Monday, November 7, 2011

Ngeleja apongezwa na Wananchi wa Jimboni kwake



Waziri wa Nishati na Madini
William Ngeleja
Na Mwandishi Wetu.

WANANCHI wa Jimbo la Sengerema mkoani Mwanza, wamempongeza mbunge wao, William Ngeleja (CCM), kwa kile walichokieleza kufurahishwa na utekelezaji wake wa miradi ya maendeleo anaoufanya jimboni humo, na wamemuahidi kumchukulia fomu ya kugombea tena nafasi hiyo katika Uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2015.

Mwandishi wa mtandao huu kutoka Sengerema mkoani Mwanza Sitta Tumma anaripoti kuwa ,wananchi hao wamesema, tangu Tanganyika ipate Uhuru wake mwaka 1961, hawajawahi kupata mbunge anayesikiliza na kutatua kero za wananchi wa Sengerema, na kwamba utekelezaji wa miradi ya umeme na barabara za lami jimboni humo, ni kielelezo tosha kwamba mbunge wao huyo anawathamini na kuwajali wananchi wake na Wilaya hiyo kwa ujumla.

Wananchi hao walitoa kauli hiyo mbele ya Ngeleja na viongozi wengine wa vyama na Serikali, kwenye mkutano wa hadhara ulioandaliwa na mbunge huyo ambaye pia ni Waziri wa Nishati na Madini, kisha kufanyika katika Kata ya Katungulu wilayani Sengerema mkoani hapa.

Kwa mujibu wa wananchi hao, Ngeleja na Waziri wa Nishati na Madini, amekuwa mstari wa mbele katika kupigania maendeleo aliyowaahidi wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, na kwamba hawakutegemea kupata barabara za lami na umeme, lakini kwa sasa miradi hiyo imeanza kujengwa na Serikali jimboni na wilaya hiyo, jambo ambalo walisema wapo tayari kumchukulia fomu ya kugombea tena ubunge mwaka 2015.

"Mimi na uzee wangu huu wa miaka 76, sijawahi kumpongeza mbunge yeyote waliopita...lakini leo wewe Ngeleja nakupongeza kwa uchapakazi wake mzuri. Tulikuwa tukililia umeme na barabara ya lami, lakini umetuletea, nasema wewe ni mbogo wa maendeleo ya Sengerema.

"Kutokana na mazuri haya unayotufanyia wanasengerema, mwaka 2015 tutakuchukulia sisi fomu ugombee tena ubunge. Hauna mpinzani...wewe ni mbogo wa maendeleo ya Sengerema", alisema Mzee Ngata Madulu (76), kisha kuungwa mkono na umati mkubwa wa watu waliohudhuria mkutano huo wa hadhara.

Hata hivyo, waliendelea kusema kwamba, juhudi binafsi zinazofanywa na Ngeleja katika kupigania maendeleo ya wananchi wa Sengerema na taifa kwa ujumla, zinaonesha ni jinsi gani amejitolea kuwatumikia vema wananchi, hivyo wanamuombea kwa Mungu aendelee kuwa na afya njema milele.

Kwa upande wake, Ngeleja aliwaahidi wananchi hao kuendelea kuwatumikia vema katika kuwaletea maendeleo makubwa ya kisekta, kwani hiyo ndiyo dhamira yake tangu alipofikilia kugombea nafasi hiyo ya kisiasa.

"Wapo waliodhani sitaweza kitu, lakini kwa sasa hawana cha kusema tena maana maendeleo wanayaona wenyewe. Tumemaliza barabara ya lami ya Busisi Sengerema hadi Geita, na sasa tupo kwenye mpango wa kujenga nyingine ya lami kutoka Kamanga hadi Sengerema...umeme nao nimeleta na Mei mwakani utawaka rasmi", alisema Ngeleja.

Aliwahakikishia wananchi wa Sengerema na taifa kwa ujumla kwamba, Serikali inatambua na kuthamini michango ya wananchi wake, hivyo utekelezaji wa miradi utaendelea ili kuondoa kabisa kama si kupunguza kero zinazowatatiza Watanzania wenyewe.

Kwa mujibu wa Waziri Ngeleja, Serikali imepanga kufikisha umeme kwa kila makao makuu ya wilaya zote nchini, na kwamba mradi wa umeme wa Milleniam Chalange Corparation (MCC), umelenga kuinufaisha mikoa sita pekee, ambayo ni mikoa ya Iringa, Dodoma, Mbeya, Tanga, Morogoro na Mwanza kupitia wilaya yake ya Sengerema, na kwamba mradi huo wa umeme unatarajiwa kukamilika rasmi na kuanza kutumia Mei mwaka 2012.

No comments: