Saturday, November 12, 2011

MAKAMU WA RAIS AZINDUA KAMPENI YA CHANJO YA UGONJWA WA SURUA NA POLIO KWA WATOTO, KITAIFA JIJINI ARUSHA

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Mohammed Gharib Bilal, akisoma hotuba yake wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Chanjo ya ugonjwa wa Surua na Polio kwa watoto kati ya mwezi mmoja hadi miaka mitano, Kitaifa iliyofanyika kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha leo.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akimpa tone la dawa ya Chanjo mtoto, Renatha Faustine (1) wakati wa alipokuwa akizindua Kampeni ya Chanjo ya ugonjwa wa Surua na Polio kwa watoto kati ya mwezi mmoja hadi miaka mitano, Kitaifa iliyofanyika kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha leo Novemba 12, 2011. Aliyembeba mtoto ni mama wa mtoto huyo, Selina Hando Mkazi wa Moshono Arusha. Kulia ni Agness Joseph mkazi wa Mbulu, akiwa na mtoto wake, Marry Emmanuel, wakisubiri kupata chanjo hiyo.
Watoto wa Shule za Msingi, wakipita mblele ya jukwaa la mgeni rasmi Makamu wa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal, na mabango yenye ujumbe wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Chanjo ya ugonjwa wa Surua na Polio kwa watoto kati ya mwezi mmoja hadi miaka mitano, Kitaifa iliyofanyika kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha leo Novemba 12, 2011. Picha na Muhidin Sufiani-OMR.

Na Mwandishi Maalum – Arusha

Makamu wa Rais Dk. Mohammed Gharib Bilal amezindua kampeni ya chanjo ya kitaifa ya surua na kuwataka wananchi kote nchini kujitokeza kuwapeleka watoto kwenye vituo vya kutolea huduma ya chanjo ili chanjo hiyo iwafikie wote kwa asilimia 100.

Katika hafla hiyo iliyofanyika leo katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid,mjini Arusha Dk. Bilal alizindua pia kampeni ya utoaji wa matone ya polio,Vitamin “A” na dawa za minyoo kwa watoto wa chini ya umri wa miaka mitano.

Akifafanua, Makamu wa Rais alisema sayansi ya utoaji chanjo ya surua kwa watoto waliokamilisha miezi 9 inasisitiza kuwapata watoto wote kwa asilimia 100, lakini kiwango cha chanjo ya surua hapa nchini kimefikia asilimia 92.

“Takribani asilimia 10 ya watoto ambao hawakupatiwa chanjo, kuna uwezekano mkubwa wa kupatwa na ugonjwa wa surua na hatimaye kusababisha kutokea kwa mlipuko wa surua baada ya miaka mitatu,” alieleza Dk. Bilal na kuongeza “Ili kuthibiti mlipuko, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, kupitia Mpango wa Taifa wa Chanjo hulazimika kufanya kampeni ya chanjo ya surua kila baada ya miaka mitatu.”

Alisema Serikali na wadau wake inaendelea na jitihada za kununua na kusambaza chanjo za kutosha,kuongeza vituo vya kutolea huduma ya chanjo hadi kufikia vituo 6,300 na pia kuongeza huduma za mkoba kwa maeneo yasiyofikika na yasiyo na vituo vya kutolea huduma za chanjo zikijumuishwa na huduma nyingine za mama na mtoto.

Alibainisha kuwa kampeni hiyo ya siku nne imelenga kuwapatia chanjo ya surua takribani watoto milioni 6.7 wa kuanzia miezi tisa hadi umri chini ya miaka mitano, chanjo ya polio watoto milioni 7.9 walio chini ya miaka mitano, watoto milioni 7.1 wa umri kati ya miezi sita hadi chini ya miaka mitano watapata matone ya Vitamin A na watoto milioni 6.2 walio na umri kuanzia mwaka mmoja hadi chini ya miaka mitano watapewa dawa za minyoo.

“Kuwapatia chanjo kutawasaidia watoto wote kutopata maradhi mbalimbali,ambayo yanazuilika kwa chanjo na hivyo kuwa na afya njema. Kukamilisha chanjo kutaiwezesha Serikali kutumia fedha ambazo zingetumika kugharamia wagonjwa na matibabu ziweze kutumika katika miradi mingine ya maendeleo,”alisema Makamu wa Rais.

Alisema Serikali imepata mafanikio makubwa katika kufikia malengo ya millennia kwa kupunguza vifo vya watoto chini ya miaka mitano kutoka vifo 112 kati ya watoto 1,000 kwa mwaka 2005 hadi kufikia vifo 81 kati ya watoto 1,000 kwa mwaka 2009 na kwamba lengo hilo limeweza kufikiwa ikiwa ni pamoja na kuhakikisha watoto wengi wamepatiwa chanjo.

Kwa mujibu wa Dk. Bilal tiba ya ugonjwa huo na madhara yake yana gharama kubwa kutokana na ukweli kwamba surua husababisha hususan vifo, upofu au ulemavu wa maisha.

Awali akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii,Dk. Hadji Mponda alisema mbali ya chanjo zilizopo, wizara yake inatarajia kuanzisha chanjo ya kuzuia magonjwa ya vichomi na kuhara kwa watoto pamoja na saratani ya shingo ya kizazi itakayotolewa kwa wasichana.

Alisema matumizi ya ratiba mpya ya chanjo ya vichomi na kuhara yataanza Januari 01, mwakani na chanjo ya saratani ya shingo ya kizazi itatolewa kwa wasichana wa umri wa miaka 9 na itatolewa kwa awamu ukianzia mikoa mitatu ya Dodoma, Dar es salaam na Kilimanjaro.

No comments: