Thursday, April 19, 2012

Madudu Ya TBS Yanawachanganya Wabunge!


KAULI mbili zinazotofautiana zilizotolewa na mawaziri wa Wizara ya Viwanda na Biashara juu ya tuhuma zinazomkabili bosi wa Shirika la Viwango (TBS), Charles Ekerege, zimewakera wabunge ambao wameitaka Serikali itoe tamko ni kauli ya waziri upi ni ya kweli. 

Hatua hiyo ilijitokeza jana baada ya Mbunge wa Mwibara, Alphaxard Lugora, kuomba Mwongozo wa Spika kutokana na Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Cyril Chami na Naibu wake, Lazaro Nyalandu kutofautiana juu ya uchunguzi dhidi ya bosi wa TBS. 

Wakati Nyalandu anajibu swali juzi alisema uchunguzi wa CAG umekamilika na ameshawasilisha ripoti serikalini, bosi wake, Dk. Chami alisema jana uchunguzi huo haujakamilika na unaendelea kufanywa na CAG. 

Ekerege anatuhumiwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mashirika ya Umma (POAC) na ile ya Hesabu za Serikali (PAC) kuweka kampuni hewa za kukagua magari nje ya nchi na hivyo kuingizia hasara ya Sh bilioni 30 ambazo zimeainishwa katika ripoti ya CAG. 

Baada ya Lugora kumaliza kuomba mwongozo, alisimama Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi aliyesema ni kweli majibu ya mawaziri hayo hayafanani na Serikali imeliona hilo, na Ofisi ya Waziri Mkuu itakusanya ushahidi wote juu ya jambo hilo na itatoa taarifa bungeni. 

Lakini Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba (CCM) alihoji kwa nini Serikali inashindwa kutoa majibu ya uhakika juu ya suala hilo wakati wabunge wanachotaka kufahamu ni kauli ipi yenye ukweli. 

Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (Chadema) alisema kamati yake anayoiongoza ya Mashirika ya Umma iliunda kamati ndogo kushughulikia tuhuma zinazomkabili Ekerege na tayari wameshawasilisha taarifa kwa spika ambaye anatakiwa aipeleke Ofisi ya Waziri Mkuu ili walete taarifa ya utekelezaji bungeni. 

Kwa upande wake, Naibu Spika Job Ndugai alikiri kuwa jambo hilo ni la muda mrefu umefika wakati liishie kwa kupatiwa ufumbuzi kwani linawapaka matope wabunge bila sababu za msingi.
 Chanzo: Habari Leo

No comments: