watoto hawa.

Kama kila Mtanzania ataweza kumsaidia mtoto yatima mmoja, kila mtoto
ataweza kupata huduma na kwa miaka ijayo hakutakuwa na mtoto anayeishi
katika mazingira hatarishi, hakutakuwa na mtoto atakayeshindwa kwenda
shule kwa kukosa ada na vifaa, hakuna mtoto atakayelala na njaa kwa
kukosa chakula”, alisema Nasibu.

Aidha alisema kuwa mradi huo unalenga kuwafikia watoto wengi na
kuwapatia mahitaji yao kwa kutumia jamii , watoto hawataishi katika
vituo vya kulelea watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi bali jamii
inayowazunguka itaweza kuwasaidia watoto hawa huku wakiwa katika mikono
ya wazazi na walezi wao.

Akizungumza kwa niaba ya wawakilishi kutoa Sekta Binafsi Richard
Kasesela Mwenyekiti wa Shirikisho la Sekta Binafsi (Biashara) Afrika
alisema kuwa makampuni mengi yanatoa msaada kwa watoto yatima kwani
Sekta binafsi iko kila mahali hivyo ni rahisi kwao kuwafikisha watoto
ukilinganisha na sekta zingine.

Kasesela alisema, “Kutokana na shughuli zinazofanywa na Sekta binafsi
kuwepo hadi vijijini tumekuwa tukitoa misaada mbalimbali kwa watoto
wanaoishi katika mazingira hatarishi walioko mijini na vijijini
ukilinganisha na Sekta zingine hivyo basi tukiunganisha nguvu zetu kwa
pamoja tunaweza kuwafikia watoto wengi zaidi na kwa haraka”


Aliendelea kusema kuwa watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi
wakiendelea kuwepo wanaweza kuleta janga kubwa hapo baadaye kwani kuna
kipindi jamii iliacha kuwaangalia watoto ndiyo maana wameongezeka kwa
kasi huku wengi wakiwa wamekosa malezi na misaada.

FHI Pamoja Tuwalee ni mradi wa miaka mitano unafadhiliwa na Serikali ya
Marekani kupitia ofisi ya shirika lao la Maendeleo hapa nchini (USAID
Mission/Tanzania) mradi huo unafanya kazi kazi katika mikoa ya Dar es
Salaam wilaya tatu, Pwani wilaya sita, Morogoro wilaya sita na Zanzibar
wilaya 10.






No comments: