Friday, May 25, 2012

DKT.BILAL AMWAKILISHA RAIS KATIKA MKUTANO WA MAENDELEO ENDELEVU AFRIKA JIJINI GABORONE, BOTSWANA.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Mohammed Gharib Bilal akihutubia kwenye mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Maendeleo Endelevu katika Bara la Afrika mjini Gaborone.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Mohammed Gharib Bilal akizungumza na Rais wa Liberia Bibi Ellen Johnson Sirleaf kwenye mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Maendeleo Endelevu Barani Afrika mjini Gaborone.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Mohammed Gharib Bilal akiwa katika picha ya pamoja na Wakuu wa Nchi pamoja na wawakilishi  kutoka nchi za Afrika waliohudhuria mkutano wa Maendeleo Endelevu katika Bara la Afrika.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Dkt. Mohammed Gharib Bilal amemwakilisha Rais Jakaya Kikwete katika mkutano wa Maendeleo Endelevu Afrika unaolenga katika kujumuisha thamani ya Rasilimali Asilia katika kupima maendeleo ya kiuchumi katika nchi za Afrika.
Katika mkutano huo, Tanzania imeunga mkono kuanzishwa kwa mfumo wa kujumuisha thamani ya raslimali asilia ambao utahusishwa kwenye tathmini ya pato la taifa kwa manufaa ya vizazi vya sasa na  vijavyo.
Makamu wa Rais alisema wakati akihutubia mkutano huo leo Alhamis Mei 24, 2012 kuwa, mchango wa rasilimali asilia zina nafasi kubwa katika kuchangia katika pato la taifa lakini ili mchango wake utambulike, nchi zinahitajika kuwa na utaratibu wa kuzifanyia tathmini hasa kuhusu matumizi yake na faida zake katika uchumi huku pia athari zake zikitazamwa hasa zile zinazotokana na kupoteza uhalisia wa mazingira ama kuharibu mazingira ya nchi.
“Ni imani ya serikali ya Tanzania kuwa mpango huu utasaidia kutoa nafasi ya nchi kujikagua hasa kwa kuzingatia rasilimali zinazotumika na faida inayopatikana. Tena mpango huu utatoa nafasi kwa nchi kujiuliza kama matumizi ya rasilimali zake yanalenga kutambua faida ya sasa na siku zijazo ili kuhakikisha kuwa mazingira yanabakia kuwa salama kwa ajili ya vizazi vijavyo,” anasema Mheshimiwa Makamu wa Rais Katika hotuba yake.
Kwa mujibu wa Makamu wa Rais, dhana ya kutathmini mazingira na kujumisha raslimali asilia kwenye hesabu za pato la taifa, kunaweza kusaidia nchi kufikia maamuzi ambayo yataliwezesha taifa kupata maendeleo endelevu hali ambayo itachangia jitihada za kupunguza umaskini na kukuza uchumi.
“Tathmini ya hesabu kuhusu maendeleo, ukijumuisha na hesabu za raslimali asilia, zinaweza zikatupa takwimu za kina kwa ajili ya kusimamia vizuri uchumi,” anaeleza Makamu wa Rais na kuongeza:
“Tena kwa upande mwingine, hesabu za mapato katika sekta za maji, nishati na nyinginezo, udhibiti wa uchafu wa mazingira na hali kadhalika matumizi makubwa ya raslimali zinahitajika ili kukuza uchumi na wakati huo huo zikitakiwa kufanyiwa tathmini ya faida zake na hasara kwa mazingira na hali ya nchi katika miaka ijayo.”
Katika mkutano huo, pia kumejadiliwa suala la umuhimu wa serikali za nchi za Afrika kutazama  upya sera na mikakati ya nchi hizo na kuweka  mikakati inayolenga katika kutunza mazingira ambayo itawezesha kupata maamuzi ya busara  yatakayohakikisha upatikanaji wa maendeleo endelevu.
Dkt. Bilal anaueleza mkutano huo kuwa, Tanzania iliona umuhimu wa raslimali asilia tangu nchi ilipopata uhuru mwaka 1961 ambapo iliweza kutenga asilimia 30 ya eneo la nchi kwa ajili ya wanyama na viumbe hai. Tena ziliwekwa sera nzuri zilizolinda uvunaji wa raslimali hizo kwa manufaa ya taifa.
“Dunia hivi leo inakabiliwa na matumizi yasiyo endelevu ya raslimali asilia. Tumemaliza benki ya raslimali asilia kwa kuwa matumizi yamekuwa makubwa zaidi kwenye uvuaji wa samaki, uvunaji wa misitu, hewa iliyopo na vingine vingi vilivyobaki. Mbaya zaidi, tumekuwa tukitumia vibaya raslimali hizo wakati zaidi ya watu bilioni moja wanaishi katika umaskini uliokithiri, “ anasema
Makamu wa Rais ameueleza mkutano huo pia kuwa, nchi nyingi za Afrika zinategemea kilimo kama njia kuu ya uchumi na sekta hii bado inategemea mvua huku ikihusisha wakulima wadogo wadogo hali ambayo inaonesha ma mazingira yataharibiwa ni wazi maisha ya wengi yataathirika. Anasisitiza kuhusu kuwepo kwa mfumo mpya wa kilimo unazingatia kutoharibu rasilimali asilia na wakati huo huo kuhakikisha kuwa mazingira yanabaki kama yalivyo ili yasaidie jamii zijazo.
Akifungua mkutano huo, Rais Seretse Khama Ian Khama wa Botswana alisema nchi yake imeandaa mkutano huo kwa lengo la kutaka kuzungumzia masuala ya Afrika kwa pamoja juu ya maendeleo endelevu na kuangalia namna nchi hizo zinavyoweza kutumia utajiri wa raslimali za asili katika kukuza maendeleo ya nchi zao.
Katika mkutano huo, Tanzania na Botswana zimepongezwa kwa uhifadhi wa maliasili na mazingira kwa ajili ya kizazi cha sasa na cha baadaye.
Mkutano huo wa pia unahudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka nchi zipatazo 11 wakiwemo Marais Hifikupenye Pohamba wa Namibia, Bibi Ellen Johnson Sirleaf wa Liberia, Waziri Mkuu wa Msumbiji na nchi .
Mkutano huu ni maandalizi ya mkutano wa Mazingira wa Rio +20 unaotarajiwa kufanyika nchini Brazil mwezi ujao katika jiji la Rio de Janeiro. Maazimio ya mkutano huu yanalenga nchi za Afrika kushiriki mkutano huo zikiwa na sauti moja kuhusu utunzaji wa mazingira na pia kukabiliana na tabia ya uharibifu mkubwa wa mazingira hasa unaofanywa na nchi tajiri duniani.
 Imetolewa na:  Kitengo cha Habari
                 Ofisi ya Makamu wa Rais
              Alhamisi – 24/5/2012   

No comments: