Mke wa Rais,Mama Salma Kikwete akikata utepe kuashiria kuzinduliwa kwa matembezi ya kusaidia watoto wenye mahitaji mbalimbali ya kujikimu na hasa wanaougua ugonjwa wa saratani yaliyoandaliwa na Edge Entertainment Limited na Children in Cross Fire,jijini Dar es Salaam leo
Mke wa Rais,Mama Salma Kikwete akiongea na watu walioshiriki matembezi ya kusaidia watoto wenye mahitaji mbalimbali ya kujikimu na hasa wanaougua ugonjwa wa saratani yaliyoandaliwa na Edge Entertainment Limited na Children in Cross Fire.
Mama Salma Kikwete watatu kutoka kushoto, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Edge Entertainment Co. Limited Edwini Ngere (katikati) na wa pili kushoto Naibu Waziri wa maendeleo ya jamii, jinsia na watoto Ummi Mwalimu wakiwa katika matembezi ya kusaidia watoto wenye mahitaji mbalimbali ya kujikimu hasa wanaougua ugonjwa wa saratani.
Mama Salma Kikwete akiimba wimbo wa taifa pamoja na wanafunzi.
Picha ya pamoja ya Mke wa Rais mama Salma Kikwete na wanafunzi wa shule ya msingi FEZA walioshiriki matembezi ya kusaidia watoto wenye mahitaji mbalimbali ya kujikkimu hasa wanaougua ugonjwa wa saratani.Picha na Mwanakombo Jumaa - Maelezo.
Na Anna Nkinda – Maelezo
Wazazi nchini wametakiwa kutokufuata sana mambo ya utandawazi bali waweke mkazo katika jukumu la kuwalea watoto wao kwenye misingi na maadili ya kitanzania na siyo jukumu hilo kuwaachia mabinti wa kazi peke yao.
Wito huo umetolewa leo na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akiongea na wazazi, walimu na wanafunzi wa shule mbalimbali za jijini Dar es Salaam walioshiriki matembezi ya hisani ya kuwasaidia watoto wenye mahitaji mbalimbali ya kujikimu na hasa wanaougua ugonjwa wa saratani yaliyoandaliwa na Edge Entertainment Limited na Children in Cross Fire.
Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema kuwa hivi sasa wazazi wengi wako busy na kazi za kujitafutia riziki jambo ambalo limewafanya wakose muda wa kukaa na watoto wao na hivyo kuwaacha mabinti wa kazi jukumu zima la kulea watoto hao kitu ambacho si kizuri kwani mtoto anatakiwa kupata malezi ya mzazi.
“Dada wa kazi anafanya kazi ya kukusaidia kulea mtoto wako lakini wazazi wengine mmejisahau kiasi ambacho mnashindwa kutenga muda wa kulea watoto wenu hadi inafikia hatua mtoto akipewa chakula na mzazi wake anakataa kula kwa kuwa hajamzoea lakini akipewa na dada wa kazi anakula kwa kuwa yuko amemzoea na yuko karibu naye”, alisema Mama Kikwete.
Aliwata watoto kuwatii watu wanaowazidi umri kwani hao ni sawa na wazazi wao na waachane na tabia ya kusema kuwa huyu si mzazi wangu hawezi kuniambia jambo lolote kwani mtoto ni wa jamii nzima.
Mwenyekiti huyo wa WAMA aliendelea kusema kuwa jukumu la kusaidia wahitaji ni la kila mtu kwani si jambo jema kutegemea watu wachache au wafadhili kutoka nje ya nchi ili waje kutusaidia kutatua matatizo yetu na hasa pale ambapo sisi wenyewe hatujaanza kuchukua hatua na kupanga mikakati madhubuti ya kuweza kupata ufumbuzi utakaokuwa ni suluhisho la mahitaji mbalimbali katika jamii.
Mama Kikwete alisema, “Matembezi haya yanalenga kuwasaidia watoto wenye matatizo mbalimbali na wasioweza kumudu gharama za mahitaji yao ya kujikimu na matibabu yao pia. Wote tunafahamu kuwa watoto ndio taifa la kesho na tatizo linalomkumba mtoto mmoja ni tatizo linalogusa jamii nzima kwa ujumla kwani mtoto wa Mwenzio ni wako”.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Edge Entertainment Co. Limited Edwini Ngere alisema kuwa kutokana na watoto kuwa wenye uhitaji maalum na watanzania wengi kutokuwa mwamko wa kuisaidia jamii kampuni hiyo ilifanya utafiti katika mikoa sita na kugundua kuwa kuna watoto wanaohitaji kusaidiwa.
Aliitaja mikoa hiyo kuwa ni Dar es Salaam watoto 95 wako katika wodi ya saratani Muhimbili, Arusha kituo cha Fire wasso watoto 66, Kilimanjaro kituo cha Upendo wa mwana watoto 82, Mwanza kituo cha Kuleana watoto 70, Dodoma kijiji cha matumaini watoto 164 na Zanzibar Hospitali ya Mnazi Mmoja watoto 50 wanaishi katika mazingira magumu na kwa matumaini hivyo wanahitaji kusaidiwa.
Ngere alisema, “Mradi huo unatarajiwa kufanyika katika mikoa hiyo huku tukiwa na malengo ya kukusanya shilingi milioni 400 kwaajili ya kuwasaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu na wenye mahitaji mbalimbali na hasa wanaougua ugonjwa wa saratani, katika mkoa wa Dar es Salaam tunatarajia kukusanya shilingi milioni 80 na milioni 64 katika mikoa mingine”.
Zaidi ya shilingi milioni 45 , magodoro 50, sabuni na katoni moja ya soda aina ya Chemicola zilitolewa na wadau mbalimbali waliohudhuria matembezi hayo ambayo yaliendana sambamba na zoezi la uchangiaji.
No comments:
Post a Comment