Monday, April 23, 2012

Bil.28 Kusaidia Mikoa Ya Kusini
---
MRADI wa Kuimarisha Mtandao wa Maeneo ya Hifadhi Kusini mwa Tanzania utakaogharimu zaidi ya Sh Bilioni 28 (Dola Milioni 17.3) umezinduliwa mjini Iringa April 20 katika hafla iliyohudhuriwa na wadau mbalimbali.
 
Mradi huo utakaotekelezwa kwa miaka mitano kwa uratibu wa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa), unafadhiliwa kwa pamoja na serikali ya Tanzania, Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) na Mfuko wa Dunia wa Mazingira (GEF)
 
Katika shughuli ya uzinduzi wa mradi huo iliyofanyika katika ukumbi wa Veta mjini hapa, Mratibu wa mradi huo, Godwell Ole Meing’ataki alisema mradi unalenga kuboresha hifadhi ya mazingira katika maeneo yote ya hifadhi kusini mwa Tanzania ili kulinda baionuwai yake kwa maendeleo ya taifa.


Alisema mradi utajikita katika maeneo makubwa mawili yenye ikolojia inayofanana ambayo ni Ukanda wa Ikolojia wa Ruaha unaohusisa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, maeneo ya jumuiya za hifadhi za wanyamapori ya Mbomipa na Umemarua, na mapori ya akiba ya Rungwa, Muhesi na Kizigo.

Meinng’ataki alilitaja eneo la pili kuwa ni ukanda wa Ikolojia wa Kitulo- Kipengele unaohusisha Hifadhi ya Taifa ya Kitulo, pori la akiba la Mpanga Kipengele, bonde la Numbe, hifadhi ya mlima Rungwe na Bujingijila.
 
Alisema kwa pamoja maeneo hayo ya hifadhi na mapori ya akiba  na tengufu yana umuhimu mkubwa kwa maendeleo ya taifa katika kutunza vyanzo vya maji na hifadhi ya viumbe hai na mimea ya asili.
 
Awali Mkurugenzi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), Allen Kijazi alisema pamoja na mafanikio yanayoendelea kupatikana, Hifadhi za Taifa zinaendelea kukabiliwa na changamoto mbalimbali.
 
“Kuna baionuwai nyingi tu nchini zinazotakiwa kuhifadhiwa kwa sheria ya hifadhi ya Taifa lakini haziko chini ya Hifadhi za Taifa,” alisema.
 
Alisema serikali inahitaji kupanua eneo la Hifadhi za Taifa na kuyapandisha maeneo yaliyohifadhiwa (Protected Areas) kwa kuyaingiza katika Hifadhi za Taifa  ili kuboresha shughuli za hifadhi zinazofanywa na Tanapa.
 
Alisema Hifadhi za Taifa nyingi nchini zimepakana na maeneo ya hifadhi (Protected Areas) kama misitu ya hifadhi, mapori ya akiba, mapori tengufu na maeneo ya jumuiya za wanyamapori ambayo hayasimamiwi na Tanapa.
 
Alisema kiutendaji  uratibu wa kiutawala katika maeneo hayo umethibitika kuwa dhaifu na hivyo kuathiri maendeleo ya Hifadhi za Taifa.
 
Alisema udhaifu wa kiutendaji unatokana na usimamizi wa misitu mikubwa ya hifadhi kuratibiwa na Idara ya Misitu na Nyuki huku misitu mingine mingi ya hifadhi ikiwa chini ya tawala za wilaya.
 
Alisema uratibu huo una madhara makubwa kwa maendeleo ya Hifadhi za Taifa, kwa kuzingatia kwamba matatizo ya kiusimamizi katika maeneo hayo ya hifadhi yameendelea kuhatarisha baionuwai ndani ya hifadhi za taifa.


Mshauri wa Mradi huo, Paul Harrison alisema ukanda wa ikolojia wa Ruaha na Kitulo-Kipengele ni lazima utazamwe kama kitu kimoja ili kulinda baionuwai yake kwa ajili ya maendeleo ya kizazi cha sasa na kijacho.


Alisema ili baionuwai ya Kusini mwa Tanzania ihifadhiwe ipasavyo ni lazima kuwe na mfumo wa ushirikiano wa kuboresha uwezo wa usimamizi wa hifadhi hizo
Na Francis Godwin.
 

No comments: