Thursday, December 8, 2011

Dk. Salim: Chonde, chonde na Katiba

Watanzania wa pande zote mbili za Muungano wana nafasi kubwa ya kutoa maoni yao kwa uhuru juu ya aina ya muungano wanaoutaka, Waziri mkuu wa zamani Dk. Salim Ahmed Salim, (pichani), amesema.
“Zanzibar wana madukuduku yao, Tanzania Bara wana madukuduku yao juu ya muungano ni muhimu wakubaliane kikatiba,” alisema Dk. Salim katika mahojiano na NIPASHE yaliyofanyika Kiwengwa, mjini Zanzibar juzi.
Alisema jambo la msingi kwa sasa ni wananchi kupewa nafasi ya kutafuta ufumbuzi wa dukuduku hizo kwa njia ya mjadala utakaoendeshwa kupitia mchakato wa kuratibu maoni ya wananchi juu ya katiba mpya.
Alisema itakuwa ni vizuri kwa vyama vya siasa kujiweka kando ili kuachia wananchi nafasi kubwa zaidi kwa sababu katiba kimsingi inatakiwa iandikwe kwa kuzingatia maoni yao na matakwa yao.

Dk. Salim alisema sehemu kubwa ya kizazi kilichopo kinaundwa na kizazi kipya hivyo ni vizuri wakapewa nafasi ya kushiriki na kuamua aina ya katiba ambayo wanaamini itakidhi matarajio yao.
Akizungumzia mambo ambayo anaamini ni hatari kwa taifa, Dk. Salim alisema ni pamoja kuingiza udini na ukabila katika masuala ya siasa.
Alionya kwamba wakati Tanzania inaendelea na mchakato wa kuandika katiba mpya, haitakuwa jambo zuri kwa taasisi za nje kuingilia shughuli za upatikaji wa katiba mpya.
“Watanzania sio roboti, kila mmoja ana akili na fikira zake, muhimu kulinda umoja wetu, na wananchi hasa wa vijijini kupewa nafasi zaidi ya kutoa maoni juu ya katiba yao,” alisema Dk. Salim.
Hata hivyo, Dk. Salim alisema hashagazwi na kitendo cha kuingilia mambo ya ndani ya mchakato wa katiba kwa sababu Tanzania ni sehemu ya ulimwengu na haiwezi kujitenga kuwa peke yake.
Kuhusu miaka 50 ya uhuru, alisema Tanzania imefanikiwa kuwa na katiba yenye misingi mizuri ya viongozi kubadilishana madaraka na hivyo kudumisha amani.
Dk. Salim alishauri kuwa itakuwa ni kosa kubwa kwa Watanzania kujaribu kuwa na katiba inayoondoa ukomo wa viongozi kukaa madarakani, kwani jambo hilo linaweza kuipeleka Tanzania kwenye migogoro ya kisiasa.
Aidha, alisema Muungano wa Tanganyika na Zanzibar umeleta faida kubwa kwa wananchi wake ikiwemo kujenga misingi ya umoja wa kitaifa tangu mwaka 1964.
Alisema kwamba jambo la msingi hivi sasa ni wananchi kupewa nafasi ya kujadili kero za muungano na kutoa maoni yatakayosaidia kuimarisha muungano huo.
Kuhusu sera ya mambo ya nje ya Tanzania, Dk. Salim alisema katika kipindi cha miaka 50 ya uhuru Tanzania imefanikiwa kwa kiwango kikubwa katika kuimarisha uhusiano wake kimataifa.
Hata hivyo alisema sifa hiyo haikuja yenyewe bali ilitokana na mabalozi waliokuwa wakiteuliwa kufanyakazi kwa kuweka mbele maslahi ya taifa badala ya maslahi binafsi.
Alisema Watanzania wanaopewa nafasi za ubalozi ni vizuri wakafanyakazi kwa kuzingatia uadilifu na kujituma ili kujenga heshima kwa taifa lao.
“Huwezi kujifundisha diplomasia kwa kukaa nyumbani na kupiga soga vijiweni, pia uaminifu kwa nchi, jambo la msingi ukiwa nje ya nchi ukipata kashfa hiyo ni kashfa ya nchi yako.” alisema Dk. Salim ambaye ni mwanadiplomasia mkongwe nchini.
Alisema katika kipindi cha miaka 50 ya uhuru mataifa mengi barani Afrika na Ulaya yanatambua mafanikio ya Tanzania katika kupingania ukombozi wa Bara la Afrika pamoja na misingi ya haki za binadamu na ubaguzi wa rangi.
Hata hivyo, alisema kwamba vyama vya siasa bado vina mchango mkubwa katika kulinda na kutetea misingi ya umoja wa kitaifa katika kuadhimisha miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara.
CHANZO: NIPASHE

No comments: