Wananchi kadhaa wametoa maoni tofauti kuhusiana na uamuzi wa Mahakama Kuu kumvua ubunge Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam Dk. Azaveri Lwaitama, amesema uamuzi huo hauwezi kumzuia Lema kushinda tena katika uchaguzi wa marudio.
Alisema aliyekuwa mgombea wa CCM katika uchaguzi wa jimbo hilo Batilda Burian ambaye kwa sasa ni Balozi wa Tanzania nchini Kenya, alikuwa anapigiwa debe na vigogo, lakini alishindwa kwa kura nyingi na Lema.
Aidha, alisema hata Sioi Sumari aliyegombea Arumeru Mashariki alikuwa kambi ya Lowassa na akashindwa.
Pia alisema wananchi wa Arusha Mjini hawatabadilisha mawazo na kumchagua mtu mwingine atakayesimama na Lema katika uchaguzi wa marudio kwani wanaonyesha jinsi gani wanakikubali Chadema.
Naye Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana, alisema kila mtu ana nafasi ya kukimbilia mahakamani kwa kuwa hiyo ni demokrasia na kuongeza kuwa Chadema hakina haja ya kukimbilia mahakamani kwa kuwa kwenye uchaguzi wa marudio kitashinda.
Alisema katika uchaguzi uliopita katika Jimbo la Arusha Mjini, Chadema iliongoza kwa kura nyingi na kuiacha CCM na kwamba kadri siku zinavyozidi kwenda, chama hicho tawala kinapoteza wapiga kura wao wengi pamoja na umaarufu wake.
Baadhi ya wahadhiri wa vyuo vikuu vya Dodoma, wamesema hawajafurahishwa na kitendo cha kurudiwa kwa uchaguzi wa Jimbo la Arusha Mjini, kwa sababu ni kudidimiza nchi kiuchumi.
Makamu wa Chuo cha St. John (Taaluma), Profesa Eginald Mihanjona na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udomasa), Paul Loesulie, walisema uchaguzi mdogo unaisababishia nchi gharama kubwa.
“Tanzania ni masikini sana hakuna fedha za kuendesha uchaguzi wa mara kwa mara na kufanya hivyo ni kuididimiza nchi katika umasikini,” alisema Profesa Mihanjo.
Pia alitaka Watanzania kuliangalia jambo hilo katika mchakato wa Katiba mpya ili utafute utaratibu mwingine inapotokea kutenguliwa kwa ushindi ili kuepusha gharama hizo.
Aliwataka wananchi wa jiji la Arusha kutulia na kutoingilia maamuzi yaliyotolewa na Mahakama Kuu wakati wakisubiria kutangazwa kwa uchaguzi mdogo.
Kauli hiyo iliungwa mkono na Loesulie ambaye alisema hafurahishwi na kurudiwa kwa uchaguzi huo kwa sababu nchi inaingia katika gharama nyingine na kuleta usumbufu kwa wananchi.
Hata hivyo, alisema: “Lakini ninachojua kilichokuwa kikipingwa (si idadi ya kura ila ni kashfa…Itupe fundisho wanachama, Watanzania na wagombea kuwa makini wakati wa kampeni za uchaguzi ili kuepuka usumbufu kama huu.”
Kwa nini Dk. Burian hakulalamika?
Wakazi kadhaa mkoani Iringa, wamesema hukumu hiyo inashangaza kwa kuwa shahidi mkuu wa Jamhuri ambaye anadaiwa kudhalilishwa hakutokea mahakamani kueleza jinsi alivyodhalilishwa.
Badala yake wamekishauri Chadema kutokata rufaa ili Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) itangaze kwamba kiti hicho kipo wazi na kuitisha uchaguzi ili wakazi waamue tena kama walivyokitendea haki chama hicho mwaka 2010.
Mhadhiri wa Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Ruaha (RUCo) ambaye pia ni Wakili wa kujitegemea, Rwezaura Kaijage, alisema:
“Tunaamini daima kwamba Mahakama ndiyo sehemu ya kutenda haki, lakini nazo zinaongozwa na akili za kibinadamu. Kwa hiyo nawashauri Chadema hata kama wanayo haki ya kukata rufaa wasifanye hivyo, badala yake waachanane nayo ili uamuzi wao uilazimishe Tume ya Taifa ya Uchaguzi itangaze tena nafasi hiyo na Chadema waweze kudhihirisha nguvu ya umma ni suluhisho la migogoro ya kisiasa.”
Mchambuzi wa masuala ya siasa, uchumi na biashara, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Frank Mwaisumbe, alisema:
“Sina shaka na uamuzi wa Mahakama, tatizo kubwa nililonalo ni walalamikaji ambao walifungua kesi hiyo wanaonekana walitengenezwa kupanda vita ya kisiasa pasipokujua kwamba maamuzi hayo yatamwongezea umaarufu wa kisiasa Lema na kuwafanya wananchi waamini kwamba Chadema kinaonewa. Na ukiangalia anayedaiwa kudhalilishwa hakufungua kesi jambo ambalo litaongeza chuki dhidi ya chama tawala na serikali yake.”
Alisema uamuzi huo utaongeza ari ya wananchi kupambana na CCM hata kama uchaguzi huo utarudiwa karibuni.
MHADHIRI MUCCOBS: DEMOKRASIA NI GHARAMA
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Ushirika na Biashara (MUCCoBS), Prof. Suleiman Chambo, alisema kwa kawaida demokrasia ni ghali hivyo ni lazima fedha zitumike vinginevyo fujo zitatokea.
“Suala la kuvuliwa ubunge au kutovuliwa hilo ni la Jaji husika aliyetoa uamuzi, kwa sababu ametoa hukumu kutokana na ushahidi uliotolewa mahakamani,” alisema.
Naye, Joseph Chuwa, mkazi wa mjini Moshi, alisema uamuzi huo ni fundisho kwa wanasiasa kuwa makini wakati wa kampeni zao na kutumia lugha nzuri na si matusi, lakini pia alisema serikali itafakari kwa kina kwani gharama za uchaguzi mdogo ni kubwa huku wananchi wakikosa huduma muhimu.
“Katiba mpya izingatia suala hili la uchaguzi mdogo, zinatutia gharama kubwa huku hospitali zikiwa hazina huduma muhimu, hivi majuzi tumetoka kwenye mgomo wa madaktari kwa sababu ya maslahi duni, sasa fedha zinaenda kutumika tena kwenye uchaguzi mdogo,” alisema.
Waziri wa Elimu wa Serikali ya Wanafunzi ya Chuo Kikuu cha Teofilo Kisanji (Tekuso), Milanzi Petro, alisema mahakama ndiyo mwamuzi wa mwisho, anakubaliana na uamuzi wake, lakini kwa upande mwingine imewaumiza wananchi wa Arusha na Watanzania kwa ujumla.
Alisema kuwa Lema hakuwa mbunge wa kwanza kutumia matusi kwenye kampeni na kuwa wakati mwingine matusi na vijembe huwa ni hulka ya binadamu inayokuja kwa bahati mbaya. Alisema kuwa kama tatizo lilikuwa ni matusi aliyoyatoa Lema jukwaani, ilipaswa mahakama kutumia busara kwa kukutanisha pande mbili na kumaliza tatizo bila kutengua matokeo ya uchaguzi.
Mwanafunzi wa sheria aliye mwaka wa mwisho katika Chuo Kikuu HuriaTanzania (OUT) Tawi la Mbeya, Eddo Mwamalala, alisema ingawa mahakama haipaswi kuingiliwa katika maamuzi yake, lakini kwa uamuzi huo wa kutengua matokeo ya uchaguzi Jimbo la Arusha Mjini imebaka demokrasia.
Alisema kuwa Lema alikuwa mbunge aliyechaguliwa kwa kura nyingi na wananchi wa Arusha na pia alikuwa ni kioo cha vijana wanaopenda demokrasia, hivyo kwa uamuzi huo mahakama imewaliza wengi.
Mwenyekiti wa mtandao wa wasomi mkoa wa Mbeya, Prince Mwaihojo, alisema amesikitishwa na uamuzi huo kwa kuwa msimamo wake ni kutaka vyama vya upinzani viwe na nguvu.
Mwenyekiti wa Chama cha NCCR Mageuzi Wilaya ya Rungwe, Anyimike Mwasakilali, alisema hali ilivyo katika Jimbo la Arusha, Chama cha Mapinduzi (CCM) hakiwezi kupata ushindi kwasababu Chadema wameshajua mbinu chafu zinazofanywa na chama tawala kupata ushindi.
Mwasakilali ambaye pia ni Diwani wa Chadema kata ya Kawetele Tukuyu mjini, alisema vyombo vya sheria lazima viwe vinaangalia suala la kesi za kupinga matokeo ya ubunge na udiwani kwa makini kwasababu wananchi wanapokuwa wamechagua wanakuwa wametumia demokrasia yao kumchagua mtu wanayemtaka.
Mwanachama wa CCM John Mwakila mkazi wa Vwawa wilaya Mbozi, alisema kurudia uchaguzi katika jimbo la Arusha yatakuwa ni matumizi mabaya ya fedha kwasababu uwezekano wa CCM kupata ushindi ni mdogo. Mwenyekiti wa APPT Maendeleo Mkoa wa Mbeya, Godfrey Davis, alisema pamoja na kwamba sheria imefuata mkondo wake lakini hata hivyo kabla ya kutolewa hukumu hiyo vyombo vya sheria vilipaswa kuliangalia suala hilo kwa undani zaidi.
Davis alisema, mahakama ndiyo sehemu ya kutenda haki lakini hata hivyo Chadema wasikate rufaa badala yake waiache Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) itangaze tena kuwa jimbo hilo lipo wazi.
Aidha baadhi ya wananchi mkoani Mbeya wamesema NEC itakapoitisha uchagazi huo watajitolea kwenda Arusha kusaidia kampeni za Chadema
Mkazi wa Mwanza, Jared Ghachocha, amesema uamuzi huo unamaanisha kufanyika kwa uchaguzi mwingine mdogo hali ambayo itaathiri uchumi wa nchi kutokana na gharama zitakazotumika.
Hata hivyo, Ghachocha ambaye ni Mkuu wa wilaya mstaafu, alisema hiyo ndiyo gharama ya demokrasia, hivyo si rahisi kuepuka hali hiyo, na kwamba mahakama kama mhimili wa nchi imetimiza wajibu wake kwa mujibu wa sheria. Emmanuel Luanda, Mwanajeshi mstaafu, alisema hapingi uamuzi wa mahakama, lakini akasema kuwa ipo haja kwa serikali kutafuta njia mbadala ya kupata mwakilishi wa jimbo husika pale mbunge aliyepo anapofariki au ushindi wake kutenguliwa.
Alisema si busara kuendelea kufanya chaguzi ndogo ilhali taifa linakabiliwa na matatizo mengi, ukiwemo uhaba wa nishati ya umeme, miundombinu mibovu na kupanda kwa gharama za maisha.
Badala yake alishauri kwamba inapokuwa imebaki miaka mitatu ni vema jimbo lililo wazi kwa sababu zozote zile likawakilishwa na mbunge wa jimbo jirani.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chadema Mkoani Mwanza, Jane Kajoki, alisema hakufurahishwa na kudai uamuzi huo ni njama za makusudi zilizofanywa kwa lengo la kunufaisha kundi fulani la watu kwa hasara ya wananchi wengi.
Alifafanua kwamba kama ni kampeni za matusi zimekuwa zikifanywa na wagombea wengi wakiwemo wa CCM, hivyo haipaswi kuwa sababu ya msingi ya kutengua ushindi wa Lema.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (Sua), Dk. Clavery Tungaraza, alisema ingawa hajapitia hukumu hiyo, lakini kama ilithibitika alitoa lugha chafu wakati wa kampeni, alipaswa kuvuliwa madaraka hayo, lakini kama sheria hiyo imepindishwa kwa lengo la kuwakomoa watu wa kundi fulani, litakuwa tatizo.
Dk. Tungaraza alisema sheria hiyo pia ingepaswa kutumika wakati wa kampeni kabla na hata kufanyika kwa uchaguzi sambamba na kuwachukulia watu waliotoa matusi akiwemo Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde ambaye alitoa matusi ya wazi katika kampeni za uchaguzi wa Jimbo la Arumeru Mashariki.
“Kwa sheria tunavyojua hata ukitukana hadharani unashtakiwa, sasa tunataka na Lusinde naye ametukana hadharani, kila mtu amesikia katika kampeni za uchaguzi Arumeru Mashariki naye avuliwe ubunge,” alisema Dk. Tungaraza.
Mwanafunzi wa mwaka wa pili katika Chuo Kikuu cha Mzumbe, Ally Bwakira, alisema pamoja na Lema kuvuliwa ubunge, bado kuna ngome kubwa ya Chadema katika jimbo hilo na kwamba litarudi tena kwa chama hicho.
“Arusha ni ngome ya Chadema kwa hiyo hata wafanyeje linarudi watu wameshaichoka CCM na ahadi zake zisizotekelezeka,” alisema Bwakira.
Imeandikwa na Godfrey Mushi, Iringa; Sharon Sauwa na Jacqueline Massano, Dodoma; Salome Kitomari; Moshi, Ashton Baraigwa; Morogoro; Thobias Mwanakatwe na Emmanuel Lengwa, Mbeya; George Ramadhan, Mwanza na Samson Fridolin, Dar.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment