Friday, April 27, 2012

Dk Slaa: Polisi njooni mnikamate


KATIBU Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa

Ibrahim Yamola
KATIBU Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa, amewajibu jeshi la polisi mkoani Mwanza kuwa, anawakaribisha wote wanaotangaza kutaka kumkamata kufuatia madai ya kutoa kauli za uchochezi katika mkutano wake wa hadhara uliofanyika mwishoni mwa wiki.
Kauli hiyo imekuja siku moja baada ya Jeshi la Polisi mkoani Mwanza, kutangaza kumchukulia hatua za kisheria Katibu Mkuu huyo .

Akiwa katika mkutano huo uliofanyika kwenye Viwanja vya Sahara, Dk Slaa alitoa wiki moja kwa Jeshi la Polisi mkoani humo  kuwakamata wale wote waliohusika na vurugu katika uchaguzi mdogo wa udiwani Kata ya Kirumba uliofanyika mwanzoni mwa mwezi huu.

Ilidaiwa kuwa vurugu hizo ambazo zilihusisha wafuasi wa CCM, zilisababisha kujeruhiwa vibaya kwa wabunge wa Chadema, Samson Kiwia wa Ilemela na Salvatory Mchemli wa Ukerewe.

Katika mkutano huo, Dk Slaa alisema kama Jeshi la Polisi halitawakamata watuhumiwa na kuwachukulia hatua za kisheria ndani ya siku saba,  yeye mwenyewe atachukua jukumu la kuwahamasisha wananchi wa Mwanza kuwakamata vijana hao.

Lakini jana baada ya kuulizwa kuhusu kuchukuliwa hatua na Polisi Dk Slaa alisema, “Nalikaribisha Jeshi la polisi  wakati wowote kuja kunikamata na nitafurahi kwa kuwa nafanya hivi kwa ajili ya kutetea haki za watanzania wanaoporwa uhuru wao na jeshi lao,”.
Mgombea huyo wa Urais kwa tiketi ya Chadema katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 , aliwataka polisi kabla ya kumkamata yeye waanze kuwakamata waliohusika, kuwakamata askari waliokuwapo katika eneo la tukio wakati wabunge wa Chadema wakishushiwa kipigo.

“Haiingii akilini uhalifu unafanyika na polisi wako katika eneo hilo halafu wasiwakamate watuhumiwa, kuna nini hapa katikati? Alihoji Dk Slaa.
Habari kwa hisani ya Vijimambo blog

Alisema  jeshi hilo linatakiwa kutambua tofauti ya uchochezi na kukemea kwani anachokifanya ni kueleza ukweli kwa kuwa alikuwa na majina yote ya watuhumiwa pamoja na magari yaliyotumika katika tukio hilo.

“Kama watashindwa kulifanyia kazi kwa wakati tutawasemea kwa wananchi ili wachukue hatua wenyewe” alisisitiza Dk Slaa.

Dk Slaa alifafanua udhaifu wa Polisi kwamba wamekuwa  wazito kufuatilia taarifa za hatari zinazotolewa na wananchi hasa kunapotokea matukio yanayohatarisha utulivu na amani.

“Tulishatoa taarifa kwa polisi kuwa mkoani Mbeya kuna mtu anatengeneza Dola za Marekani lakini jeshi hilo,” alitoa mfano Dk Slaa

Aliongeza, “Harakati hizi hazitakwisha hadi pale Tanzania itakapopata uhuru kwa wananchi kutosingiziwa kesi, hata tafiti zinaonyesha kuwa asilimia 50 ya watuhumiwa wanabambikiwa kesi na polisi”.

Hatua hiyo ya jeshi la polisi kutangaza kumchukulia hatua Dk Slaa imekuja baada ya Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Philipo Kalangi kusema  kauli zilizotolewa na Katibu mkuu huyo wa Chadema ni za uchochezi ambazo zinaweza kuharibu amani ya nchi.

Kamanda Kalangi alisema Jeshi la Polisi linafanya kazi kwa mujibu wa sheria za nchi na si kwa matakwa ya mtu binafsi.
Habari kwa hisani ya Vijimambo Blog

1 comment:

Tulinagwe said...

Sina imani na serikali yangu maana sielewi inakotupeleka,kila kukicha ni matatizo juu ya matatizo..lol!!HAYATI MWALIMU NYERERE TUNAKUOMBA AFUFUKE ANGALAU HATA KWA DAKIKA MOJA UFANYE KITU YA KUINUSURU HII NCHI YETU...