Mkutano wa Tano wa Bunge unatarajia kuanza Jumanne tarehe 8 Novemba, 2011 na kumalizika tarehe 18 Novemba, 2011 mjini Dodoma. Shughuli zitakazokuwepo Katika Mkutano huo, ni kama ifuiatavyo:
1. KIAPOI CHA UTII.
Kutakuwa na Shughuli za Kuwaapisha Wabunge wawili wapya ambao ni, Dkt. Dalay Peter Kafumu (CCM) Mbunge aliyechaguliwa katika uchaguzi mdogo uliofanyika Jimbo la Igunga na Mhe. Mohammed Said Mohammed, Mbunge wa Baraza la wawakilishi aliyechaguliwa kujaza nafasi wazi baada ya kifo cha Mhe. Mussa Amme Silima.
2. MISWADA YA SHERIA YA SERIKALI
Katika Mkutano hujao, jumla ya miswada mitatu (3) itasomwa kwa mara ya pili na kujadiliwa na Bunge. Miswada hiyo ni kama ifuatayo:
• Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali za Biashara wa mwaka 2011. (The Business Law ( Miscellaneous Amendments Bill, 2011)
• Muswada wa Sheria ya Manunuzi ya Umma wa Mwaka 2011. (The Procurement Bill, 2011)
• Muswada wa Sheria ya Mapitio ya marekebisho ya Katiba wa mwaka 2011. (The Constitutional Review Bill, 2011)
Miswada hii yote inaendelea kuchambuliwa na kamati zilizopangiwa za Kamati ya Viwanda na Biashara, kamati ya Fedha na Uchumi, na Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala. Aidha ,hatua iliyofikiwa ni kwamba kamati zote zinaweza kukamilisha shughuli za Uchambuzi siku ya Jumanne tarehe 8/11/2011 na kamati ya Katiba, Sheria na Utawala inatarajiwa kumaliza uchambuzi wake tarehe 11/11/2011.
2. MAAZIMIO YA BUNGE
Katika Mkutano ujao, Bunge linatarajia kuazimia Azimio la Bunge la kuridhia Mkataba wa Vijana wa Afrika (African Youth Charter) la Mwaka, 2006. Azimio hili linatarajia kuingizwa Bungeni endapo Mkataba wake utapatikana na kuwasilishwa kwenye kamati inayohusika ya maendeleo ya Jamii kwa ajili ya Uchambuzi.
4. TAARIFA YA KAMATI TEULE YA BUNGE
Kamati Teule ya Bunge iliyoundwa kwa ajili ya kuchunguza uhalali wa utaratibu wa Wizara ya Nishati na Madini kuchangisha fedha kupitisha Bajeti na kubainisha endapo kitendo cha Katibu Mkuu Kiongozi kutoa taarifa kwa waandishi wa habari juu ya uchunguzi wa suala la fedha zilizokuwa zimechangishwa kimeingilia na kuathiri madaraka ya Bunge, itawasilisha taarifa ya uchunguzi wake na kujadiliwa na Bunge katika Mkutano ujao.
5. HOJA BINAFSI ZA WABUNGE
Mhe, Said Arfi (Mb), Mbunge wa Jimbo la Mpanda kati anakusudia kuleta Hoja binafsi Bungeni kuhusu uwekezaji kwenye ardhi na madhara yake kwa wananchi. Kwa sasa Mhe. Arfi ameombwa awasilishe rasmi hoja yake ili iweze kuangaliwa kama inakidhi matakwa ya Kanuni ya 54 ya Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la 2007.
6. HOJA ZA KAMATI
Aidha Bunge linatarajia kupokea taarifa ya kamati ya Nishati na Madini kuhusu uendeshaji wa Sekta Ndogo ya Gesi Nchini.
7. MASWALI
Katika Mkutano wa Bunge ujao, takribani maswali 125 yanatarajiwa kuulizwa na kujibiwa Bungeni kwa vikao tisa vya Bunge. Aidha katika kipindi cha Maswali kwa Waziri Mkuu, inakadiriwa kuwa Maswali yasiopungua 16 yataulizwa na kujibiwa na Mhe. Waziri Mkuu.
8. SEMINA KWA WABUNGE
Katika Mkutano wa Bunge ujao, semina zifuatazo zitafanyika Bungeni Dodoma wakati wa Mkutano wa Tano wa Bunge:
• Semina kwa Wabunge wote kuhusu tathimini ya Matumizi ya kanuni za Bunge, Toleo la 2007.
• Semina kuhusu Muswada wa Sheria ya Mapitio ya Marekebisho ya Katiba wa Mwaka 2011.
• Warsha kwa Wabunge kuhusu Rasimu ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
Ratiba kamili ya Mkutano wa Bunge ya jinsi shughuli zitakavyowasilishwa inatarajiwa kutolewa 9/11/2011 mara baada ya kamati ya Uongozi kukutana.
Imetolewa na:
Idara ya Habari, Elimu kwa Umma, na Uhusiano wa Kimataifa
Ofisi ya Bunge
DAR ES SALAAM
No comments:
Post a Comment